Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu amesema sasa anageukia ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi.
Kingu alisema siku nyingi alikuwa na shauku ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, kwamba kuondolewa katika wadhifa huo kutampa nafasi ya kujipanga na kuhakikisha anashinda jimbo hilo linaloongozwa na Mohamed Hamisi Missanga (CCM).
“Unajua kwa muda sasa akili yangu ilijikita zaidi katika ubunge ili niweze kuwasaidia wananchi kwa ukaribu zaidi. Wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi wamekaa muda mrefu bila kupata mtu wa kutatua matatizo yanayowakabili,” alisema.
Alifafanua kuwa Februari 28, mwaka huu atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika jimbo hilo, ataitumia siku hiyo kutangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge.
“Nitakachokifanya sasa ni kuwa karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha matatizo yanayowakabili ninayajua kiundani ili niweze kuyatatua kwa urahisi,” alisema.
Aliongeza, “Namshukuru Rais Kikwete kwani aliniamini na kazi aliyonipa niliifanya kwa uaminifu na uzalendo wa hali ya juu, kufanikiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, afya, mifugo, uvuvi na maendeleo kwa vijana,” alisema Kingu (pichani).
“Rais ameamua nipumzike na ninamshukuru kwa uzalendo wake mkubwa naamini bado ana imani kubwa na mimi.”
Akitoa ushauri wa wakuu wapya wa wilaya alisema, “Wanatakiwa kuhakikisha wanamsaidia kazi Rais Kikwete na kutekeleza ilani.”
Wakati Kingu akieleza hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Alisema: “Sina maneno mengi kwa sasa nitasema kauli tatu; Asante kwa pongezi yako, namshukuru Mwenyezi Mungu, namshukuru sana Rais Kikwete kwa kuniteuwa kushika wadhifa huu.”
Kwa upande wake Martha Umbulla aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, alipotafutwa na gazeti hili siku nzima ya jana alisema kuwa yupo katika kikao na kuahidi kuzungumzia uteuzi huo baada ya kumalizika kwa kikao, jambo ambalo hakulitekeleza.
Wilaya ya Kiteto ni moja kati ya wilaya zilizokithiri migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, iliyosababisha watu zaidi ya 10 kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Akizungumzia uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Bara, John Mnyika alisema unadhihirisha kuwa nchi ina mifumo legelege ya kupima wanaopendekezwa kuteuliwa kabla ya uteuzi.
“Uteuzi huu unapaswa kuibua mjadala wa haja ya kufuta wadhifa wa ukuu wa wilaya. Watanzania wanatakiwa kuikataa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu imependekeza vyeo vya wakuu wa wilaya ambavyo vipo kwa ajili ya kufanya hujuma na kuiba kura katika chaguzi,” alisema.
Hata hivyo, mkurugenzi wa masomo ya shahada ya kwanza kutoka Chuo cha Usimamaizi wa Fedha (IFM), Dk Shaban Ngole alisema kuwa mabadiliko yaliyofanywa kwa wakuu wa wilaya yanalenga kukiimarisha chama tawala baada ya tathmini ya matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Ndiyo maana unaweza ukaona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanazua maswali katika jamii, mfano, uteuzi wa Paul Makonda hauna kitu kingine zaidi ya kuongeza ushawishi wa chama katika Wilaya ya Kinondoni. Chama kimeona kuwa anaweza kuhimili mikikimikiki ya hapa mjini,” alisema Dk Ngole.
Alifafanua kuwa Makonda anaeleweka kuwa ni kada wa CCM ambaye hajifichi kutokana na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya chama hicho, hivyo kuteuliwa kwake hakuwezi kuwa na maana nyingine.
Licha ya kukiimarisha chama, Dk Ngole alisema kuwa Serikali ina dhamira ya kuongeza ufanisi katika utendaji wake. Hilo limeisukuma kufanya mabadiliko ya msingi ili kujiongezea nafasi ya ushawishi miongoni mwa wananchi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake