Kama upo kwenye uhusiano na mtu mwenye wivu uliopitiliza kiwango, unatakiwa kuwa makini sana ili msije mkaachana wakati bado mnapendana.Unaweza kuwa umeingia kwenye uhusiano na mtu ambaye kila wakati anataka kukufuatilia kujua unafanya nini, uko na nani na mambo mengine ambayo kwa upande mwingine unaweza kuona ni kero kwako.
Kikubwa hapa ni kutokasirika wala kuhisi kwamba umepata mtu asiyefaa, msumbufu, mwenye wivu wa kijinga. Tambua hiyo ni hulka yake hivyo unachotakiwa kufanya ni kujua namna utakavyokabiliana naye na kumfanya awe na amani kisha uhusiano wenu uendelee.
Kwa kulijua hilo, leo nimeona nikupe njia ambazo unaweza kuzitumia katika kukabiliana na mpenzi au mwanandoa ambaye wivu wake ni balaa. Si kwamba kwa kuyafanya hayo utamfanya asiwe na wivu, ni kwamba wivu wake hautakuwa na madhara na kwa kiasi flani utapungua.
Mshirikishe kwenye ratiba zako
Kama mpenzi wako ana wivu sana ni vyema ukamfanya ajue ratiba yako ikoje kila siku pale inapobidi. Kama uko huru si vibaya kutumia muda mwingi ukiwa naye lakini kama uko mbali, ni vyema ukamfanya ajue.
Ni vizuri akajua muda flani utakuwa wapi na nani, ukifanya nini. Kwenye suala la mapenzi wala siyo kitu kibaya hasa pale ambapo utagundua kwamba ukimpa taarifa anakuwa na amani. Hiyo itamfanya hata pale utakapokuwa mbali na macho yake asiwe na mawazo potofu licha ya kwamba kama anakupenda kweli hatakiwi kukufikiria tofauti.
Watu wajue uhusiano wenu
Ni jambo zuri kumfanya mpenzi wako awe sehemu ya maisha yako. Usimtenge wala kumbagua. Ndugu zako wote, marafiki pamoja na wafanyakazi wenzako itakuwa poa sana kama utamtambulisha kwao.
Usiwe na tabia ya kumuacha nyumbani na kwenda mitoko mbalimbali na marafiki zako au kwenye sherehe bila yeye. Hii itamfanya awe na wivu na ahisi huenda una mwingine wa kwenda naye, mwenye vigezo vya kujulikana kwa marafiki zako na ndugu zako.
Simu iwasogeze karibu
Hakuna kitu kibaya kama kupitisha siku nzima bila kumtumia meseji wala kumpigia simu mpenzi wako. Kumbuka simu ukiitumia vizuri inaweza kukufanya ukawa karibu zaidi na mpenzi wako.
Kwa ulimwengu wa sasa ukiwa ni mgumu kutuma sms wala kupiga simu, mwenzi wako atahisi una mtu mwingine ‘anayeku-keep bize’.
Hata kama uko bize sana na shughuli zako za kila siku, jitahidi kuwasiliana naye angalau kwa siku mara tatu. Mbaya zaidi ni pale ambapo atakutumia sms na usijibu kwa wakati au akakupigia kisha usipokee, hii itamfanya aumie sana na kufikiria vinginevyo.
Thibitisha unampenda
Kumwambia tu unampenda hakuwezi kumfanya mpenzi wako akaamini kwamba unamaanisha. Waswahili wanasema hayo ni maneno tu, hata kwenye kanga yapo.Unachotakiwa kukifanya ni kumuonesha mpenzi wako jinsi gani unampenda na unamhitaji kila mara kwa vitendo. Usiogope kumwambia kila kitu kilichopo moyoni mwako.
Lakini kubwa la kumfanya aamini kwamba unampenda ni kumtendea yale ambayo unajua yatamfanya awe na furaha. Kuwa naye karibu wakati wa furaha na huzuni, mpatilize anachokitaka ambacho kipo ndani ya uwezo wako, muoneshe kwamba kwake umefika, ni kati ya mambo yanayoweza kumfanya atulie na aamini kweli amepata mtu sahihi.
Usizoeane sana na watu wa jinsi nyingine
Kama mpenzi wako ana wivu sana, acha utaniutani na watu wa jinsi nyingine. Ikibidi iwe ni kwa sababu maalum ambazo hata mpenzi wako atazielewa. Kama wewe ni mwanaume, kupigapiga picha na mademu, kuwasiliana nao mara kwa mara na hata kutaniana nao kunaweza kumfanya mwenza wako akajinyonga kama siyo kukuacha wakati bado unampenda.
GPL
No comments:
Post a Comment