ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 16, 2015

Mnyika aipa angalizo serikali kuhusu ajali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Mnyika.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Mnyika, ameitaka serikali kulichukulia kwa uzito tatizo la kukithiri kwa ajali za barabarani, kama ambavyo taifa linavyotumia nguvu kubwa kukabiliana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyofumka kwa kasi kubwa nchini.

Mnyika alisema takwimu za kiwango cha ajali zilizotokea ndani ya siku 102 zilizotolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara, Mohamed Mpinga, zinaonyesha kuwa tatizo hilo ni kubwa, ambalo hatua za haraka zinahitaji kuchukuliwa.

Alisema haitoshi kwa Rais Jakaya Kikwete kuishia kutuma salamu za rambirambi kwa waathirika kila ajali inapotokea, badala yake anachopaswa kukifanya ni kuchukua hatua za kuunganisha nguvu za kitaifa kudhibiti tatizo hilo.

“Angechukulia uzito wa ajali kama taifa linavyotumia nguvu dhidi ya mauaji ya albino, kwani idadi ya wanaokufa kwa ajali ni zaidi ya ile ya albino wanaouawa. Rais aingie kwenye vita kubwa, badala ya kuziachia takwimu za Mpinga, ambazo hazitekelezwi,” alisema Mnyika na kumtaka pia Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kulizungumzia tatizo hilo.

Alisema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa waziri wa uchukuzi, aliwahi kuunda kamati iliyochunguza vyanzo vya ajali nchini.

Hata hivyo, alisema uchunguzi huo ulikamilika, lakini mpaka sasa ripoti imefanywa kuwa siri.
Alimtaka Waziri Sitta kuiweke ripoti hiyo hadharani ili kila mdau ajue na kuunganisha nguvu ya pamoja kudhibiti tatizo hilo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Mremaaa! Mnamkumbuka Mrema alivyokuwa waziri wa mambo ya ndani? unakumbuka lile agizo la Mrema kupiga marufuku safari za Usiku kwa mabasi ya Abiria? Tunahitaji maamuzi makubwa kutoka serikalini. Ajali zitatumaliza. Act NOW