ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 18, 2015

MEYA KINONDONI AANZA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS LA KUONDOA MAJI KATIKA MAENEO YALIYOATHIRIWA NA MAFURIKO MBWENI, BOKO

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akikagua athari za mafuriko katika eneo la Mbweni, Dar es Salaam alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mvua zilizokuwa zikinyesha mwishoni mwa wiki jijini.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda wakiangalia athari za mafuriko wakati walipotembelea maeneo yya Mbweni, Boko na maeneo mengine yaliyoathiriwa na mvua zilizonyesha kwa mfululizo jijini hivi karibuni.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa viongozi wa Kata ya Mbweni wakati kuhusu athari za mafuriko zilizosababishwa na mvua zilizonyesha mfululizo jijini, Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya ukaguzi katika maeneo ya Boko, Mbweni na mengine yaliyoathiriwa na mvua hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mck Sadick (mbele), Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda na viongozi wengine wakikagua athari za mafuriko katika maeneo ya Mbweni wakati walipofanya ziara maeneo hayo mwishoni mwa wiki, jijini.

Na Mwandishi wetu

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick kwa kushirikiana na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda wameanza kutekeleza agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete la kuondoa maji katika makazi ya watu kwenye maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo yaliyosababishwa na mvua zilizokuwa zikinyesha jijini hivi karibuni.

Rais Kikwete alitoa agizo hilo wiki iliyopita wakati alipofanya ziara katika maeneo ya Namanga, Nyaishozi, Dawasco na Basihaya kuangalia athari za mafuriko zilizosabaisha wananchi kuyakimbia makazi yao.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuanza kuyaondoa maji katika maeneo hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, Sadick alisema maji yaliyojaa katika maeneo ya Basihaya na Nyaishozi yanatolewa kwa pampu na kuelekezwa katika bwawa la Dawasco ambako yatatolewa na kuelekezwa kwenye mtaro mkubwa ambao umeanza kuchimbwa kwa ajili ya kuelekezwa baharini.


Alisema zoezi hilo linafanyika kwa haraka ili kuweza kuwafanya wananchi kurudi kwenye nyumba zao na kuishi kama zamani.

Alisema baada ya zoezi hilo la kuondoa maji katika makazi ya watu kukamilika wataanza taratibu za kujenga miundombinu ya kudumu ili maji yasiweze kutuama tena katika maeneo hayo pindi mvua kubwa inaponyesha.

Aliongeza kuwa katika kufanya ukaguzi katika maeneo yaliyojaa maji wamebaini kuwa kuna wananchi ambao wamejenga katika sehemu ambazo haziruhusiwi ikiwemo kujenga kwenye mikondo ya maji.

"Nitumie nafasi hii kuwataka wananchi ambao wamejenga katika maeneo hatarishi kuondoka ili kuacha kuingizia serikali hasara zisizokuwa za lazima,"alisema Sadick.

Alisema watu wote ambao wapo maeneo ambayo ni hatarishi ni vema wakaondoka na kama wanahitaji viwanja vya kujenga nyumba wakafanya mawasiliano na uongozi wa manispaa ya Kinondoni ili waweze kuuziwa viwanja mbadala badala ya kuendelea kukaa sehemu ambazo ni hatari kwa maisha yao.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda alisema kuanzia sasa wataanza kufanya uhakiki ili kubaini watu ambao wamejenga katika maeneo ambayo hawaruhusiwi ili kuweza kuwaondoa ili kuepuka hasara ambayo Serikali inaipata pindi linapotokea suala la mafuriko kama ilivyo sasa.

“Niwaahidi tu kuwa tutaanza kufanya uhakiki ili kubaini watu walojenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa waanze kuondoka mara moja. Na hii ni kwa sababu ya kuepuka hasara za mara kwa mara zinazoipata Serikali.” Alisema.

Katika Kata ya Bunju, zaidi ya nyumba 120 ziliathiriwa na mafuriko hayo na wananchi kulazimika kuyakimbia makazi yao.

1 comment:

Anonymous said...

Hali ya picha hii inanikumbusha metalized ya kuwa"usipoziba ufa utajenga ukuta".kwani waheshimiwa hawajui waanzie wapi.wakati solution ilikuwa ni kuweka good master plan zinazozingatia drainage system.