ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 16, 2015

MISHENI MAALUM ZA KISIASA ZIWE WAZI NA JUMUISHI-BALOZI MANONGI

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akibadilishana mawazo na Bw. B. Lynn Pascoe ambaye ni kati ya wajumbe 14 wa Tume Huru iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya tathmini kuhusu hali ya sasa ya Operesheni za Ulinzi wa Amani pamoja na Misheni Maalum za Kisiasa. Tume hiyo huru iliyoteuliwa mwishoni mwa mwaka jana imekwisha anza kazi.

Siku ya Jumatano April 15, 20`5  Baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo akiwamo Bw. Pascoe walikutana katika majadiliano yasiyorasmi na Wawakilishi wa Kamati Maalum ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya jumla yahusuyo Misheni Maalum za Kisiasa. Mkutano huo uliandaliwa na Idara ya Siasa ya Umoja wa Mataifa.

Akichangia majadiliano hayo, Balozi Manongi, amesema kwamba Misheni Maalum za Kisiasa, pamoja na umuhimu wake na mchango wake katika mustakabali wa amani na usalama, lakini ni misheni ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na nchi wanachama, hasa kutokana na ukweli kwamba uundwaji wake hauko wazi, si shirikishi wala jumuishi.

Kutokana na mazingira hayo, Balozi Manongi ameishuri Tume hiyo Huru kuliangalia kwa mapana suala la Misheni Maalum za Kisiasa ikiwa ni pamoja na muundo wa uundwaji wake na pia kuboresha uwazi, uwajibikaji na uwakilishi utakaozingatia uwakilishi jumuishi wa kila kanda.

Kama ilivyokuwa kwa wazungumzaji wengi, Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kwamba Taarifa itakayoandaliwa na Tume hiyo Huru itazingatia michango na maoni ya nchi wanachama kwa lengo la kuboresha Operesheni za Ulinzi wa Amani ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi na vilevile kuboresha utendaji wa Misheni Maalum za Kisiasa.

No comments: