Saturday, February 21, 2015

Afya za Watanzania hatarini

Waziri wa afya, Dr Seif Rashid

Hali afya za wtanzania zipo hatarini kutokana na kasi ya kuingizwa nchini dawa zisizofaa kwa tiba asilia, kutoka nchi kadhaa za bara hususani Korea Kaskazini.

Uchunguzi wa NIPASHE Jumamosi uliofanywa kwa zaidi ya miezi mitano, umebaini kuwa dawa hizo zinaingizwa na kuuzwa nchini pasipo kuwa na maelezo mahususi, huku taarifa nyingine zikithibitisha kuwa zina ujazo wa madini yanayoizidi kiwango kinachotambulika kwa afya za watu.

Chanzo kimojawapo cha gazeti hili kilibaini kuwa, dawa za asili zinazouzwa na waganga wa jadi kutoka Korea Kaskazini, wenye vituo vyao vya afya sehemu tofauti nchini zilipaswa kuwa na maelezo ya viambato vilivyomo ndani ya dawa husika, lakini hali haipo hivyo.

“Itakuwaje bidhaa kama dawa inayotumika na kuweza kuathiri afya za watu, iingizwe na kuuzwa kwa matumizi pasipo kuwa na maelezo ya nini kimo ndani yake,” kilihoji chanzo hicho.

AINA YA DAWA
Dawa zinazotolewa na waganga wa jadi hao, hazina majina wala viambato vinavyoeleza zimetokana na miti aina gani, muda muafaka kwa matumizi na uwezo wa kutibu magonjwa husika. Hali hiyo ni tofauti na tiba asilia na tiba asilia zinazotoka nchini kwenda nje.

Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asilia (Chawatiata) mkoa wa Dar es Salaam, Maneno Tamba, anasema utaratibu uliopo kwa dawa asilia za Tanzania zinazosafirishwa nje ya nchi, ni kuwa na maelezo yenye majina, aina ya miti iliyotumika kutengenza.

Pia anasema usafirishaji wa dawa hizo unahusisha kuwa na uthibitisho kutoka mamlaka husika kwamba hazina sumu.

“Mimi ninasafirisha dawa zangu nje ya nchi na huko lazima kila dawa iwe na jina, aina ya mti na uthibitisho kwamba hazina sumu…haya yanayouzwa na Wakorea Kaskazini zina maelezo na kama hayana viambatanisho hivyo basi wanaopaswa kushughulikia hilo ni serikali,” anasema.

Licha ya ukosefu wa maelezo hayo, wagonjwa wanapopewa dawa kwenye vituo vya waganga hao, wamekuwa wakishawishiwa kuongezewa ‘dozi’ zaidi hasa wanapobainika kuwa na fedha za ziada.
Hali hiyo inaibua wasiwasi kuhusu ufanisi ama uwezekano kwa watumiaji wake kuathirika, sababu ikiwa ni ‘dozi’ ya nyongeza kutokuwa kwenye mpango wa tiba ya awali.

VIAGRA YA SAA 180
Miongoni mwa dawa zinazouzwa kwenye vituo hivyo ni Viagra inayotengenezwa China, ikiwa na maandishi ya Ki-china ambayo hayaeleweki kwa Watanzania walio wengi.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Viagra hizo zimetengenezwa zina uwezo wa kutumika mwilini mwa binadamu kwa saa 180 mfululizo, wakati wastani wa matumizi kwa mujibu wa ushauri wa kitaalamu ni kati ya saa 4 hadi 36.

Pia zipo Viagra zinazotoka Korea Kaskazini zikidaiwa kuwa kiasi kikubwa cha madini kama risasi chuma (99ppm), zebaki (37ppm) na yale yanayojulikama kwa kiingereza kama arcenic (12ppm). Kipimo cha ppm ni sawa na ujazo wa miligramu 1 kwa kilo 1.

Hata hivyo viwango hivyo vinaelezwa na vyanzo tofauti kuwa ni hatari kwa afya ya mwanadamu na vinaweza kusababisha madhara kama upofu, kupoteza fahamu, mwili kulegea na kuwa kiziwi.

Pia vipo tofauti na viwango vinavyotambulika na nchi nyingine zikiwamo Korea Kusini, Japan, nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani.
Viwango vya nchi hizo kwa kipimo cha ppm kwenye mabano ni Korea Kaskazini, zebaki 0.2), risasi (5) na arcenic (3), Japan ina wastani wa jumla wa madini chuma kwa tiba asilia kati ya 10-20 ppm.

Kwa ulinganifu huo, madini chuma yaliyobainika kwenye dawa hizo yanafikia jumla ya kiwango cha 148 ppm ikiwa ni zaidi ya kati ya mara 7-15 ya kiwango kinachotambulika Japan.

WIZARA YANENA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbano, aliliambia gazeti hili kuwa ni makosa ikiwa dawa za tiba mbadala na zile za asili kutoka nje zinatolewa kwa wagonjwa pasipokuwa na maelezo yanayotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, kutokana na Dk Mmbano kukabiliwa na majukumu, alimuagiza mwandishi wetu kuwasiliana na mtaalamu wa masuala hayo kupitia kwa Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja.

Akizungumza kwa niaba ya mtaalamu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, Mwamaja alisema dawa zote `zinaangaliwa’ na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kwamba si rahisi zikasajiliwa pasipo kukubalika na mamlaka hiyo.

ITAENDELEA KESHO
CHANZO: THE GUARDIAN

1 comment:

  1. zichunguzwe kwa umakini ili watu wasije pata madhara baadae

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake