ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 17, 2015

CCM YATANGAZA TAREHE ZA VIKAO VYAKE VIKUBWA VITAKAVYOFANYIKA MJINI DODOMA

 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye akifafanua jambo mbele ya waandishi wa Habari leo (hawapo pichani) ,jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kubadilika kwa tarehe ya mkutano wao kufuatia kuingiliana na Mkutano wa Baraza la Wawakilishi.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye Akizungumza na waandishi wa Habari leo, jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kubadilika kwa tarehe ya mkutano wao kufuatia kuingiliana na Mkutano wa Baraza la Wawakilishi.

Na Chaalila Kibuda

Chama cha Mapinduzi (CCM),kinatarajia kufanya vikao vyake mjini Dodoma,ambapo Mei 22 kitafanyika kikao cha kamati kuu ya CCM,na kufuatia kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Taifa kitachofanyika Mei 23 na 24-2015 mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa Habari ,jijini Dar es Salaam,Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,Ndugu Nape Nnauye amesema kuwa kubadilika kwa siku za mikutano hiyo kunatokana na kuingiliana na Mkutano wa Baraza la Wawakilishi.

Nape amesema vikao vyote vikubwa vitafanyika mkoani Dodoma,ambapo ajenda mbalimbali zitatolewa ikiwa ni pamoja na maoni ya Ilani ya CCM 2015-2020 ambayo itawasilishwa na Kamati iliyoundwa kwa kazi hiyo.

Amesema kutakuwa na vikao vya kawaida Mei 21 hadi 22 ambavyo vitakuwa vinafanyika mkoani Dodoma na Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Kamati kuu  ya CC na Halmashauri Kuu (NEC).

Nape amesema vikao hivyo vitaongozwa na Mwenyekiti wa CCM,Rais Jakaya  Kikwete katika kujadili masuala mbalimbali ikiwemo hali ya siasa ya chama hicho.

Wakati huo huo Nape amesema kuwa wanachama sita  waliofungiwa  bado hatma yake kutokana na suala hilo linashughulikiwa na kamati mbili ambazo ndizo zinaweza kusema kifungo kinaendelea ama la,amesema na kuongeza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM)  kinaongozwa na kanuni ambazo yeye mwenyewe amezikuta hivyo ni lazima wanachama na makada wazifuate kanuni na miongozo ya chama.

Amesema wanachama kutangaza nia ya kugombea sio tatizo lakini mazingira yanayoendana baada ya kutangaza nia hiyo ndipo kanuni na miongozo ya chama inaanza kutumika,amesema kanuni na miongozo ya CCM zinasema mtu ambaye yuko kwenye kifungo katika chama haruhusiwi kugombea nafasi yeyote ndani ya chama ambazo zipo wazi.

Amesema mikutano hiyo itajadili jinsi gani watu watapochukua fomu,urudishaji wa fomu pamoja na njia ambazo zitatumika katika utangazaji nia kwa wagombea kutokana na mazingira yaliyopo.

No comments: