ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 6, 2015

Gwajima Asema Atakufa na Lowassa na Dr. Slaa, Asisitiza huu sio Muda wa Kuchaguliana Marafiki


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Pia askofu huyo, amewataka waumini wote wa kanisa hilo kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi, Alhamisi ijayo siku ambayo atakwenda kukamilisha mahojiano dhidi ya tuhuma za kumtukana Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.

Akihubiri mamia ya waumini waliofika kanisani hapo kwa ajili ya ibada ya Pasaka jana, Gwajima alisema kumekuwa na uvumi kwamba kuhojiwa kwake na polisi kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na kuzungumza na waumini wake.

Alisema alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996 wakati huo mbunge huyo akiwa Waziri wa Ardhi na tangu kipindi hicho amekuwa mtu wake wa karibu.

Alisema alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994 kabla hajagombea nafasi ya urais kupitia Chadema na kwamba tangu wakati huo amekuwa rafiki wa familia.

“Hawawezi kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa karibu hata kabla hawajawa na ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao karibu,” alisema.

Asimulia mahojiano
Akizungumzia mahojiano yake na polisi, Gwajima aliwaeleza waumini wake kwamba mambo mengi aliyohojiwa hayakuhusiana na suala la kumkashifu Kardinali Pengo.

“Polisi walinihoji mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali ya Pengo yalikuwa machache sana,” alisema.

Hata hivyo, Gwajima alisema hana ugomvi na polisi wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo hivyo. Akitoa mfano, alisema Februari mwaka huu alipeleka barua polisi kueleza anataka kudhamini kampeni kwa ajili ya kupinga mauaji ya albino kwa kushirikiana na jeshi hilo.

“Niliwaeleza kwamba tungezunguka na polisi mikoa yote Tanzania na wamenijibu kwamba nipeleke ratiba ya shughuli hiyo ili tuanze,” alisema.

Alisema pia alidhamini mafunzo ya ulinzi shirikishi kwa vijana 400 kwa kushirikiana na polisi... “Shughuli hizi zinaonyesha kwamba sina ugomvi na polisi, bali nimekuwa rafiki kwa kushiriki katika shughuli zenye masilahi kwa Taifa.”


Viongozi wamiminika
Alisema pia hana ugomvi na Serikali na kwamba viongozi wake wamekuwa wakimiminika katika kanisa lake.

Aliwataja viongozi hao kuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe.

Viongozi wengine, alisema ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na wabunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Vicky Kamata wote wa CCM

“Kama ningekuwa na ugomvi na Serikali viongozi hawa wasingekuja katika kanisa langu kwa nyakati tofauti. Hii inaonyesha nilivyo na uhusiano mzuri na Serikali,” alisema.

Alhamisi ijayo
Askofu Gwajima amewataka waumini wake kumsindikiza katika Kituo cha Polisi siku ambayo atahojiwa kwa mara nyingine. “Nitakwenda Central Police Alhamisi saa moja asubuhi, nawaomba waumini wote mfike katika eneo hilo lakini msilete fujo wala kumtukana mtu, kuweni watulivu wakati wote nitakapokuwa nahojiwa,” alisema.

Askofu huyo alitakiwa kuhojiwa Alhamisi iliyopita lakini polisi waliahirisha kutokana na hali yake kutokuwa ya kuridhisha.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Jeshi la Polisi halitaruhusu mkusanyiko wa watu katika eneo hilo wakati Askofu Gwajima atakapohojiwa.

“Atatakiwa kufika na wakili wake na mtu mmoja ambaye ataona anafaa kuingia naye kwenye mahojiano. Kama kuna waumini wanajiandaa kukusanyika katika ofisi zetu hapa Central Polisi, wafahamu kwamba haturuhusu na wakikaidi tutachukua hatua.”

Ilivyokuwa kanisani
Gwajima alifika katika kanisa hilo lililopo kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe saa 5.00 asubuhi na kupokewa kwa shangwe na waumini walioanza kufika tangu saa 2.00 asubuhi.

Msafara wa magari matatu; Toyota Land Cruiser mbili na Hammer, yaliwasili kwenye viwanja vya kanisa hilo na kulakiwa na waumini walioyazingira kwa shangwe na vigelegele wakitaka kumwona Askofu Gwajima.


Waumini hao walikuwa na shauku ya kumwona Gwajima na walionekana wakisukumana ovyo kila mmoja akitaka kumwona.

Akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na shati jekundu, Gwajima aliteremka katika Hammer akishikiliwa na wasaidizi wake na kukalishwa katika kiti cha magurudumu mawili kilichokuwa kikisukumwa na wasaidizi hao kuelekea kwenye jukwaa la kanisa hilo.

Baada ya kufika, vikundi vya kwaya viliendelea kuimba na kucheza nyimbo mbalimbali za kumtukuza Mungu.

Gwajima alizungumza na waumini wake kuanzia saa 5.30 hadi saa 6.45, akiwaeleza kilichotokea kuanzia siku alipofika polisi kwa mara kwanza, mahojiano hadi alipotoka hospitali.

Katika mahubiri yake, Gwajima alisema ataendelea kuwaonya viongozi wa Serikali na wa dini watakaokosea masuala mbalimbali.


“Sitajali ni kiongozi wa aina gani amekosea nitawakemea. Rais akikosea nitamkemea. Waziri akikosea nitamkemea na viongozi wa dini wakikosea nitaendelea kuwakemea,” alisema.

1 comment:

Anonymous said...

Jamani Gwajima hatoi wala hato wapa pesa wenye media..mtaandika mpaka mtachoka..