ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 24, 2015

WATANGAZA NIA WAELEWE KUWA RAIS WA AWAMU YA TANO ATABEBA MIZIGO MIZITO

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

TUMSHUKURU Mungu kwa kutupa uhai, hatuna budi kumpongeza kwa kutupendelea kwani wengi kawachukua na sasa wametangulia mbele za haki.

Baada ya kusema hayo nianze mada ya leo kwa kusema kwamba rais ajaye wa awamu ya tano hapa nchini atabeba mizigo mizito na kwa hali hiyo ni wazi kwamba atakuwa na wakati mgumu pengine kuliko watangulizi wake wanne.

Naamini kwamba wanasiasa wote waliotangaza nia ya kuwania ofisi hiyo kubwa kuliko zote nchini kiutendaji wanalitambua hilo, na wamejipima na kujiridhisha kuwa wako tayari kukabiliana na changamoto zinazotokana na jukumu hilo kubwa.

Mifano ni mingi ya jinsi atakavyokumbana na changamoto nyingi kama vile, itakuwa kazi ngumu kwake kuwafunga midomo Watanzania ambao kwa sasa wameelimika, wanajitambua pia wanafahamu haki zao, wanafahamu nini wanakitaka, nini wanakikosa na baadhi yao wanajua sheria za nchi.

Kiongozi ajaye, awe wa CCM au upinzani, hakuna shaka kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuunda serikali, jukumu ambalo pia siyo rahisi kama ilivyokuwa zamani pia atakuwa na jukumu la kutekeleza kazi zote zilizoanzishwa bila kukamilishwa na mtangulizi wake wa awamu ya nne, Rais Jakaya Kikwete.

Mbali ya ahadi za Kikwete, pia kuna masuala mengine mengi yamekuwa sugu na serikali yake imeshindwa kukabiliana nayo. Hayo ni pamoja na ujangili, rushwa, biashara ya dawa za kulevya, matumizi mabaya ya fedha za umma yaani ufisadi na mikataba mibovu inayoangamiza nchi.

Kuna matatizo mengi kama vile migogoro baina ya wakulima na wafugaji karibu maeneo mengi nchini na inasumbua wengi na kusababisha vifo katika baadhi ya sehemu kama yalivyoainishwa vizuri kwenye ripoti ya kamati teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoongozwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.

Tatizo hili ni kubwa na zito linalohitaji ufumbuzi wa haraka. Ardhi, ni rasilimali kubwa, utajiri ambao nchi yetu imejaliwa kuwa nao, lakini imekuwa na mzozo hasa baada ya kuwaingiza wawekezaji ambao wanalalamikiwa na wananchi kutokana na kuingiza unyanyasaji.

Hapa nchini kwa sasa ardhi inauzwa hovyo wakati mwingine kwa kisingizio cha uwekezaji mkubwa au mdogo, dhuluma za kuwania viwanja au mashamba zinaongezeka, mijini na vijijini.

Ardhi, badala ya kuwa rasilimali, imegeuka chanzo, sababu kubwa ya ugomvi na maafa makubwa kwenye jamii zetu nyingi.

Matokeo ya maafa ya ardhi siyo madogo na haipo sababu ya kufumbiwa macho na kuachwa yapite, rais ajaye atakumbana na changamoto hii.

Mbali ya ardhi, kuna tatizo la mauaji ya Albino,wanawake kwa wanaume, hasa wenye umri mkubwa kutokana na ushirikina na yamekuwa yakitokea Shinyanga, Mwanza au mikoa mingine ya kanda ya ziwa, hili ni tatizo ambalo rais ajaye lazima ahakikishe analimaliza.

Kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), ni wengi, wanaendelea kuwindwa kama vile wao ni swala wanaowindwa kwa ajili ya kitoweo, kisa ni dhana potofu kwamba ngozi zao ni biashara nzuri, yenye kuleta utajiri. Upuuzi huu ni kama mfupa mgumu ambao serikali ya awamu ya nne imejaribu kuutafuna, lakini imeshindwa, sasa utahamishiwa kwa rais ajaye.

Pia, kuna tatizo la Katiba Mpya ambayo inasubiriwa kupigiwa kura ya maoni siku si nyingi, lakini mchakato huo ukikwama litakuwa ni jukumu jingine la rais ajaye.

Nchi yetu, ambayo imejitangaza kama kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano katika miaka ya karibuni imeshuhudia pia matukio mengi ya mauaji na uhalifu unaongezeka, ujambazi na udini umeanza kushamiri. Ni jukumu la rais ajaye kuona tatizo hili linalotishia amani ya nchi yetu nzuri.

Ukabila pia una harufu yake, hivi sasa kuna ukanda, hili ni tatizo zito ambalo rais ajaye atatakiwa atoe kucha kuliangamiza.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

GPL

No comments: