Kwako Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.
Ni matumaini yangu kwamba unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku ambayo yanakufanya uwe bize muda mwingi. Najua itakuwa vigumu kuonana na wewe kwa mara nyingine tangu tulipoonana siku ulipotembelea chumba chetu cha habari. Hata hivyo, hiyo hainizuii kukufikishia ujumbe wangu kwako.
Mheshimiwa, mimi siyo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum wa Dar es Salaam kama wewe, sina cheo wala ujuzi wowote wa kipolisi, hata kushika bunduki tu sijui. Sijawahi kushiriki kwenye oparesheni yoyote ya kupambana na majambazi kama wewe.
Sijawahi kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya na mikoa mingine kadhaa kama wewe. Mimi ni raia wa kawaida kabisa, nisiye na chochote cha maana. Hata hivyo, ningekuwa mimi ndiyo wewe, nakuhakikishia ningetazama upya ufanisi wangu katika kutimiza majukumu ya kipolisi na kuwaongoza walio chini yangu.
Ndiyo, ningetazama kwa jicho la tatu hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam na kuangalia jinsi ninavyotimiza majukumu yangu ya kila siku kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu.
Ningekaa na kutafakari kwa mapana tukio lililotokea hivi karibuni, la kundi ya vijana wadogo wahalifu wanaojiita Panya Road, kutingisha Jiji la Dar es Salaam Januari 2, mwaka huu na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wake.
Siku ya tukio, ulinukuliwa ukizungumza na vyombo vya habari, ukisema kwamba tatizo la Panya Road kuvamia wananchi, kuwajeruhi na kuwapora usiku huo, halikuwa kubwa kama watu walivyokuwa wakifikiria.
Ukanukuliwa ukisema kuna kundi la watu linakuza tatizo hilo kwa kutumia mitandao ya simu na mitandao ya kijamii na kulifanya lionekane kuwa kubwa sana. Kama lengo la kauli yako lilikuwa ni kuwatuliza watu, basi ilikuwa ni sahihi kuzungumza hivyo.
Lakini kama lengo lako lilikuwa ni kusema ukweli, hakika ulichemka na kilichofuatia baada ya hapo, kinadhihirisha hili. Siku chache baadaye, msemaji wa jeshi la polisi alinukuliwa akisema zaidi ya vijana 510 walikamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Huhitaji kuwa na elimu ya chuo kikuu kugundua kwamba vurugu inayoweza kusababishwa na zaidi ya vijana 510, itakuwa na ukubwa wa kiasi gani. Kamanda, taarifa zilizozagaa siku ya tukio zilikuwa zinaeleza kwamba maeneo ya Magomeni, Sinza, Tabata, Kijitonyama, Kimara, Mwananyamala, Kinondoni, Tegeta, Manzese, Ubungo, Kigogo, Temeke, Gongo la Mboto, na Buguruni, yote yalikuwa yamevamiwa na vijana hao na kusababisha taharuki kubwa.
Wananchi wa maeneo hayo, walikuwa mashahidi wa jinsi kulivyotokea taharuki usiku huo. Wewe ukasema kwamba tatizo halikuwa kubwa bali lilikuwa linakuzwa, baadaye jeshi la polisi likatangaza kuwashikilia zaidi ya vijana 600 kwa kuhusika na tukio hilohilo, huoni kama kuna mkanganyiko hapo?
Ukubali ukatae, Panya Road ni tatizo jijini Dar es Salaam. Ninachojiuliza, wewe na jeshi lako mlikuwa wapi kwa kipindi chote hicho mpaka vijana hao wanajikusanya, wanatafuta silaha na kuanza kuingia mitaani?
Jeshi lako lilikuwa na taarifa juu ya uwepo wao kabla ya siku ya tukio? Kama taarifa zilikuwepo, nini kilifanyika kuzuia tatizo lisitokee? Baada ya tukio kutokea usiku huo, jeshi la polisi lilichukua hatua gani za haraka kukabiliana nao zaidi ya wewe kusikika na kuonekana kwenye runinga ukisema tatizo lilikuwa limekuzwa?
Mtu yeyote akijiuliza maswali haya, lazima aanze kuwa na shaka na utendaji wako na jeshi zima la polisi, kwamba mnafanya kazi kama zimamoto. Hata wewe mwenyewe ukijiuliza, utaanza kuelewa ninachomaanisha. Hivi kwa mfano, ingekuwa vijana hao wanatumia bunduki, ni watu wangapi wangeathirika usiku huo?
Makundi ya vijana wanaofanya uhalifu wapo kwa wingi, nenda kwenye fukwe za Bahari ya Hindi nyakati za jioni maeneo ya Kunduchi, Msasani, Kawe mpaka Coco uone jinsi wananchi wanavyohenyeshwa kwa kukabwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao.
Sasa wakati haya yanafanyika, wewe kazi yako kubwa ni nini? Vijana wako wanafanya kazi gani? Yapo madai pia kuwa polisi wako wanavamia watu hata kwenye mechi za mpira wa miguu kama ilivyokuwa Uwanja wa Vinyago Mwenge Dar Jumatano iliyopita na kukamata watu ili ionekane polisi wamekamata Panya Road wakati walikuwa ni raia wema! Hii ni kasoro ingine, iangalie!
Wasalaam.
CREDIT:GPL
1 comment:
Mkuu kwa hilo naunga mkono kuwa tatizo lipo kwa huyu Kova..utendaji wake wa kazi sio sahihi kuna haja ya mabadiliko makubwa katika jeshi la polisi
Post a Comment