ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 1, 2015

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, LAZARO NYARANDU AAGIZA ASKARI WA MAREKANI KUONDOKA KATIKA HIFADHI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na waandishi wa habari mjini Mwanza jana juu ya askari wastaafu wa Marekani wanaodai kuwa nchini kupambana na ujangili. (Picha na Loveness Bernard)

NA LOVENESS BERNARD, Mwanza

Waziri wa Maliasili na Utali, Lazaro Nyalandu amekipiga marufuku kikundi cha wanajeshi wastaafu wa Marekani (Vetpaw) ambacho kinadai kupambana na majangili nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri Nyalandu alisema kuwa kikundi hicho kimekuwa kikitumia mitandao kujitangaza kuwa kinapambana na majangiri kwa kuwapiga risasi za vichwa kinyume na sheria.

“Naagiza wakurugenzi wa Mamlaka ya Ngorongoro, Tanapa na Mkurugenzi wa Idara ya wanyamapori kuhakikisha wamarekani hao wanaondoka katika hifadhi mara moja,”alisema Nyalandu
Waziri Nyalandu alisema hakuna askari kutoka nje ya nchi anayeruhusiwa kuingia katika hifadhi akiwa na silaha kwani jukumu la kupambana na majangili nchini linafanywa na askari wa wanyamapori.

Alisema watu hao ambao ni wazushi na waongo wanachafua jina la nchi na kuchangisha fedha duniani kwa kudanganya kuwa wanapambana na majangili nchini.

Aliagiza mamlaka ya NCAA kufuta makubaliano yeyote waliofanya ama kama walikuwa na nia ya kufanya na matapeli hao.
“Vetpow hairuhusiwi kujiingiza katika shughuli zozote za uhifadhi nchini, kazi hiyo inafanywa na vikosi maalum vya walinzi wa wanyapori” alisema.

1 comment:

Anonymous said...

kwani vipi tena? mbona walikuwa na Mhe kule marekani washington DC walipokutana?