HAKUNA ladha inayopendwa na mashabiki wa muziki Bongo kwa sasa kama Bongo Fleva. Zipo nyimbo nyingi ambazo zinapita masikioni mwa mashabiki na kufurahia lakini kizuri zaidi ni jinsi video za Bongo Fleva ambazo zimekuwa zikija kimataifa kila siku.
Unapotaja kati ya video za muziki huo ambazo zipo juu kwa sasa ni wazi utataja moja kwa moja video za staa wa nyimbo hizo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kama vile Mdogomdogo, Nitampata Wapi, My Number One ambazo zote amezifanyia nchini Afrika Kusini.
Achana na video, twende kwenye shoo zake, Diamond ametokea kuteka majukwaa mbalimbali kwa kujaza nyomi ya watu. Miongoni mwa shoo zilizofanya poa ni pamoja na shoo za funga na fungua mwaka ambazo ni Usiku wa Wafalme iliyofanyika katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala-Zakhem, jijini Dar pamoja na ile iliyofanyika Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.
Je, Nyuma yake unajua kuna nani?
WCB kwa kirefu unaweza kuwaita Wasafi Classic Baby.
Kruu nzima ya WCB bado inaendelea kumfanya Diamond awe bora zaidi kwenye kila video hadi shoo. Katikati ya wiki hii, WCB ikiongozwa na meneja wao, Babu Tale walitinga katika mjengo wa Global Publishers uliopo Bamaga, Mwenge ambapo walifunguka mengi mbele ya waandishi wa mjengoni hapo.
Kwanza kabisa kuna Rais wa Wasafi, Diamond, chini yake kuna mameneja watatu wanaomuongoza ambao ni Babu Tale, Said Fella na Salam.Diamond hawezi kuamua mwenyewe avae nini aende wapi au afanye nini, kuna Q-Boy Msafi na Morgan ambao wapo kwa ajili hiyo. Baada ya hapo kuna msemaji wa kati ambaye pia ni DJ kwenye shoo zote tunazokwenda, Romy Jones.
WCB pia inaundwa na madansa nane ambapo wanaume wapo sita na wasichana wawili. Baada ya madansa kuna baunsa anaitwa Mwarabu Platnumz na hayupo kwa ajili ya kumuangalia Diamond tu bali yupo kuwaangalia WCB kwa ujumla. Ukiachana na baunsa kuna wapiga picha watatu lakini ambao tunasafiri nao ni wawili tu.WCB jumla inaundwa na watu 16.
Kifupi sitaki kumsifia Diamond, lakini hakuna kitu chochote unachokiona kimeruka cha WCB bila kukipitisha Diamond mwenyewe. Tukishuka kwenye ndege moja kwa moja huongoza hotelini kukaa zaidi ya saa moja tukichagua picha za kupelekwa kwenye media. Kama ukituchunguza tukisafiri tunakuwa tuna awamu nne za kuchagua picha na awamu tatu za kuziposti.
Tumeona kuwa Instagram na mitandao mingine ya kijamii ina nguvu kuliko hata tovuti ya Diamond hivyo nguvu zote tumezihamishia huko. Niwaahidi kuwa ndani ya mwaka huu kuna mambo mengi ambayo yatakuja ikiwa ni pamoja na kuiboresha upya tovuti hiyo.
Hatuwezi kuongea bei kutokana na mazingira ya kazi zetu ila kama mtu anataka kufanya na sisi shoo tunamwambia tupo 14, wawili lazima wakae daraja la kwanza, mmoja lazima alale hoteli yenye hadhi ya nyota tano mfano tulivyokwenda Mombasa tulipokelewa na ving’ora, Uganda, Rwanda vivyo hivyo. Mfano wasanii wa nje wakija kufanya shoo nchini wanachoomba na sisi tumefikia hatua hiyo.
Kwa nini madensa wakiume wengi kuliko wakike?
Tuliamua kuongeza wasichana wawili kutokana na mashabiki kutaka hivyo. Kwa jinsi watu wanavyokuwa ndivyo vitu vinavyoongezeka, mfano Diamond alikuwa anaongozwa na mimi peke yangu (Babu Tale), nikaona siwezi, nikamwomba Fella, naye bado tukaona wawili hatuwezi tukamchukuwa na Salam bado tukaona hatuwezi na sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kumuajiri mzungu muda wowote atatua nchini kutuongoza.
Ndani ya wiki mbili hizi tutazindua ofisi ambayo itasimama kama WCB ambapo kuna wasanii watakaokuwa ndani ya WCB na watafanya video kubwa kama WCB, hatuwezi kusema Diamond ataimba na kuwika milele hapana.
Kwa wapenda burudani na wapenzi wa muziki mzuri, huu mwaka ni wetu na utaendelea kuwa wa kwetu, tarehe 20 mwezi huu tutaachia wimbo ambao Diamond amefanya na msanii mkubwa kutoka Nigeria na niwaambie kuwa huu mwaka hautaisha bila Diamond kufanya muziki na msanii ambaye yupo Top 5 duniani.
Wapo vizuri kwa sababu wakati Davido alipoachia ile meseji mtandaoni hakuwa akimlenga Diamond lakini kilichotokea ni kwamba siku ambayo Diamond aliposti meseji ile ya kuonyesha kumjibu Davido, meneja wa Davido alinipigia na kuniambia vipi mbona Diamond anafanya hivi, sikuwa nimeangalia ikabidi nifuatilie lakini ukweli ukajulikana Diamond hakuwa na lengo la kumfikishia ujumbe Davido.
Tena kuna mipango ya kuachia ngoma mpya na Davido na kipindi hicho walichodai wana bifu walikuwa ndo kwanza wametoka kutengeneza ngoma ya pamoja sasa iweje wagombane? Meseji ya mwisho tuliyokuwa tukiwasiliana na meneja wa Davido amenitumia juzi tu (Jumamosi).
Mwanzoni tulikuwa tuna tisheti za WCB baada ya Mkinga kutuvamia (kutengeneza nguo feki) tukawa tunaangalia kwaliti kwa yule aliyekuwa akituletea mwanzo. Baada ya kuona ubora unashuka tukaamua kusitisha. Baadaye akaibuka Mkinga na kutengeneza kama za kwetu hadi kofia kwa ubora wa chini kabisa. Niwaahidi kwamba katika kampuni tutakayoizindua hivi karibuni tutaweka vyote hadi vitenge vyenye lebo ya WCB, tunataka hata Miss Tanzania naye avae WCB.
Sasa hivi poa, mwanzoni tulikuwa tunapata tabu tukishuka kwa wenzetu, kuna kipindi tulikuwa tunamtania Diamond tukifika uwanja wa ndege na kumwambia hapa ndiyo mwisho wako huko tuendako hakuna cha kaa nikujue lakini sasa hivi tukishuka hata Afrika Kusini waandishi na watu kibao wanakuja wakitaka kumuona na kupiga naye picha.Makala haya yanapatikana pia kwenye video kupitia mtandao wa Globa TV,
No comments:
Post a Comment