ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 16, 2015

'Bwege' adai wananchi ndio wameochoka kuibeba Serikali ya CCM


Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Said Bungara ‘Bwege’ Pichani (CUF), ametofautiana na wabunge wenzake wa upinzani wanaosema Serikali ya CCM imechoka, badala yake amesema Watanzania ndio waliochoka kuibeba.

Alisema wapo wabunge wanaoitetea serikali, kwa kuibeba, lakini wapo wabunge wanaofanya kazi zao za kuikosoa.

Akichangia hotuba ya mwelekeo wa kazi za serikali, makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2015/16 iliyowasilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Jumanne iliyopita, Bwege alisema serikali haijachoka kama wengine wanavyosema isipokuwa waliochoka ni Watanzania wanaoibeba.

Alisema kwa kuwa Watanzania wanaoibeba serikali hiyo wamechoka, wamejiandaa kuiondoa madarakani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kuwaweka wagombea wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) madarakani.

Huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere kwamba, ‘chama legelege huzaa serikali legelege’ alisema Serikali ya CCM ijiandae kufunga virago.

“Fungeni virago muondoke…anakuja mbunge hapa na kusema serikali imejenga shule, zahanati halafu baadaye wanaomba/wanalalamika miradi ya maendeleo katika majimbo yao haijatekelezwa.

“Wabunge wa CCM wamechoka, wanajiaga wenyewe,” alisema.

Alisema kwa mfano, patasi haifanyi kazi mpaka igongwe, na ndivyo ilivyo kwa CCM haifanyi kazi mpaka igongwe.
Alisema katika jimbo la Rais Jakaya Kikwete aliahidi kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita nne lakini hadi wakati huu barabara hiyo haijajengwa.

Hata hivyo, alisema anamwomba Rais Kikwete kwenda Kilwa kufungua barabara hiyo siku ya kuadhimisha sikukuu ya wakulima.

Hali kadhalika alisema Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, ameshindwa kutekeleza mradi wa maji wa Sh. milioni 800 katika jimbo hilo.

Hoja ya kuchoka kwa Serikali ya CCM ilitolewa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), Jumanne iliyopita akiituhumu serikali hiyo kwa kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Tangu siku hiyo wabunge wengi wa upinzani wanaochangia hotuba ya Waziri Mkuu wamekuwa wakitumia lugha hiyo huku wabunge wa CCM wakijitutumua kuitetea kuwa haijachoka.


CHANZO: NIPASHE


No comments: