Mchungaji James Regnald Mhando enzi za uhai wake.
Na Haruni Sanchawa/Uwazi
MAITI ya Mchungaji James Regnald Mhando aliyefariki Februari 18, mwaka huu imezua tafrani nzito kwa ndugu na jamaa baada ya kujulikana kuwa alikuwa na wake wawili ambapo mke mmoja alitaka mwili uagwe hospitali na upande wa pili ukitaka ukaagwe kwa mama yake marehemu.
Katika msiba huo ilibainika kuwa, mchungaji huyo (kanisa lake tunalihifadhi kwa sababu maalum), alikuwa na watoto sita kwa mama tofauti na wote walijitokeza katika mazishi ya baba yao.
Inadaiwa kuwa Mchungaji Mhando alianza kuumwa Jumamosi ya Februari 14, mwaka huu lakini inadaiwa baadhi ya watoto na ndugu wengine hawakujulishwa hadi Jumanne ambapo inadaiwa alibebwa na gari la wagonjwa kutokea Morogoro hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Habari zinasema ilipofika Jumatano saa tano usiku, mchungaji huyo aliaga dunia na mbali ya kuaga dunia, bado tukio hilo lilikuwa ni siri na ilidaiwa ilikuwa afanyiwe shughuli za mazishi kwa siri bila ya baadhi ya watoto wake wakubwa kujua.
Hata hivyo, habari za msiba huo zilizagaa haraka na kumfikia mke wa kwanza wa ndoa ambaye alikuwa nchini kwa ajili ya mapumziko kwani anafanya kazi nje ya nchi, hivyo ukoo ukaanza kutaarifiana.
Mchungaji Mhando alioa na kufunga ndoa Novemba 17, 1979 katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, jijini Dar es Salaam, hata hivyo, ilidaiwa kuwa mwaka 1985 mtumishi huyo wa Mungu aliamua kuondoka nyumbani alikokuwa akiishi na mkewe na kwenda kuishi na mwanamke mwingine ambaye inadaiwa kuwa alikuwa ni wa dhehebu lingine na wakafunga ndoa serikalini.
Habari zinadai kwamba mwanamke huyo alikuwa anaitwa Mwanaheri kabla ya kubadili dini na kuitwa Glory na wakafanikiwa kuzaa watoto wawili, mmoja akapewa jina la Reginald Junior na mtoto mwingine anaitwa Sada au Doreen Mhando. Habari zinasema kabla ya kuondoka kwa mke wa kwanza, mchungaji huyo alizaa naye watoto wawili, wa kiume na wa kike....Askari akiwa eneo la tukio.
Hata hivyo, wakati wa msiba huo watoto wengine wawili walijitokeza nao wakidai kuwa ni baba yao, hali iliyozusha minong’ono kwa watu walioshangazwa na mwenendo wa marehemu.Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Dorofea Mhando (82) alisema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo ni kibaya kwani alimshawishi mwanaye kuisaliti familia yake.
“Mwanamke huyo mwingine alikuwa akiishi na mwanangu kwa siri kubwa sana, kama vile marehemu hakuwa na familia na akawa anajifanya kuwa yeye ndiye mke wa kwanza, kitu ambacho ni cha uongo kwani marehemu alishaoa kanisani mwaka 1979.
“Marehemu baada ya kumpata mwanamke huyo alikuwa hashiriki shughuli nyingi za hapa nyumbani kwa kuhofia watu watajua kuwa alikuwa na familia nyingine, kitu ambacho kilinisikitisha,” alidai mama huyo.
Mama huyo aliongeza kuwa maisha ya mchungaji huyo yalikuwa sehemu mbili, Morogoro na jijini Dar es Salaam, alikuwa akifikia Mivinjeni kwenye ofisi ya shughuli zake.“Baada ya kupata taarifa ya msiba niliagiza mwili uletwe hapa Ukonga Majumba Sita ukitokea Muhimbili kwa ajili ya shughuli za kuagwa lakini mke mdogo akawa anapinga,” alidai mama huyo.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mke mdogo alisisitiza kuwa baada ya kuandaa mwili wa marehemu uagwe Muhimbili, kisha upelekwe katika Makabauri ya Kinondoni kwa mazishi. Kulitokea mabishano ambapo mtoto mkubwa wa marehemu aliyefahamika kwa jina Feda, alisema baba yao hawezi kuagwa kama mkimbizi kwani ana watoto, mke na mama yake mzazi, hivyo akaamuru mwili ukaagwe kwa bibi yake Ukonga Majumba Sita.
Habari zinadai kuwa mvutano huo ulifikishwa Polisi Kituo Kikuu ambapo lilifunguliwa jalada namba CD/ RB/ 2627/ 2015 ambao waliamuru shughuli za mazishi zisifanyike hadi muafaka upatikane.
Habari zinadai kikao kilifanyika polisi na muafaka ukapatikana kwamba mwili ukaagwe kwa mama yake mzazi Ukonga Majumba Sita.
Maofisa wa polisi walitoa askari wenye silaha chini ya kamanda wao aliyefahamika kwa jina moja la Manyama aliyeongozana na wana familia hao hadi Muhimbili kisha Ukonga, baadaye kwenye Makaburi ya Kinondoni ambapo mchungaji huyo alizikwa chini ya ulinzi.
Credit:GPL
No comments:
Post a Comment