- Waliguswa na wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini
- Meya Silaa apokea vifaa hivyo na kutaka wengine kuiga mfano wa RWG
- Shule bado ina upungufu wa madawati 100,
- Vyumba 7 zaidi vya madarasa vyahitajika na matundu 24 ya vyoo
- Shule pia haina nyumba hata moja ya mwalimu
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jerry Silaa, amewataka Watanzania kwa ujumla kuacha mambo ya siasa katika masuala ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kulalamika bila kushiriki kuisaidia serikali yao.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akipokea msaada wa madawati 50 na vitabu 250, kwa ajili ya Shule ya Msingi Bombambili, iliyoko kata ya Kivule jijini Dar es salaam.
Msaada huo umekabidhiwa kwa meya Slaa, na chama cha Royal Women group cha jijini Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za kusaidia maendeleo ya elimu kwa shule za pembezoni mwa Jiji hilo.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya wanachama wa chama hicho, Mwenyekiti mstaafu, Agness Shayo, alisema msaada huo una thamani ya Sh milioni 10 na vitabu hivyo ni vya masomo ya sayansi, hisabati na Kiswahili kwa darasa la tano hadi la saba.
Katibu mstaafu, Jenister Mchau, chama hicho kilizindua kampeni ya kuchangia elimu katika mazingira rafiki, ili kuwezesha wanafunzi wa shule za umma zenye upungufu mkubwa wa madawati na vitabu kusoma katika mazingira rafiki na hivyo kufanya vizuri.
“Tumeazna safari ya kuchangia maendeleo ya elimu, itakuwa endelevu kwa kila mwanachama kutoa sehemu ya faida yake kwa mwaka kuipa jamii…tumejikita kwenye elimu kwa kuwa tunatambua huwezi kufanya vizuri bila kuwa na mazingira rafiki,” alisema.
Mwenyekiti wa sasa wa Royal, Jane Mwakipunda, alisema chama hicho kina mtaji wa Sh milioni 50 na kinatoa mikopo kwa wanachama wake hadi Sh milioni 10, katika kupiga vita umaskini.
Alisema kampeni hiyo itaendeshwa kila mwaka kwa mikoa wa Dar es Salaam maeneo ya pembezoni yenye upungufu na Pwani, ili kusaidia jitihada za serikali katika kuboresha elimu.
Silaa alisema kwa mwanadamu kumsaidia mnyonge ni sawa na kumkopesha Mungu, na kwamba kilichofanywa na Royal kinapaswa kuigwa na watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Leah John, alisema shule hiyo ina upungufu wa madawati 100, vyumba saba vya madarasa, matundu ya vyoo 24 na hakuna nyumba za walimu.
No comments:
Post a Comment