ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 3, 2015

MIAKA 38 YA CCM NA FALSAFA YA RAIS BORA LAZIMA ATOKE CCM

Rais wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa wiki iliyopita kimeadhimisha miaka 38 tangu kuzaliwa kwake katika kaya hii. Mazuri na mabaya yake sitayajadili leo bali nitaangalia jambo moja nalo ni IMANI.
2015 ni mwaka wa uchaguzi. CCM kama chama tawala kinaingia kwenye kinyan’ganyiro hicho kikiamini falsafa ya ya kiongozi wake wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere kuwa rais bora hawezi kutoka nje ya CCM.
Kwa masikio yangu mimi Mkuu wa Kaya nilimsikia mwenyekiti wa chama hicho taifa, Jakaya Kikwete, akisherehesha imani hiyo alipokuwa anahutubia maelfu ya wafuasi wa CCM katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Najiuliza; imani ya chama hicho tawala inaambatana na matendo? Maana ni wazi Nyerere aliposema rais bora atatoka CCM alimaanisha CCM bora siyo dhaifu.
Msingi wa hiki ninachokisema unajengwa na kauli ya muasisi huyo pale aliposema: “Bila CCM imara nchi itayumba.” Hapa ndipo mahali pa kujadili.

Je, wakati mwenyekiti wa sasa akisisitiza imani ya chama chake mbele ya wanachama anaamini kuwa CCM anayoingoza ni bora kama zama za Mwalimu na kwamba ina sifa za kutoa rais bora? 
Namkumbusha; Kikwete aliposisitiza kuuenzi wosia wa Mwalimu anakumbuka kauli ya muasisi wake aliyosema; Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje?
Kwa mawazo ya leo, hakuna asiyejua kuwa kioo cha CCM kimemeguka vipandevipande na taswira zinazoonekana ndani zinatofautiana. Chama kimegawanyika katika makundi.

Leo hii mwenyekiti akisimama mbele ya kioo cha chama chake haonekani mwili mzima, amegawanyika kiasi cha kutoutambua utimilifu wake na ndiyo maana anasisitiza ongezeko la wagombea urais wenye sifa kwa kuwa waliojitokeza hawajaweza kuziba ufa wa kioo chake.

Mwenyekiti angali anatishwa na kivuli cha makundi; Nyerere hakuwa mwoga, alikuwa jasiri, mwenye kusimamia anachokiamini. Waliofanya naye kazi wanashahidisha kuwa hakuongoza kwa matakwa ya chama bali ya wananchi.

Msingi huu ndiyo ambao CCM inapaswa kuufuata katika kuelekea kuipatia kaya hii mkuu mpya mwenye sifa ya ubora. Vinginevyo imani waliyorithishwa kuwa rais bora atatoka CCM itakuwa haina maana.
Mwananzengo wenzangu; wakati chama hicho kikiadhimisha miaka 38 ya uhai wake, falsafa tatu lazima tuzifikirie sana kwa mustakabali wa kaya hii, nazo ni RAIS BORA KUTOKA CCM, WATANZANIA WANATAKA MABADAILIKO NA BILA CCM IMARA NCHI ITAYUMBA.

Kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, lazima wananzengo tujihoji juu uimara wa chama tawala na kama kitaweza kumteua mgombea bora tunayemtaka. Maana tunaweza kuamini falsafa kuwa rais bora atatoka CCM lakini wakubwa wakajiteulia mgombea atakayelinda maslahi yao na sisi tukadanganywa kwa imani iliyokufa na kuzikwa kuwa rais bora lazima atoke CCM. Tusikubali!

Jambo la pili ni uhitaji wa mabadiliko. Mgombea ajaye lazima awe na kigezo cha kuiletea kaya hii mabadiliko ambayo Wanazengo wanayataka. Tukiletewa mgombea ambaye hana sifa hii tutoke usingizini tuyatafute mabadiliko yetu nje ya CCM!

Mwisho wake ni CCM dhaifu kuiyumbisha nchi. Kama nilivyosema, chama hiki kutokana na makundi ya urais yanayonyukana kuingia ikulu, yanaweza kukidhoofisha chama hicho. Hilo likitokea tusikubali kuyumbisha nchi nzima, badala yake tukiache chama kiyumbe chenyewe na ikiwezekana kianguke madarakani kabisa!
Huu ndiyo msimamo wangu mimi Mkuu wa Kaya. Shime Wananzengo wenzangu, niungeni mkono katika mawazo haya!
SOURCE:GPL

2 comments:

Anonymous said...

MHESHIMIW RAIS UMESEMA, LAKINI TUKUHAKIKISHIE hii ni kauli ya aliyekuwa muasisi na kwa nyakati hizi viongozi wengi wamekuwa wezi, rushwa, na kutojali wananchi wao wanavyotaabika, kodi hailipwi ipasavyo na fedha nyingi kuhodhiwa na wenye nazo, na wakijisafisha kuwa hawana utajiri hii ni kudanganyana!! Rais bora kwa TANZANIA YAsasa hivi hatakiwi kabisa kutoka CCM, WANAONGOA wasema ukweli kucha na meno bila ganzi!! Huu ndio wakati muafaka!! wewe nenda kapumzike tunakushukuru sana kwa muda uliotuongoza!!

Anonymous said...

Asante ndug yetu na mheshimiwa Rais wetu!! Hiki kipindi kilikuwa kigumu na tunakupongeza kwa zile jitihada ulizofanya ila ya Tegeta ESCROW kwa ujumla imetuliza waTanzania wengi kwa kukubali kuwa fedha ile sio ya serikali lakini kwa upande mwingine wananchi wamo>?!R5aisi atokaye CCM ni mla rushwa tu kwanza pesa hiyo ameipata wapi ni wakuogopa kama Ukoma!! hafai hafai!!