Wiki iliyopita niliishia pale kwenye kundi nililolilenga la mwanamke anaishi na mumewe lakini kila senti anayopewa anaibana ili akafanyie maendeleo yake kwa siri na mumewe asijue!
Nilisema mke mwenye sifa za kumchuna mumewe ni yule ambaye inapotokea ameona mumewe ana pesa nyingi yupo radhi amwambie waende bichi wakatumbue maisha kuliko kumwambia anunue viatu au aongeze mashati.Wiki hii tunaendelea...
Kuna wanaume walikuja kubaini baadaye sana kwamba, wake zao wamejenga kwa siri na hali hiyo imevunja ndoa nyingi kwani mwanaume anakuwa anawaza mambo mengi, likiwemo la nyumba hiyo kujengewa na mwanaume mwingine au alikuwa akichunwa kwa faida binafsi ya mkewe.
NILIWASHIRIKISHA WATU
Ili kupata uwiano wa uchunguzi wangu na kinachojulikana na watu, niliamua kuwashirikisha baadhi ya wanandoa kuhusu hali hiyo ambapo wengi walikuwa na mawazo ya kupishana.Mzee Abdallah, mkazi wa Keko, Dar yeye ana ushahidi binafsi kuhusu mke kumgeuza buzi mumewe.
Anasema: “Nina mke mdogo kwa sasa baada ya kuachana na mkubwa. Mke wangu mkubwa alinichuna sana kwa sababu kila nilipokuwa nikipata mshahara nilimkabidhi yeye kupanga matumizi lakini akawa anawanunulia mabati wazazi wake bila mimi kujua.
“Kuna wakati nilimwambia apeleke pesa kwao ili wazazi wake wanunue mabati ya kuezekea nyumba ya nyasi akaniambia niachane na mpango huo, kwamba baba yake atajinunulia mwenyewe. Kumbe alikuwa akifanya huo mchezo, pesa zangu anapeleka kwao kwa siri.
“Siku moja alifiwa na bibi yake mzaa baba, msiba ukawa kijijini kwao, tukaenda. Kufika nilishtuka kuona nyumba yote imepigwa mabati na sambamba na ukarabati mwingine. Nikampongeza baba mkwe wangu kwa moyoni.
“Baada ya msiba kumalizika, kama kesho naondoka, nilikaa na shemeji yangu mdogo, akaniambia ananishukuru sana kwa kusaidia manunuzi ya mabati na fedha nyingine zilizowezesha nyumba kukarabatiwa.
“Huyo shemeji alisema yeye ndiye alikuwa akipokea fedha kutoka kwa dada yake, yaani mke wangu. Sasa afadhali mke mwenyewe angekuwa anafanya kazi, alikuwa mama wa nyumbani tu.
“Kwangu hazikuwa pongezi bali kashfa! Nilifika Dar na kusubiri mke wangu arejee. Alipokuja nilimuuliza kuhusu mabati na ukarabati wa nyumba, akatak kuniongopea bila kujua kwamba nilizungumza na ndugu yake wa damu. Aliniambia ni pesa za baba yake, alikuwa akifanya biashara. Sikutaka amalize, nilimpa ukweli wote, nikamwandikia na talaka palepale.
“Kama angekuwa akiniomba pesa za kufanyia maendeleo kwao nakataa hapo sawa. Ningesema amejibanabana ili afanikishe lakini alikuwa akikataa nisisaidie kwao. Sasa mwanamke wa hivyo wa nini mimi?”
KAULI YA MWANAMKE
Nilibahatika kuzungumza na mama Hussein, mkazi wa Tandale, Dar. Yeye alisema:
“Mimi ninavyojua mke kumchuna mumewe inatokana na staili ya maisha yaliyopo. Wapo wanaume ili mke kuiona pesa yake afanye kazi nzito, ndiyo maana akipata upenyo anawekeza ili afanyie mambo ya maendeleo kijijini kwao.”
Swali: “Je, inapotokea mke ndiyo hataki kupewa pesa za kusaidia kwao lakini kwa siri anakusanya na kuzituma?”Mama Hussein: “Kwa kweli mke wa aina hiyo ni mchunaji kwa asilimia mia moja.”
Swali: “Lakini hili la mke kuona mumewe amepata pesa na kumtaka waende kujirusha bichi badala ya kumshauri aongeze viatu au mashati, nalo unalizungumziaje?”
Mama Hussein: “Hilo pia ni tatizo kubwa. Mke ndani ya nyumba anaweza kumpendezesha mumewe hata kwa pesa za mfukoni mwa mume huyohuyo.“Unajua wapo wanawake siku hizi betri kichwani zimeisha chaji, hawa ndiyo wanaosumbua na kusababisha samaki mmoja akioza wote watoe harufu.”
NINAHITIMISHA HIVI
Nimejitahidi kuchukua maelezo ya wasomaji wangu wawili lakini kila upande umewakilisha kilichosemwa na wengine. Ni kweli kuna wake za watu ambao wanawachuna waume zao kwa staili niliyoisema.
Hata tabia ya baadhi ya wanawake wakipokea mshahara (kama ni wafanyakazi) halafu pesa zao zinatumika saluni, ananunulia nguo nzuri nyingine anatuma kwa wazazi wake halafu mshahara wa waume zao ndiyo wa kununulia chakula, kulipia bili za maji, umeme na ada za wanafunzi, huko pia ni KUCHUNA!!
Tuonane wiki ijayo kwa makala nyingine kali.
GPL
No comments:
Post a Comment