ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 13, 2015

Mrembo Sitti: Nilitaka kujiua

Dar es Salaam. “Nilitaka kujiua kwa njia yoyote ambayo ningeona inafaa, lakini nilirudisha moyo nyuma kwa sababu ingekuwa shida kubwa nyumbani.”
Hayo ni maneno ya aliyekuwa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu aliyeamua kulitema taji hilo la ulimbwende baada ya kubebeshwa kashfa za udanganyifu wa umri wakati akishiriki mashindano hayo.
Aliongeza: “Sikuwa na amani, niliishi maisha ya hofu, kujifungia ndani, kulia wakati wote. Ilifikia hatua baba yangu alipata mshktuko kiasi cha kwenda kutibiwa Afrika Kusini. Mama yangu pia alipata mshtuko...ningeweza kumpoteza.”
Anazikumbuka siku 30 za majonzi na maumivu, ambazo kwa kiasi kikubwa zilimuathiri mama yake mzazi ambaye ndoto za binti yake kwenye mashindano ya urembo zilifika tamati.
“Mama yangu alisali na mimi, alinipigania, hakuonyesha hadharani jinsi gani anaumia, lakini ukweli ni kwamba nilimwona alivyokuwa anadhoofu na kukosa raha. Nyumba yetu iligeuka sehemu ya huzuni, amani ilitoweka ni kama tulikuwa na msiba.”
Sitti anasema siku moja mama yake alimwambia: “Sitti mwanangu, nilipompoteza mama yangu nililia na kuumia sana, lakini machungu ninayoyasikia sasa na utu uzima wangu ni mazito.”
“Sikutamani kumwona mama yangu analia, iliniuma na hata sasa nawaza machungu na maumivu aliyopitia kwa ajili yangu,” anasema na kuongeza: “Asichokijua mama, siku moja nilikuwa natoka chumbani kwangu nikimwangalia mama akiwa na gazeti lililokuwa na habari yangu. Nilishikwa na uchungu na kurudi chumbani, niliona kama vile dunia imeniangukia.”
“Wakati huo wote baba yangu alivumilia bila kuonyesha maumivu yake, daima alikuwa mtulivu na japo alipinga vikali mimi kushiriki Miss Tanzania,” anasema Sitti.
Baba aliniambia: “Mwanangu usijali, hivi siyo vita vyako tena, sidhani kama sasa wanakutafuta wewe tena, utabaki kuwa mwanangu.”
Anasema kuna wakati baba yake alikwenda Afrika Kusini na akiwa huko alimtumia ujumbe wa kumuomba msamaha na alimwambia kwamba hizo ni changamoto.
“Aliniambia yeye alikuwa na wasiwasi na mimi, lakini kwa upande wake yupo vizuri, hajawahi kuandikwa sana, lakini kama mzazi ilimuuma sana.”
Sitti anasema alikuwa katika wakati mgumu kiasi cha kufikia uamuzi wa kutupa laini yake ya simu ya zamani.
“Wakati huo nilikuwa sisomi sana magazeti, nilikuwa naingia kwenye blogu na mitandao. Kwenye Instagram nilishuhudia vikiandikwa vitu ambavyo sivijui kabisa,” anasema.
“Marafiki walijitenga na mimi, nadhani sababu ilikuwa ni kunipa muda wa kufanya uamuzi kwa yale yaliyokuwa yakiniandama.
“Wakati mwingine nilikuwa najikuta ninalia, halafu ninacheka yaani ni maumivu makali ambayo sikuwahi kuyafikiria, siku zilikuwa zinatofautiana.”
Sitti anasema suala hilo japokuwa lilikuwa baya kwa upande wa baba yake ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, lakini anahisi lilimjenga kisiasa.
“Katika mambo ya siasa, suala langu limempa mwanga baba ingawa kuna watu walitegemea angeporomoka,” anasema.
Ili kuepuka kushambuliwa kwenye mitandao, Sitti anasema aliamua kujiondoa kwenye mitandao yote kwa miezi kadhaa.
“Nilijitoa kwenye Facebook, Instagram, Twitter na katika mitandao mingine tangu Mei mwaka jana, maana nilifikia hatua nikajiona kama napata adhabu.”
Sitti anasema baada ya yote hayo, anaami ipo siku mambo yatakwenda sawa na atakuwa na mchango wa kuielimisha jamii kuondoa dhana na mitazamo isiyokuwa na ukweli kupitia mitandao.
Hata hivyo, anasema siyo sahihi kuweka maisha ya faragha ya mtu mitandaoni bali ni vyema kutumia namna nyingine ya kufikisha taarifa hizo.
Alipoulizwa kama anafahamu ni nani aliyetoa nyaraka zake za vyeti vya kuzaliwa, pasi ya kusafiria, leseni ya udereva Sitti alisema hadi leo hafahamu.
Licha ya hekaheka aliyoipata mrembo huyo aliyetoka Kanda ya Temeke, anasema familia yake ndiyo iliyoathirika zaidi.
Mwananchi

No comments: