Kuna kibao chake kimoja kinasema Roho Yangu. Kwa sisi wapenzi wa Bongo Fleva, huu ni moja kati ya tunzi zenye kuelimisha, achilia mbali burudani nzuri inayopatikana ndani yake. Katika mstari mmoja miongoni mwa versi, unasema ‘Ukiwa mjanja kuchapiwa ni siri ya ndani.’
Sina uhakika ni watu wangapi wanajua maana ya msemo huu, lakini kwa wale ambao huenda wanapata taabu kidogo, ni kwamba ikitokea umebaini kuwa mwenza wako amechepuka na wewe umegundua, hili si jambo la kuanza kulitangaza kwa marafiki na majirani, bali ni wakati muafaka, wa kulifanya kuwa la kifamilia zaidi.
Utatoka nje ya nyumba yako na kukimbilia kwa marafiki au majirani na kumshitaki mwenza wako jinsi alivyo mchepukaji. Katika hatua za awali, akili yako itaamini kabisa kuwa unajiweka katika nafasi salama na tena, kujaribu kujionyesha kuwa wewe ni mtu safi, unayetiwa dosari na mwenzako.
Ni sawa, lakini nikuambie kitu, sisi, kwa maana ya waswahili, hatuna wema unaodhani tunao. Utajikimbiza hadi kwa shoga yako na kumwelezea jinsi mume au rafiki yako alivyokusaliti kwa kushiriki mapenzi na mtu mwingine. Bila shaka utaomba ushauri, ufanye nini, umuache, mzungumze mbele yake au kwa mjumbe, ama mkakae wenyewe na kujadili.
Labda niongeze kitu kingine, kukimbilia kwa mashoga, majirani na wajumbe hakuishii tu kwenye mambo ya kimapenzi. Yapo mambo mengine pia ya kifamilia ambayo tunadhani hatuwezi kuyamaliza wenyewe pasipo kuwashirikisha watu wa nje.
Mathalani, mume kuwa na mkono wa birika katika kumpendezesha mkewe, mume kuwa mnywaji wa kupitiliza, mke kupenda kugawa vitu ovyo vya ndani, mke kupenda umbeya, mume kukaa vijiweni, mke kuwa na mazoea na vijana wa kiume na mambo mengine chungu nzima kama tunavyojua huko mitaani!
Haya yote, yanajadilika ndani ya nyumba au chumba chenu. Hakuna kitu chochote cha kifamilia kinachoweza kuwa nje ya baba na mama. Nasisitiza, hakuna.
Iko hivi, mnaweza kuwa katika ugomvi mkubwa baina yenu, mkawahusisha wazazi au hata ndugu wengine wa karibu. Lakini mwisho wa siku, wote hao, watataka mshikane mikono, msameheane.
Unajua kwa nini inaishia hivi, ni kwa sababu hakuna mbabe yeyote duniani anayeweza kuwalazimisha nyinyi kuishi pamoja. Sasa basi, mtaenda huko mnakoenda, mnatoleana siri zenu, mnadhalilishana, halafu mwisho wa siku mnaambiwa mshikane mikono msahau tofauti zenu!
Lakini wakati mnasameheana, tayari watu wa nje wameshajua udhaifu wenu, mmeshawapa faida na wanatumia nafasi hiyo kuwang’ong’a.
Kumbe ingewezekana kabisa kabla ya kutoka nje na kuwaalika watu, mngeweza kukaa wenyewe na kuzungumza na kuzimaliza tofauti zenu. Usije ukaniambia baba flani haambiliki, siyo kweli. Hujamjulia tu, hakuna mtu anayependa nyumba yake iwe ya moto, kila mara wote tunapenda nyumbani pawe sehemu salama.
Unachopaswa kufanya ni kupima tu upepo. Kama mke au mume wako ana kawaida ya kukasirika siku tatu au wiki baada ya kukwaruzana, subiri muda huo upite, halafu muombe muda wa kujadiliana naye, kisha mweleze jinsi gani, anavyokunyima furaha kwa matendo yake.
Binadamu ana hulka ya kutaka kuheshimiwa, hata kama ni mkosefu. Ukimweleza kosa lake taratibu, kwa upole, atakuelewa tu. Na ili jambo hili mlimalize vizuri, msitafute mshindi. Hakuna mtu anayekubali kushindwa mbele ya mwenza wake, hasa tunapotoka katika kukwaruzana.
Narudia na kusisitiza, malizeni tofauti zenu ndani ya nyumba, mjifungie, ongeeni kwa sauti za chini, kila mtu aonyeshe heshima kwa mwenzake, mwisho wa siku, mtaishia kicheko na maisha yenu yataendelea kuwa raha mustarehe!
GPL
No comments:
Post a Comment