Winga hatari wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Ngasa, amewaaga na kuwashukuru mashabiki wake kwa kumpa sapoti katika kipindi chote alichokaa kwenye klabu hiyo ya Jangwani.
Ngasa, mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka jana na mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita, mwishoni mwa wiki alikisaidia kikosi cha wanajangwani kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Ngasa alifunga mabao mawili na kupika mengine mawili, lakini muda mfupi baada ya mechi hiyo aliandika maneno kwenye ukurasa wake wa Instagram yanayoashiria kuondoka Yanga.
“Kwa heri Yanga. Nakupenda, nashukuru kwa kila kitu,” ulisomeka ukurasa wa Ngasa wa Instagram juzi jioni.
NIPASHE ilimpiga simu Ngasa jana mchana, lakini hakupokea huku uongozi wa Yanga ukiweka wazi kwamba atakuwa huru kuondoka Jangwani baada ya msimu huu.
"Kwenye ukurasa ule yale si maneno ya Ngasa, ninadhani kuna mtu ameamua kufanya hivyo. Hata hivyo, Ngasa hajasaini mkataba mpya na Yanga, hivyo yuko huru kujiunga na timu nyingine baada ya kumalizika kwa msimu huu," alisema Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano na Yanga baada ya kutafutwa na NIPASHE kwa simu jana alasiri.
Katika mechi dhidi ya Platinum FC, Ngasa ambaye miezi miwili iliyopita aliweka wazi kutokuwa na furaha Yanga kutokana na deni la zaidi ya Sh. milioni 40 alizowalipa Simba kufanikisha kuwatumikia mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara, hakushangilia mabao yote waliyofunga Jumapili dhidi ya Platinum FC.
Nyota huyo alionekana akikutanisha viganja vyake ikiwa ni ishara ya shukrani huku pia akionyesha ishara ya kulia, kilio ambacho hata hivyo, kilihusishwa na kifo cha kocha Sylivester Marsh aliyemuibua.
Katika ukurasa wake huo, Ngasa aliposti picha yake ya mechi ya juzi akilia na aliambatanisha na maneno hayo.
Mbali na Yanga, mkali huyo wa kufumania nyavu, amewahi kuzichezea timu za Kagera Sugar, Azam FC na Simba.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment