ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 21, 2015

JAMII YAASWA KUTOWAFICHA WALEMAVU

 .Mkurugenzi wa Hazina Foundation William Mungai na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Mufindi Community Walefare Amina Rajab wakikabidhi kabati likiwa na madawa mbalimbali kwa  kituo cha Makalala kilichoko mafinga liganga.
  Mkurugenzi wa Hazina Foundation William Mungai na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Mufindi Community Walefare Amina Rajab, wakiwa katika picha ya pamoja na walimu na wanafunzi walemavu wa kituo cha Makalala kilichoko mafinga liganga.

...........................................
NA DENIS MLOWE, MUFINDI

JAMII imewatakiwa kuacha tabia ya kuwaficha walemavu bali kutoa taarifa za watoto hao waliopo kwenye familia mbalimbali kwa lengo la kupata huduma bora  hasa katika sekta ya elimu na afya.

Hayo yamezungumzwa na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Mufindi Community Walefare Amina Rajab wakati wa kutoa msaada wa madawa mbalimbali na nguo kwa walemavu wanaolelewa na kituo cha Serikali cha Makalala kilichoko Luganga Mafinga kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Hazina Foundationi ya mjini humo, William Mungai ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa Chadema na Mgombeo ubunge jimbo la Mufindi Kaskazini.

Amina alisema kuwa kuna wazazi wengi wana kasumba ya kuwaficha watoto wenye ulemavu bila kujua kuwa wanahaki sawa na watoto wasiowalemavu na wakipatiwa elimu wanaweza kuwa wakombozi wa familia hasa katika masomo ya ufundi.

Alitoa wito kwa serikali kuona umuhimu wa kutumia vituo mbalimbali vinavyolea watoto wenye ulemavu kuhakikisha vinawejengea miundo mbinu rafiki na uboreshaji mipango na mfumo wa utoaji elimu, afya na usafiri kulingana na tofauti za umri wa watoto nchini.

Aliongeza kuwa walemavu wanayo haki ya kuishi na kujitegemea iwapo jamii itawajengea uwezo badala ya kuwafungia ndani na kuwaona kama ni mkosi katika familia  ila kugundua vipaji walivyonavyo na kuiwezesha serikali kuwaingiza katika mipango mbalimbali ya kuwapatia huduma

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hazina Foundationi, William Mungai aliomba jamii kubadilika sasa na kuondokana na dhana potofu ya kuwatenga walemavu katika shughuli za kijamii

Alisema kuwa bado elimu zaidi inahitajika kwa jamii ili kuweza kuondokana na mila zisizo na maana za kuwatenga na kuwadharau walemavu katika jamii.

Naye Rahel Kumbo  ambaye ni Mlezi wa kituo cha Makalala kinachofadhiliwa na serikali alitoa wito kwa jamii kuwa walemavu wasifichwe majumbani na badala yake  wapelekwe hospitalini mapema ili wapate matibabu na kuwapatia elimu katika shule husika za walemavu.

Alisema kuwa licha ya nia ya serikali kutaka watoto walemavu wapelekwe shule bado mazingira ya kujifunza katika shule nyingi hayawavutii watoto hawa hali inayosababisha baadhi yao kukacha masomo licha ya kuwa na vipaji vikubwa.

Alisema kuwa serikali imejenga sana shule za kata lakini ujenzi wa shule za walemavu hasa upande wa sekondari umekuwa kikwazo kwa baadhi ya watoto kwa kuwa hali zao za kimaumbile zinawapa ugumu kurandana na hali ya mazingira ya shule.

Alitoa wito kwa serikali kuwa makini na suala zima la ujenzi wa shule unaoendelea kuangalia na walemavu wanapaswa kujengewa vyoo vya kukidhi haja zao,maana hali hiyo ikiendelea walemavu watapata magonjwa mengi na kushindwa kuhudhuria masomo yao.

No comments: