ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 2, 2015

Milioni 100 zaiua Yanga U/Taifa

Wachezaji wa Yanga (kijani na njano) wakichakarika mbele ya wapinzani wao, Ndanda FC, katika mechi ya ligi kuu bara kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam jana Jumapili. 
By Khatimu Naheka 
Timu hiyo ambayo imesajili wachezaji wengi chipukizi na wasio na uzoefu, imewahi kukanya Dar es Salaam mara moja tu lakini walipofika kwenye Stand Kuu ya Mabasi Ubungo wakaonyeshwa uelekeo wa Mbagala ambako walikwenda kucheza na JKT Ruvu na walipotoka wakapitiliza kwao Mtwara wakabaki kuusikia tu Uwanja wa Taifa kwenye redio na magazeti.
NDANDA FC ya Mtwara imeweka rekodi ya aina yake kwa kukanyaga kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na kulazimisha suluhu na Yanga ambayo usajili wake ni zaidi ya Sh500 milioni.

Timu hiyo ambayo imesajili wachezaji wengi chipukizi na wasio na uzoefu, imewahi kukanya Dar es Salaam mara moja tu lakini walipofika kwenye Stand Kuu ya Mabasi Ubungo wakaonyeshwa uelekeo wa Mbagala ambako walikwenda kucheza na JKT Ruvu na walipotoka wakapitiliza kwao Mtwara wakabaki kuusikia tu Uwanja wa Taifa kwenye redio na magazeti.

Lakini jana Jumapili kwa mara ya kwanza wametoa ushamba baada ya kuingia na kucheza kwenye uwanja huo wakiwa na usajili wao wa Sh100 milioni ambao uliizuia Yanga yenye wachezaji watano wa kigeni na Kocha Mholanzi Hans Pluijm.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Ndanda ambao jana walikuwa wakishangilia kana kwamba wametwaa ubingwa, Edmund Kunyengana, alithibitisha kwamba kwenye usajili mkubwa walitumia Sh80 milioni na dirisha dogo Sh20 milioni.

Katika mchezo wa jana, Yanga ikitumia mastraika wake mahiri; Kpah Sherman, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete na Danny Mrwanda ilikosa mabao manne ya wazi kitendo ambacho kilimkera kocha Pluijm.

Pluijm alisema: “Tumekosa mabao manne ya wazi na kama wangekuwa makini tungepata ushindi kabisa, kila mtu ameona.” Matokeo hayo yameifanya Yanga sasa kuwa na pointi 19 ikishikilia nafasi ya pili huku Ndanda ikiwa na pointi 14. Katika kipindi cha kwanza Yanga ilifanya mashambulizi matano ya maana langoni kwa Ndanda kupitia kwa Msuva, Ngassa, Mrwanda na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, lakini kipa wa zamani wa Simba, Wilbert Mweta aliyazuia na mengine yakapaa.

Ndanda ambao walikuwa wakishangiliwa na mashabiki wa Simba, walikuwa na mashambulizi mawili ya maana kupitia kwa fowadi wake Masoud huku Omega Seme akionyesha ufundi wake kuituliza Yanga.

Kipindi cha pili Yanga ilionekana kujipanga lakini Ndanda wakatumia akili za ziada kwa kujiangusha mara kwa mara pamoja na kucheza na saikolojia za wachezaji wa Yanga ambao walionekana kama wamepaniki.

Dakika ya 90 mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro alimwonyesha kadi nyekundu, Ernest Mwalupani, wa Ndanda ikiwa ni kadi yake ya pili ya njano kwenye mchezo huo ambao mashabiki wa Yanga walikuwa wakipaza sauti nje ya uwanja wakitishia kutokuja uwanjani tena huku wenzao wa Simba wakiwakejeli kwamba “Mmewashindwa hata Ndanda ambao tumewapiga, mwaka huu mnalo.”

Kocha wa Ndanda Abdul Ngange alisema walitua Dar es Salaam wakiwa wanajua mazingira ya uwanja na mchezo utakavyokuwa hivyo akawaambia wachezaji wake wakabe mpaka kivuli kuanzia sekunde ya kwanza mpaka ya mwisho jambo ambalo walifanikiwa.

Ndanda; Wilbert Mweta, Aziz Sibo, Paul Ngalema/Shukuru Chachala, Kasian Ponela, Ernest Mwalupani, Zablon Raymond/Hemed Khoja, Jacob Massawe, Omega Seme, Nassoro Kapama, Stamili Mbonde, Masoud Ally/Isihaka

Yanga; Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela, Simon Msuva, Hassan Dilunga/Said Makapu, Kpah Sherman/Amissi Tambwe, Danny Mrwanda,Mrisho Ngassa/Jerry Tegete. Katika mchezo mwingine jana, Ruvu Shooting iliishinda Stand United mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mabatini mabao yakifungwa na Juma Mpakala na Yahya Tumbo. Hamis Thabit alifunga bao la Stand.
SOURCE:MWANASPOTI

No comments: