Saturday, February 21, 2015

Wabunge NCCR-Mageuzi wakanusha kutaka kukihama chama

David Kafulila

Wabunge wawili wa chama cha NCCR-Mageuzi, wamekanusha kuwa na mkakati wa kukihama chama hicho na kwenda kujiunga na chama cha ACT-Tanzania.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, wabunge hao David Kafulila (Kigoma kusini) na Felix Mkosamali (Muhambwe), walisema taarifa iliyotolewa na kiongozi mmoja wa ACT kwamba wanataka kuchukua hatua hiyo ni njia ya kujitangaza kupitia wao.

Mkosamali alisema binafsi amezisikia taarifa za yeye kuhusishwa kuhama chama hicho, lakini amelipuuza kutokana na kwenda kinyume na dhamira yake ndani ya chama.

Alisema hashangai viongozi wa ACT kutamka maneno ya aina hiyo, kwani chama chao bado kichanga na wanatumia majina ya viongozi mbalimbali kujitangaza kwa wananchi ili wafahamike.

“Nataka kuwashauri ACT kama wanataka kujitangaza watumie njia nyingine, lakini kueneza maneno ya uongo eti nina mpango wa kuondoka NCCR-Mageuzi watakuwa wanajisumbua,” alisema Mkosamali.

Mbunge huyo aliongeza kwamba wananchi wa jimbo lake wamemchagua kuwa Mbunge baada ya kuridhika na uimara wa chama hicho, hivyo hawezi kuwasaliti kwa kuondoka na kwenda katika chama ambacho hakifahamiki.

Kwa upende wa Kafulila, alisema kama jambo hilo lingekuwa na ukweli, asingefanya kazi ya kukiimarisha kwa kufungua matawi katika jimbo lake.
“Sauti yangu haipo sawa kutokana na kufanya kazi kubwa ya kuongea na Wananchi pamoja na kufungua matawi katika jimbo langu, niliposikia jambo hili nilisikitika sana,” alisema kafulila.

Hata hivyo, aliwataka wananchama wa chama hicho kutosikiliza maneno ya mitaani, badala yake wajikite katika kujenga umoja hasa katika kipindi hiki ambacho chafuzi mbalimbali zinatarajia kufanyika.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake