Aliyekuwa Rais wa Simba Aden Rage
Kwa kawaida Simba na Yanga huwa hazishangiliani hata iweje kutokana na upinzani uliopo baina yao.
JUMAMOSI Yanga itashuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuivaa Etoile Du Sahel ya Tunisia katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage, ameamua kuweka kando itikadi zake na kuwataka wana Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia Yanga.
Rage ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini na aliyepanga kukitetea kiti chake katika Uchaguzi Mkuu ujao, alisema Yanga ni wawakilishi pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki, hivyo waungwe mkono.
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa FAT (sasa TFF), alisema Yanga inapeperusha bendera ya Taifa, hivyo ni lazima heshima inayobeba klabu hiyo ithaminike kwa kuungwa mkono uwanjani.
“Watu watake wasitake, Yanga ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania. Inapocheza wimbo wa taifa wa Tanzania hupigwa, siyo wimbo wa Yanga kama kweli upo. Wito wangu kwa mashabiki wote wa soka bila kujali Usimba na Uyanga wajitokeze uwanjani Jumamosi kuipa nguvu Yanga.”
Rage alisema itakuwa ni aibu kama mashabiki watakaofika uwanjani wakaishangilia Etoile ambao ni timu ngeni.
“Hii itakuwa ni aibu kubwa kwetu. Mara zote napenda kusisitiza utani na upinzani wetu hubaki katika ligi ya nyumbani, katika michuano mikubwa kama hii ya kimataifa lazima tupeane tafu kwa sababu inapofungwa Yanga au timu yoyote huangaliwa kama wamefungwa Watanzania wote,” alisema
Aidha Rage alidokeza kuwa wazee wa mjini Tabora wameandaa dua maalum ya kuimbea Yanga ili iweze kupata ushindi katika mchezo huo wa Jumamosi kusudi waendelee kuipeperusha bendera ya Taifa.
“Huku Tabora kuna dua nzito imeandaliwa, lengo ni kuona Yanga inapata ushindi nyumbani, kila Mtanzania kwa imani yake aiombee Yanga ili ipate mtokeo mazuri mbele ya Watunisia,” alisema Rage aliyeliambia Mwanaspoti yupo jimboni kwake kwao kwa mapumziko.
Yanga itaumana mabingwa hao wa zamani wa Afrika katika pambano ambalo ambalo litatoa dira yao katika mbio za kuwania mamilioni ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kama itaingia hatua ya mwisho ya mtoano ya 16 Bora au ndiyo itakuwa imefikia tamati katika michuano ya Afrika kwa mwaka huu.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara walipata nafasi hiyo ya kuvaana na Etoile baada ya kuing’oa FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-1 wakati wapinzani wao waliitoa Benfica de Luanda ya Angola.
CREDIT MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment