ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 18, 2015

Baada ya kufukuzwa, Zitto aigawa mitandao ya kijamii

Mitandao ya kijamii imeanza kuchukua nafasi na hata kuwa sehemu ya maisha ya kawaida, watumiaji wake hupata taarifa mbalimbali na pia nafasi ya kuanzisha mijadala motomoto.
Hata hivyo, changamoto kubwa iliyopo katika mitandao hiyo ni ugumu wa kudhibiti mijadala, hivyo wakati mwingine taarifa nyingine zinakosa ukweli na kuhitaji vyanzo zaidi ili kuzithibitisha.
Suala la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kushindwa kesi na hatimaye kuvuliwa uanachama na chama chake cha Chadema, limekuwa sehemu ya mjadala na malumbano makali katika mitandao ya kijamii.
Ili taarifa iaminiwe na wasomaji, mitandao mingi ilinukuu akaunti ya ‘twitter’ ya Kituo cha redio cha East Africa kilichoitoa taarifa ya Zitto kama habari mpasuko.
Katika taarifa hiyo, alinukuliwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akitangaza rasmi Zitto kuvuliwa uanachama.
Katika baadhi ya mitandao majibizano kati ya watetezi wa Zitto na upande wa pili, yalionyesha kama makundi hayo yangekuwa ukumbini kuna tukio baya lingeweza kutokea kwa upande mmoja kushindwa kujizuia na kuanzisha mapigano.
Hii inatokana na ukweli kwamba mbunge huyo ana mashabiki wengi kwenye mitandao ya kijamii na pengine ni miongoni mwa wanasiasa wachache wanaojitokeza hadharani kwenye mitandao na kushiriki mijadala bila woga.
Kama kuna suala linalohitaji ufafanuzi kutoka kwa Zitto, mashabiki wake hawalazimiki kusubiri kauli yake kwenye magazeti kesho yake kwa kuwa hachelewi kutoa maelezo kupitia kwenye akaunti zake kwenye mitandao.
Hata baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupilia mbali pingamizi lake la kutaka asijadiliwe na chama chake, baada ya muda mfupi Zitto aliibuka katika mitandao ya kijamii akitoa ufafanuzi wa kilichotokea.
“Hatukuwa na wito wa Mahakama leo. Jaji kahamishiwa Tabora. Hatuna taarifa ya Jaji mpya. Mwanasheria wetu anafuatilia na atatoa maelezo,’’ alisema kupitia mtandao wa Twitter.
Uandishi wake kwa kiwango kikubwa ulikidhi mahitaji ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wengi hupenda kusoma sentensi fupi fupi na zinazoeleweka kuliko maelezo marefu yenye ajenda tofauti.

Mwigulu Nchemba aibuka
Suala la kufukuzwa kwa Zitto pia limegusa viongozi mbalimbali serikalini akiwamo Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyetumia mtandao wa kijamii wa ‘Jamii Forum’ kuelezea hisia zake kuhusu tukio hilo.
Katika ujumbe wake mfupi ambao uliibua mjadala mkubwa kwa wachangiaji, aliandika akisema kuwa amesikitishwa na taarifa za kuenguliwa kwa Zitto kwenye chama alichoanzia maisha yake kisiasa.
Nikimnukuu zaidi alisema: ‘‘Nakusihi kijana mwenzangu,mwanasiasa mwenzangu na mchumi mwenzangu kuwa, Taifa linakuhitaji wakati huu tunapopambana na ufanyaji kazi wa mazoea na kuleta “mabadiliko kwa vitendo.”Hivyo usikate tamaa Watanzania watakuhesabia mema kwa yote unayoyafanya kwa ajili ya Taifa letu.
Katika mtandao huu ni nadra mwanzisha hoja kubaki jukwaani kukabialiana na mashambulizi ya mada aliyoanzisha, badala yake hukaa pembeni na kushuhudia wapambe wenye mitazamo tofauti wakijibizana.
Mwigulu alimtaja mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kama mwanasiasa aliyeleta chachu ya mabadiliko kwa vitendo kutokana na uwezo wake mkubwa na kuwa adhabu yake siyo kumfukuza bali demokrasia itumike.
Mjadala ulioanzishwa na Mwigulu mpaka leo haukupata hitimisho kutokana na ukweli kuwa wachangiaji wengi walitaka kujua sababu za mwanzisha hoja kusikitika badala ya kufurahi na kumkaribisha kwenye kundi lake.
Katika mazingira ya kisiasa, Mwigulu na chama chake cha CCM walitegemewa wangefurahi kwa kuwa hatua hiyo ilikuwa inatafsiri kudhoofika kwa chama kikuu cha upinzani (Chadema)na kinyume chake walionyesha kusikitika.
Mshangao pia ulionyeshwa na mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Edo Kumwembe ambaye kupitia akaunti yake ya Twitter alijaribu kuhusisha suala hilo na mchezaji bora wa mpira ambaye kila timu ingependa kuwa naye kikosini.
Alisema kilichomshangaza katika suala hilo ni hata Chama cha CCM kulalamika. Kwa mtazamo wake alifikiri huo ulikuwa wakati mwafaka kuona kuwa Chadema inadhoofika na bila kuchelewa wangemsajili Zitto kwa gharama yoyote kwenye timu yao.
Alijiuliza kwa nini CCM wanahuzunika badala ya kufurahi huku akioanisha tukio la mchezaji Amis Tambwe alivyoachwa na timu ya Simba ambaye mpinzani wake Yanga ilimsajili na kumwingiza kwenye kikosi cha kwanza.
Kwenye ‘Whatsapp’ wazodoana
Kwa watumiaji wa mtandao wa whatsapp picha za Zitto zilisambaa kama moto wa nyika zikimuonyesha katika matukio tofauti kuanzia uwezo wake wa kujenga hoja bungeni hadi kwenye majukwaa ya kisiasa.
Watumiaji wa mtandao huo pia walipata nafasi ya kuangalia video fupifupi zilizomuonyesha mbunge huyo machachari akishiriki harakati mbalimbali za kisiasa, ikiwa ni pamoja na msimamo wake wa kusimama upande wa wanyonge.
Tatizo kubwa la mtandao huu kuna picha nyingi za kuchongwa na maneno ya kulishwa.
Hata hivyo, kwa mashabiki wa Zitto Kabwe hilo sio tatizo sana kwao kwani kiongozi huyo wanamjua vilivyo na hata staili ya uandishi wake mitandaoni inajulikana.
Kama ilivyokuwa katika mitandao mingine hata watumiaji wa mtandao huu wamejiunga katika makundi, walijadili hoja ya kufukuzwa kwake kwa mtazamo tofauti na makundi mengi yalionekana kuwaganyika.
Baadhi ya washiriki wa mjadala kupitia mtandao huo walikosoa uamuzi wa Chadema kumfukuza mwanachama waliyeishi naye kwa miaka 19, huku wengine wakimuonyesha Zitto kama shujaa mwoga ambaye ni hatari kumuamini kwenye mstari wa mbele wa mapambano.
Walimtaja kama kiongozi mwenye uwezo wa kujieleza; mwenye kushawishi ambaye pia ni mtendaji wa kile anachokiamini; kwamba siyo kama wengine ambao nguvu yao huishia kwenye upigaji kelele majukwaani.
Pia, katika mtandao huo watumiaji wake walipata andiko lenye sifa zaidi ya ishirini za Zitto Kabwe kama zilivyoorodheshwa na mmoja wa mashabiki wake, akimsifia kama kijana anayesimamia kauli yake bila kujali matokeo mbele ya safari.
Kwa upande wa blogu, ilikosa jipya kuhusu tukio la kufukuzwa kwa Zitto Kabwe ndani ya Chadema na haikuwa na picha za tukio la mahakamani zaidi ya kunukuu taarifa kwenye mitandao mingine ya kijamii.
Sifa ya kwanza ya mitandao ya aina hii lazima iwe na picha za wakati huo ili kikidhi matarajio ya wasomaji. Wengi walitarajia kuona picha za eneo la mahakamani na jinsi watu walivyokuwa wanafurahia au kusikitishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hata blogu za kwanza kusambaza taarifa hizo pia hazikuwa na picha yoyote inayotoa taswira ya tukio la siku hiyo mahakamani.
Pamoja na mapambano yanayoendelea kwenye mitandao tofauti ya kijamii, ipo mijadala inayoonekana kubeba sura ya kitaifa kutokana na historia ya Zitto ndani ya Chadema na mchango wake ndani na nje ya chama.
Suala la kumpinga Zitto Kabwe kwa hofu ya kuogopa kukaribisha mabadiliko ya uongozi ndani ya Chadema ni hoja ambayo kupitia watetezi wake itaendelea kuelea kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu.
Mwananchi

No comments: