ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 25, 2015

HABARI KWA KINA KUHUSIANA NA VURUGU YA WANANCHI BAADA YA POLISI KUUA MTU MMOJA


Wananchi wakiangalia moto uliowashwa na watu wasiojulikana wakati wa vurugu baina ya polisi na wananchi katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa jana. Picha ya Mtandao HUKO ILULA MKOANI IRINGA

Kilolo. Polisi wa wa kituo cha Ilula kilicho Kilolo mkoani Iringa wanatuhumiwa kuua mtu mmoja, jambo lililoamsha vurugu kubwa zilizosababisha magari mawili kuchomwa moto.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa wananchi waliokuwa na hasira walichoma moto magari yaliyokuwa yameegeshwa kituoni hapo na kuchana nyaraka zilizokuwapo ndani pamoja na kufungulia mahabusi.
Mapigano hayo kati ya polisi na wananchi yalitokea wakati polisi wakifanya operesheni ya kukamata watu wanaokunywa pombe muda wa kazi na kusababisha purukushani kubwa.
Mmoja wa mashuhuda hao, Omary Kivade, ambaye ni mkazi wa Ilula, alisema kuwa polisi mmoja alionekana akimfukuza mwanamke ambaye walimtuhumu kuwa alipika pombe wakati wa kazi. Alisema baada ya polisi huyo kurudi, wananchi walishangaa kuona hakuwa amemkamata yeyote na ndipo wakaamua kwenda kuangalia sehemu walikokimbilia na kumkuta mwanamke huyo akiwa ameshafariki.
Alisema kufariki kwa mwanamke huyo kulipandisha hasira wananchi ambao walirudi kituoni ambako walipindua magari manne na kuchomo moto matatu madogo, basi aina ya Toyota Hiace, na pikipiki moja katika vurugu hizo zilizodumu kwa saa tano.
Vurugu hizo zilisababisha barabara kuu ya Dar es Salaam-Iringa kufungwa kwa takribani saa tano, kutoka saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Haikuweza kufahamika mara moja ni nini hasa kimesababisha kifo cha mwanamke huyo kati ya kupigwa na polisi au kuanguka wakati akimkimbia polisi asimkamate.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mkazi wa Ilula, Jamila Athuman alisema baaada ya vurugu kutokea klabuni na wananchi kusikia kuwa kuna mwenzao amekufa, walijikusanya na kuchoma matairi  barabarani na kusababisha magari kushindwa kupita.
Aliongeza kuwa polisi wa kituo cha Ilula walizidiwa nguvu na wananchi waliokwenda kituoni hapo na watu hao walichoma magari, kuwapiga askari waliokuwepo kituoni hapo.
Pia basi la kampuni ya Nyagawa linalofanya safari zake kati Njombe na Dar es Salaam lilivunjwa vioo vyote na wananchi baada ya askari kukimbilia kwenye basi hilo kuokoa maisha yao kutokana na kuzidiwa nguvu na wananchi.
Alisema baada ya hali kuwa ya hatari, polisi wa kijiji cha jirani kata ya Mbigili na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Iringa walifika na kutuliza hali hiyo na barabara kurejea katika hali ya kawaida.
Mmoja wa mashuhuda waliokuwapo eneo la tukio, James Kilovela alisema baada ya polisi hao kufika eneo la tukio na kuwatimua watu kwenye vilabu bila kutoa maelezo yoyote, wananchi walianza kukimbia ovyo kuepuka kukamatwa.
Aliongeza kuwa wakati wanakimbia mama mmoja alionekana akipigwa ngwala na polisi wakimtuhumu kufungua klabu wakati wa kazi kabla ya mama huyo kuanguka na kuonekana amekufa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mongi alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa hayuko mkoani Iringa.
Naye kaimu kamanda wa polisi, Pudenciana Protas  hakupatikana kutokana na simu yake kutokuwa hewani muda wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kilolo, Gerald Guninita alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata taarifa kamili.
MWANANCHI

No comments: