Mwenyekiti wa THK, Said Ndonge, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).
WITO umetolewa kwa jamii ya albino kuungana nchini ili kukomesha ukatili unaofanywa dhidi yao badala ya kubaguana kwa misingi isiyo na tija.Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti wa kile kinachojulikana kama Kamati ya Kuratibu Mapambano ya Kukomesha Mauaji na Utekwaji wa Albino ambao wito wao ni ‘Tuna Haki ya Kuishi’ (THK), Saidi Ndonge, jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
Ndonge alimlaumu Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (TAS) Ernest Kimaya kwa kuiita kamati yake kuwa ni ya wahuni na hivyo kusababisha hisia za kubaguana na kuwapa maadui zao nguvu za kuendelea kuwaua na kuwatesa.
Alisisitiza kwamba kamati yao hawautambui uongozi wa TAS na kutaka Wizara ya Ulinzi na Usalama, Wizara ya Mambo ya Ndani ziwajibike kwa kukithiri kwa mauaji hayo.
Wamemtaka pia waziri mkuu atangaze matokeo ya kura za maoni zilizopigwa juu ya utambuzi wa wauaji wa albino mwaka 2010, na rais atie saini ya hukumu ya kunyongwa kwa wauaji ili liwe fundisho kwa wengine huku wakiitaka serikali itekeleze maazimio haya ndani ya siku 14.
Aidha kamati ya THK imewaomba wadau, kampuni, taasisi na watu binafsi wenye kuguswa na mauaji hayo kuwaunga mkono katika kampeni hiyo.
(Habari/Picha: Gabriel Ng’osha /GPL)
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake