ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 4, 2015

HALMASHAURI MKOANI DODOMA ZAUNGA MKONO JUHUDI ZA FPCT, ERIKS

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi, Fredrick Kayambo akisisitiza jambo.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Elias Kaweya akizungumza.Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja akitoa hutuba.

Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja (wa kwanza kushoto) akiwa meza kuu.Bwana Lucas Mhenga akisisitiza jambo.
Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wenye Ulemavu mkoa wa Dodoma akielezea changamoto wanazopitia.

Halmashauri za Wilaya za Chamwino, Bahi na Dodoma Mjini, mkoani Dodoma zimeunga mkono jitihada zinazofanywa na Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania ‘FPCT’ kwa kushirikiana na Taasisi ya Sweden ya ERIKS Development katika kuwasaidia watoto wenye ulemevu.

Wakizungumza katika nyakati tofauti kwenye semina iliyofanyika hivi karibuni ndani ya Ukumbi wa KKKT Dodoma ya kuwajengea uwezo viongozi wa baraza la watoto wenye ulemavu, kamati ya baraza inayolea watoto wenye ulemavu pamoja na wazazi wa watoto wenye ulemavu Mkoa wa Dodoma, viongozi hao kutoka halmashauri hizo walieleza kuwa, watahakikisha watoto hao wanapata haki zao na sheria zinazowalinda zinafuatwa.

Katika siku ya kwanza ya semina hiyo, Afisa Ushawishi na Uteteti wa mpango huo, Josephat Tonner alitoa elimu juu ya haki za watoto wenye ulemavu huku akiwashirikisha pia watoto wenyewe pamoja na wazazi wao waliohudhuria.

Aidha, mtaalam wa masuala ya sheria, Gedion Mandesi naye alipata fursa ya kuelezea sheria zinazomlinda mtoto mlemavu pamoja na mikataba ya kimataifa inayompa mtoto mlemavu haki ya kuishi kama wanavyoishi watoto wengine.

Naye mratibu wa masuala ya watoto wenye ulemavu kutoka FPCT, Lucas Mhenga aliwataka wazazi pamoja na watoto wenye ulemavu kuangalia nini wanaweza kukifanya wakati wakisubiri serikali ichukue nafasi yake katika kuhakikisha haki za mtoto mlemavu zinafuatwa.

Katika siku ya pili ya semina hiyo, viongozi mbalimbali mkoani humo wakiwemo maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo ya jamii, walishiriki ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja.

Kama ilivyokuwa siku ya kwanza, siku hiyo watoto waliendelea kuelezea changamoto wanazopitia sambamba na haki zao za msingi ambazo wanaona hawazipati.Katika kuonesha kuwa halmashauri za mkoa wa Dodoma zinaunga mkono jitihada za FPCT, viongozi mbalimbali kutoka Bahi, Chamwino na Dodoma walieleza namna watakavyochukua nafasi zao kuhakikisha watoto hao wanapatiwa mahitaji yao muhimu na kuwafanya waishi katika mazingira salama.

Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja katika hutuba yake kwanza aliwapongeza FPCT kwa juhudi wanazofanya za kuwajengea misingi imara watoto walemavu kwa kuanzisha mabaraza ya watoto walemavu sambamba na kuandaa semina mbalimbali.

Akaeleza kuwa, wao kama serikali watahakikisha wanaweka mazingira bora ili watoto hao wapate haki zao za msingi lakini pia itachukua hatua stahili kwa wote watakaokaidi sheria zinazowalinda watoto wenye ulemavu
Akahitimisha kwa kuahidi kuwa, atahakikisha katika mkoa wa Dodoma, watu wenye ulemavu wanapewa upendeleo katika ajira na kwamba atalisimamia hilo lakini akawataka watoto hao kutojiona wanyonge bali wapaze sauti na vyombo husika vitawasikiliza.


(Habari/Picha: Amran Kaima)

No comments: