“Vipi Mwali mbona leo umekuwa dalali wa matusi kulikoni?”
“Anti Naa, wee acha, kweli tunapokwenda kubaya, safari hii potelea mbali namroga mtu.”
“Kwa nini?”
“Haiwezekani mtu anichukulie mume kisha anitukane, nimemkosea nini?” Mwali alisema huku akiporomosha machozi ya uchungu.
Nilipotaka ukweli, niliambiwa kuna mwanamke mmoja anatembea na mumewe bila yeye kujua. Tokea yule mwanamke alipomjua yeye ni mke wa hawara yao amekuwa hana raha, kila kukicha kumtumia ujumbe wa matusi pia hata wengine kumtangazia wana ujauzito wa mumewe.
Amekuwa akikosa raha kila siku kutokana na vitimbi anavyofanyiwa na wanawake hao. Alichosema kila akimuuliza mumewe humwambia achana nao lakini anachoshukuru upendo wa mumewe ambaye ni dereva wa gari za kwenda nje ya mkoa ni mkubwa. Alisema kwanza alivumilia lakini sasa yamemfika shingoni na kuamua naye kurudisha makombora ya maneno machafu.
Mmh! Kweli maji yalikuwa shingoni, lakini napenda kuwaeleza wanawake wote walio ndani ya ndoa zao kutowapa nafasi wanawake waliokosa heshima na kujua nini thamani ya ndoa.
Jamani wewe kama hujaolewa hebu heshimu ndoa ya wenzako. Hata kama makosa kafanya mumewe kutoka nje ya ndoa, yeye ana kosa gani? Kabla sijamjibu ningependa kuwahabarisha wanawake wote wanaoingilia uhusiano wa watu, wajaribu kuziheshimu ndoa za wenzao, si busara kumtukana mke wa mtu, kama ungekuwa bora ungeolewa wewe, umenipata hapo?
Wengi wenu huwa hampendi ndoa, mnatanguliza starehe mbele na kufanya ugeuzwe chombo cha starehe na si mwanamke wa kuolewa.
Hebu nikuume sikio muolewaji, ni kosa kubwa kujibizana au kutukanana na mtu aliye nje ya ndoa yako, hiyo ni kumpa kichwa na kuamini ameweza kukuchokonoa na likakugusa.
Nikuibieni siri, wote walio ndani ya ndoa, kupatwa na masahibu ya kusumbuliwa na mahawara za waume zenu. Hizo ni kelele za mkosaji, kupenda kwake starehe leo kumemfanya awe jamvi la mtaa, kapata raha kidogo kwa mumeo kachanganyikiwa sasa anataka kuingia ndani kabisa.
Hebu zichukulieni kelele zao kama mbu walio nje ya chandarua, wasio na uwezo wa kuwauma zaidi ya kupiga kelele, siku zote kelele za mbu hazikunyimi usingizi. Ushauri wangu kwenu kila anapotokea mtu wa kukutukana kwa vile tu wewe umeolewa na yeye kuachwa solemba hiyo si juu yako bali ya mumeo.
Kujiepusha na mtu huyu kwa kukaa kimya usimjibu kwa vile wewe umeishapata, ukimya wako ni pigo zito kwake kuliko kutukanana naye. Muache abwabwaje mwisho wake atachoka kama mbu nje ya chandarua, atakufa kwa kihoro, siku zote wakerekwao hufa siku si zao.
Mwisho nazungumza na ninyi wanaume msiojua thamani ya mwanamke ndani ya ndoa. Ni kosa kubwa kumlinganisha mkeo na hawara, kufanya hivyo ni kumdhalilisha mkeo. Mkomeshe hawara yako amheshimu mkeo kwani kama angekuwa yeye ni bora angemuweka yeye ndani.
Mwanaume mwenye tabia hizo ni zaidi ya mnyama, hufai kuwa baba wa familia. Kama ulikuwa bado una tamaa zako za mwili kwa nini ulikimbilia kuoa? Mjengee heshima mkeo ambaye ana dhamana kubwa mbele ya Mungu. Na wewe uliye nje ya ndoa heshimu ndoa ya mwenzako, kuiba penzi si kibali cha kuingilia ndoa ya mtu, usiwe hayawani uliyekosa mkia.
Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.
GPL
No comments:
Post a Comment