ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 4, 2015

Kilichoing'oa Yanga kwa Etoile hiki hapa.

Safari ya Tanzania katika michuano ya kimataifa mwaka huu ilihitimishwa juzi usiku baada ya Yanga kutolewa kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Etoile Sportive du Sahel (ESS) katika mechi ya marudiano ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Sousse, Tunisia.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Aprili 18, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, hivyo matokeo ya juzi yalimaanisha kuwa Yanga imeng'oka kwa jumla ya mabao 2-1.

Yanga ilifika hatua hiyo ya mbali zaidi ukilinganisha na timu zote nyingine tatu za Tanzania, Azam FC, KMKM na Police Zanzibar zilizotolewa katika hatua ya kwanza ya michuano ya Afrika ngazi ya klabu mwaka huu.

Hata hivyo, Yanga inapaswa kuyafanyia kazi mambo kadhaa ambayo ni wazi yamechangia kung'olewa kwao dhidi ya ESS juzi.

USAJILI WA VIONGOZI
Sehemu kubwa ya wachezaji wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga wanasajiliwa na viongozi wenye fedha ambao hawaujui mpira. Kikosi cha Yanga kilichocheza dhidi ya ESS juzi kilikosa mshambuliaji mwenye umbo kubwa na mrefu.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita, Amissi Tambwe, alizidiwa mbinu na mabeki wa ESS ambao ni warefu na wana faida nyingine ya kuwa na miili mikubwa.

Endapo benchi la ufundi la Yanga lingesajili wachezaji wa Yanga msimu huu, bila ya shaka shughuli ingelikuwa pevu kwa mabingwa wa zamani wa Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ESS.

Katika mechi ya juzi Tambwe alipiga shuti moja la mguu wa kushoto ndani ya boksi lililodakwa pamoja na vichwa viwili, kimoja kikidakwa na kingine kugongesha nguzo.

Pamoja na kuwa na umbo kubwa, mshambuliaji Mliberia Kpah Sherman, alipotea katika mechi ya juzi na hakuwa na msaada kwa kikosi cha Yanga. Alicheza kibinafsi zaidi akijaribu kupiga chenga bila ya mafanikio ukuta mzito wa wachezaji sita-saba wa Etoile kila mara hata katika wakati ambao angeweza kuwapasia wachezaji wenzake. Hadi anatolewa katika dakika ya 64 na nafasi yake kuzibwa na Hussein Javu, mshambuliaji huyo mwenye mabao mawili VPL msimu huu, alikuwa amepiga mashuti mawili akipaisha kwa kukosa utulivu katika dakika ya 33, kabla ya kupiga nje katika dakika ya 54. Kwa kifupi, Yanga ilikosa mshambuliaji mwenye nguvu kuipa wakati mgumu ESS.

BASI LA ESS
ESS walikuwa wazuri kwa kupaki basi juzi. Katika dakika 24 za mwanzo wenyeji walikuwa wamepiga kambi kwenye lango la Yanga wakisaka bao kwa nguvu. Ubora wa Kelvin Yondani na Mbuyu Twite ndiyo ulioiokoa Yanga kufungwa mabao mengi katika kipindi hicho ambacho ESS walipiga mashuti nane, moja halikulenga lango. Katika kipindi chote hicho kulikuwa na mabeki wawili wa ESS waliokuwa hawavuki mstari wa kati kuingia eneo la Yanga, lakini baada ya kupata bao katika dakika ya 24, waliacha mchezaji mmoja mbele na kupaki basi mithili ya Chelsea ya Jose Mourinho.

Hata waliposhambulia kwa kushtukiza, waliacha wachezaji 6-7 ndani ya eneo lao na Yanga ilikosa mbinu na wachezaji wa kukitegua kitendawili hicho kigumu.

Licha ya kucheza pungufu kwa mchezaji mmoja kuanzia dakika ya 42, ESS walikuwa wazuri kuzidi Yanga katika kulinda lango lao na kukaba. Hawakuruhusu Yanga ipige mashuti mengi langoni kwao. Katika mechi yote Yanga ilipiga mashuti sita, mawili yakilenga lango na kudakwa, ikiwa ni wastani wa shuti moja kila baada ya robo saa ya mchezo.

MABEKI WA PEMBENI
Ingawa kiwango cha Oscar Joshua cha juzi kilikuwa kizuri ukilinganisha na mechi kadhaa zilizopita, mabeki wa pembeni wa Yanga bado wana upungufu. Mabao yote ambayo Yanga walifungwa Botswana dhidi ya BDF XI FC yalitokana na makosa ya mabeki wa pembeni. Mathalani, katika mechi ya juzi, goli walilofungwa lilitokana na kosa la beki wa pembeni kulia, Juma Abdul. Mfungaji alipiga kichwa akiwa peke yake (free header). Ingawa mpira wa krosi uliombabatiza Yondani kabla ya kumfikia mfungaji, Yanga ilionyesha udhaifu wa kukosa mawasiliano na kuwaacha baadhi ya wachezaji wa wapinzani wao wakiwa huru. Makosa yakeyale ya mabao mawili ya Botswana.

MCHEZO WA MAONYESHO
Yanga kama kawaida yao walirudia kosa la kucheza mchezo wa maonyesho (show game) juzi. Walipiga pasi na chenga nyingi kuliko wenyeji. Hadi dakika 90 za refa Dennis Batte kutoka Uganda zinakamilika, Yanga walikuwa wamemiliki mpira kwa 51% dhidi ya 49% za wenyeji, lakini hii haikuwa na mantiki yoyote kwa Wanajangwani maana Yanga ilihitaji mabao ili isonge mbele na si kucheza soka la burudani na kufurahisha mashabiki.

REKODI ZILIWATISHA
Karibu wachezaji wote wa Yanga walicheza mechi wakiwa na hofu kubwa, pengine kutokana na rekodi za timu yao inapokutana na timu za Kaskazini mwa Afrika.

KUWAKOSA CANNAVARO, NIYONZIMA
Yanga ilikosa uongozi uliozoeleka wa nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye alifunga goli lao jijini Dar es Salaam kwa penalti ya dakika ya kwanza.

Kutokuwapo pia kwa kiungo injini ya timu, Haruna Niyonzima, kulipunguza ubunifu kuanzia eneo la katikati ya kiwanja kuelekea jirani na lango la wapinzani ambalo lilijaza msitu wa mabeki.
CHANZO: NIPASHE

No comments: