ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 2, 2015

DKT KIGODA ANASTAHILI KUPUMZIKA JIMBO LA HANDENI

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM.

UKWELI unauma. Na ili ufahamu hilo, mara nyingi watu wanaosema ukweli huwa hawapendwi. Watazushiwa na kusemwa mno kutokana na misimamo yao ya ukweli wanayosema mbele ya hadhira.

Wakati nasema haya, najipa moyo kuwa hata kama wapo watakaochukizwa na ukweli wangu, ila ipo siku jamii itaishi vizuri kutokana na kukombolewa na harakati za ukweli zinazoweza kupingwa na wachache wao waliokuwa kwenye nafasi mbalimbali za kiutawala.

Ndio, bora niseme tu Dkt Abdallah Omary Kigoda anastahili kupumzika kuongoza kama Mbunge wa Handeni, mkoani Tanga. Kigoda ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwa miaka 20 sasa.
Kigoda aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kama mbunge mwaka 1995. Watoto waliozaliwa miaka ya 1995 mwaka 2015 wametimiza miaka 20. Ni kipindi kirefu mno kuongoza katika nchi inayojipambanua kuwa inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Aidha, watoto hao waliozaliwa miaka ya 1995 na kukuta kero nyingi kama vile kukosa maji safi na salama, umeme vijijini, elimu duni, afya na mengineyo wanashangaa kama hadi leo kero hizo hazijatatuliwa ipasavyo licha ya kuongozwa na mbunge aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.
Kwanini Kigoda anastahili kupumzika? Licha ya Handeni kuwa wilaya kongwe na kubwa mno, lakini wananchi wake wanaishi maisha magumu na kuvumilia shida mbalimbali, jambo lililowachosha.

Wilaya hii haina maji. Wananchi wake wanalazimika kununua ndoo ya maji kwa Sh 700 hadi 1000 yanapotoka mbali zaidi. Kwa mtu mwenye familia ya watu wanne, atalazimika kununua ndoo tatu hadi tano. Endapo atanunua ndoo tano, basi atalazimika kulipia Sh 3500 kama atayanunua kwa Sh 700. Lakini kama atanunua kwa Sh 1000, basi mwananchi huyo atayanunua maji kwa Sh 5000. Je, pato lake kwa siku lipoje?

Mbaya zaidi, licha ya kuwa wilaya kongwe, lakini Hospitali ya wilaya ya Handeni haina chumba cha kuhifadhia maiti. Watu wanalazimika kupelekwa Hospitali ya wilaya Korogwe (Magunga) kuhifadhiwa kabla ya kuzikwa au kusafirishwa kwa wale wenye utaratibu huo. Aidha wilaya pia haina gari la kuzimia moto. Ulipotokea moto uliowatia hasara wananchi wengi, msaada ulizimika kutoka Korogwe. Hadi gari hilo lilipofika Handeni, moto huo ulishateketeza nyumba nyingi na kuwapa hasira wananchi kiasi cha kulipopoa kwa mawe gari hilo.

Huduma za afya ni mbovu. Na yote hayo yamesababishwa na utawala mbovu usiokuwa rafiki kwa wananchi dhidi ya mbunge Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara. Kumbuka Kigoda sit u ni mbunge wa muda mrefu, bali pia amewahi kuwa Waziri wa wizara tofauti kwa vipindi tofauti. Wakati yeye ni Waziri wa Viwanda na Biashara, lakini wakulima wake wa matunda wilayani Handeni wanapata hasara kubwa mno.


Maeneo ya Michungwani, Segera na kote wanapolima machungwa hawana kwa kuyapeleka na mara kadhaa wanayouza si yale yanayozaliwa. Hii ni aibu kubwa mno. Wilaya ya Handeni ipo ipo tu. Hata elimu ya sekondari ya kidato cha tano na sita ni mtihani mzito.

Licha ya ukongwe huo lakini hakuna cha kujivunia. Wakulima wanadhulumiwa mashamba yao na wenye nacho. Watu wachache wamegawana maeneo makubwa ya ardhi, hali kadhalka uwapo wa dhahabu na madini mengine hakuonekani dalili njema za kuwakomboa wananchi wa Handeni, wanaoishi kwa kupiga miayo. Ni mifano hii michache tu kati ya mingi ninayoweza kuisema hapa, nadiriki kusema Mbunge Kigoda hana cha kumfanya agombee tena jimbo hilo kwa kipindi cha tano kijacho.

Bali anastahili kupumzika na abaki kuwa mshauri tu. Watu wanaishi kwa tabu kwenye wilaya yao yenye kila aina ya matunda. Wananchi wa Handeni wataendelea kutaabika hadi lini?

Hili ni jambo la kuliangalia. Mfumo wa kiutawala wilayani Handeni umekufa na hauna mwamko tena. Mbaya zaidi, kitu chochote ambacho mbunge hakitaki aidha kwa woga wake kisiasa au vinginevyo hakubali kifanyike hata kama kina manufaa na wananchi wake.

Katika hali ya kushangaza na kuogopesha, hakuna mtu yoyote anayeweza kutoa sauti yake kumkemea au kumkosoa mbunge. Hii ni mbaya. Kumuogopa huku kunasababisha hasara kwa wilaya.

Haiwezekani mbunge akawa anajua yote. Lakini pia haiwezekani kuona mbunge analalamikiwa bila sababu za msingi. Ingawa baraza la madiwani ndio lenye mamlaka ya kisheria ya kupanga bajeti na kuisimamia, ila mbunge naye ni mjumbe kutokana na kofia yake. Na kwakuwa tumekuwa na utawala wa kuogopana, madiwani hawa wameshindwa kupaza sauti yao kusimamia mambo yenye manufaa na wilaya ya Handeni.

Leo hii ni aibu iliyoje? Ukongwe wa Handeni na rasilimali zote ilizokuwa nazo, hakuna chuo chochote kinachoweza kuwapa elimu ya juu wanafunzi wanaotokea kidato cha nne au sita.
Lini Handeni itakuwa na mwangaza? Mwangaza huo utakuja siku Kigoda atakapoamua kwa ridhaa yake au kulazimishwa kupumzika kwasababu ameshindwa kuwaongoza watu wake.

Kwa bahati mbaya, leo hii wananchi wamekuwa wakali. Wamekuwa na mtazamo chanya wa kuhoji maendeleo yao na wale wanaochelewesha mikakati inayoweza kuwakwamua kiuchumi. Wakati nasema haya, nadiriki kuona hatari ya kudhalilika juu ya mbunge huyu, hasa kama ana ndoto za kutetea kiti chake. Wananchi wamekuwa wakihoji udhaifu wake hadharani.

Mengi yanayosemwa ni kama matusi kwake. Mbunge aliyekaa madarakani miaka 20, anapoambiwa ameshindwa kufanyia kazi hata chumba cha kuhifadhia maiti ni aibu isiyokuwa na kifani.
Ni budi kwa viongozi wa juu wa CCM kuvuta taswira halisi ya ugumu wa maisha ya wana Handeni. Lakini pia viongozi hao lazima wajuwe chama chao kipo rehani kwasababu ya kumng’ang’ania mtu mmoja.
Yeye ni nani? Hakuna mwingine? Mfumo wa upatikanaji wa viongozi wa CCM hususan wa kuangalia asiyependwa ndiyo anayepita umepitwa na wakati kwa Dunia ya leo ya Sayansi na teknolojia.

Tunachokiona sasa ni tatizo kubwa la kimfumo kama nilivyojaribu kulieza hapo juu kwenye makala haya. Kama leo tunawaza namna gani ya kuleta maji, umeme vijijini, afya jua tumeshindwa.

Na udhaifu huu utachukuliwa kama tahadhari katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kuhakikisha kuwa mgombea wa CCM, hasa kama akiwa Kigoda aenguliwe. Na kama watashindwa basi hata wale wasioaamini upinzani watashawishika na kupiga kura za chuki dhidi ya Kigoda na chama chake CCM.

Bora ukweli useme bila woga. Ukweli usemwe ili watu wajirekebishe katika harakati za kuikomboa wilaya ya Handeni ambayo si wote wanaiheshimu kutokana na kiwango kibovu cha viongozi wake, wakiongozwa na mbunge wa miaka 20 madarakani jimbo halina maji, huduma za afya mbovu, elimu ya kusua sua, malalamiko ya wakulima na kadhalka.

Ajabu, wanaopita pembeni wakimsifia mbunge ni viongozi wachache wa CCM wilayani, ambao kwa namna moja ama nyingine wana manufaa naye, aidha kuwekwa wao madarakani katika Uchaguzi wa ndani wa CCM, hivyo kuendelea na sera ya kulipana fadhira.

Hilo haliwezekani. Tunahitaji kuzaliwa upya kwa wilaya ya Handeni, tukianzia na kuona namna gani mfumo uliooza chini ya Kigoda unaondolewa kwa ajili ya kuibua ari mpya, kasi mpya na vitendo vyote vya kupigania maendeleo kwa jimbo hili linaloonekana la mwisho kimaendeleo.
 

No comments: