Sasa yagundulika aliyeleta mabehewa feki alikuwa na bei ya juu kuliko wote, Aliruhusiwa na kufanyia marekebisho zabuni yake kinyemela
Aidha, imebainika pia kuwa ya Hindustan Engineering Ltd ya India, ambayo ilishinda zabuni hiyo, ilibadilishiwa vigezo (specification), vya aina ya mabehewa kinyemela baada ya zabuni kutangazwa na wazabuni kuwasilisha maombi yao.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo NIPASHE imezipata, kampuni hiyo iliomba kuiuzia TRL mabehewa 174 yenye ‘rubber’ badala ya ‘spring’ kwa dola za Marekani 18,209,317.50 (Sh. bilioni 32.8) wakati kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa yenye viwango vinavyokubalika kwa dola za Marekani 13,907,907 (Sh. bilioni 25).
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni hiyo ambayo ilihusisha kuleta mabehewa mengine 100 ya mizigo ambayo ni ya muundo wa matangi (tank wagon) na yasiyofunikwa (flat wagon) kwa dola za Marekani 10,278,182.50 (Sh. bilioni 18.5) wakati kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China iliyokuwa ndiyo yenye bei ndogo ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa kwa dola za Marekani 7,272,975 (Sh. bilioni 13.09).
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni ya kuiuzia TRL vipuri kwa thamani ya dola za Marekani 2,561,187.50 (Sh. bilioni 4.4) baada ya kuirekebisha na taarifa ya zabuni inaonyesha kuwa iliwasilisha zabuni iliyorekebishwa na ilikubaliwa.'
Kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd iliomba kuleta vipuri hivyo kwa dola za Marekani 2,475,835 (Sh. bilioni 4.46) wakati kampuni nyingine kama Transnet iliomba kwa dola za Marekani 3,108,687 (Sh. bilioni 5.6) wakati Modern Industries iliyoshindwa kwa kutowasilisha dhamana iliomba kwa dola za Marekani 3,344,925 (Sh. bilioni 6.02).
Kwa ujumla taarifa zinaonyesha kuwa kampuni ya Hindustan Engineering ililipwa dola za Marekani 31,048,688 (Sh. bilioni 55.9) wakati kampuni iliyokuwa ya bei ndogo kuliko zote ingeweza kufanyakazi hiyo kwa dola za Marekani 24,368,757 (Sh. bilioni 43.86) hatua ambayo ingeokoa dola za Marekani 6,677,931 (Sh. bilioni 12.02) na kutoitumbukiza nchi kwenye hasara hiyo ya mabehewa feki.
“Mabehewa nyenye rubber hayawezi kabisa kwa namna yoyote ile kupita kwenye reli yetu. Kilichotokea ni kwamba zabuni iliyotangazwa ilitaka wazabuni walete mabehewa yenye spring ambayo ndiyo sahihi, lakini baadaye inaonekana walibadilisha vigezo na kuielekeza kampuni waliyoipa zabuni vigezo vipya ndiyo maana unaona mabehewa yaliyokuja hayafai,” alisema mmoja wa wataalam wa reli ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka dhamana yoyote jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma na ilitaka ilipwe fedha yote kabla ya kuingiza mabehewa nchini jambo ambalo TRL ilitekeleza.
Wakati mzabuni huyo akiweka masharti hayo, kampuni nyingine zilizoomba ikiwamo iliyokuwa ya bei ndogo zaidi, iliweka dhamana na ilitaka ilipwe kwa awamu hadi itakapokamilisha kazi husika.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa pamoja na kwamba kampuni ya Hindustan Engineering Ltd ilikuwa ya gharama kubwa iliomba kufanya kazi hiyo kwa miaka miwili, wakati kampuni nyingine zilizoshindana kwenye zabuni zingeweza kufanya kazi hiyo kwa miezi tisa hadi mwaka mmoja.
Kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka gharama za matengenezo wakati kampuni nyingine zote ziliweka.
Taarifa zinaonyesha kuwa kampuni nyingine zilikosa sifa za kushinda zabuni kwa kutowasilisha dhamana (bid security), ikiwamo ile ya Modern Industries, DCD rolling stock ambayo pia iliwasilisha bei zilizokuwa na kasoro za kiuandishi pamoja na Lucky Export.
Kampuni nyingine zilizoomba zabuni hiyo ni Caeic Beigin Ltd, CNR Import and Export Corporation Ltd, Hyunan Construction Engineering Ltd, Texmaco Rail and Engineering na Transnet.
Taarifa hizo zimeibuliwa siku sita tu baada ya Alhamisi iliyopita Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kuwasimamisha kazi vigogo watano wa TRL, akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wake, Kipallo Kisamfu, kutokana tuhuma za kuihujumu serikali katika sakata la ununuzi wa mabehewa feki 274 ya mizigo na kuisababishia hasara ya Sh. bilioni 230.
Wengine waliosimamishwa ni Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles; Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Sitta alisema baada ya kuwasimamisha vigogo hao, utafanyika uchunguzi dhidi yao kwa wiki tatu kuanzia wiki iliyopita.
Kufuatia uamuzi huo, Sitta alimteua aliyekuwa Mhandisi wa TRL, Elias Mshana, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kusimamia kuundwa kwa kamati ya uchunguzi huo.
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta alichukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya kamati iliyoundwa na Waziri aliyemtangulia wizarani hapo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo imegundua kuwako kuna hujuma mbalimbali katika kuendesha TRL.
Kabla ya kuchukua uamuzi wa jana, Waziri Sitta aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya Reli kupitia taarifa hiyo na kutoa maelezo kwake juu ya suala ya ununuzi wa mabehewa hayo.
Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye amekuwa akijihusisha na biashara nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio na baadhi kuanguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini na yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi wa TRL ili kuthibitisha ubora wake.
Jana NIPASHE lilimtafuta Waziri Sitta kuzungumzia taarifa hizo bila mafanikio kutokana na simu zake za mkononi kushindwa kupatikana.
Hata hivyo mmoja wa walinzi wake aliliambia NIPASHE kuwa waziri huyo alikuwa kwenye kikao ambacho hata hivyo hakueleza kilikuwa kinafanyikia wapi.
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
Kila kona wizi mtupu maskin Tanzania yangu,tatizo ni ajira za kujuana
Huu ni uzembe usiopimika na uchunguzi wote ukamilishwe na hatua kuchukiliwa kwa kopo lote lolilohisika na sakata hii! Hii ni aibu kwa Taifa! Hatuwezi kuendeleza nchi kwa uzembe wa kila siku na fedha kuingizwa kwenye njia zisizoleta maendeleo.
Post a Comment