ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 8, 2015

KAMISHNA WA SENSA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KITETO MKOANI MANYARA

Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Hajjat Amina Mrisho Said akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu nia yake ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kiteto lililoko mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kulia kwake ni mume wake Alhajj Abeid Omary Khamis.
baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Hajjat Amina Mrisho Said wakati akitangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kiteto lililoko mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Hajjat Amina Mrisho Said ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kiteto lililoko mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Hajjat Amina Mrisho Said amesema iwapo atateuliwa na CCM kuwa mgombea wa Jimbo la Kiteto, atahakikisha anatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuleta maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.

Ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 na kufanikisha ujenzi wa Chuo cha VETA jimboni ili vijana waweze kupata elimu ya stadi za kazi na hatimaye waweze kujiajiri.

Kuhusu suala zima la ufugaji, Hajjat Amina amesema atahamasisha uendelezaji wa ufugaji wenye tija kwa kuifuatilia Serikali ili iweke miundombinu katika maeneo yote ya wafugaji jimboni.

Vipaumbele vingine ni pamoja na kuhamasisha ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao hasa mahindi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya matumizi ya stakabadhi ya mazao gharani na kuwashirikisha wananchi wote katika kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao.

Hajjat Amina Mrisho Said kitaaluma ana Shahada ya Uzamili wa Mifumo ya Kompyuta na amewahi kuwa Mkuu wa mkoa wa Iringa na Pwani ambapo kwa sasa ni Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

No comments: