Kada wa CCM kutoka Wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, akimkabidhi, Mbunge wa Jimbo hilo, William Ngeleja (wa pili kulia) kiasi cha Shilingi Milioni moja kwa ajili ya kuchukulia fomu ya urais. Picha na Aidan Mhando
Mwanza. Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akiahidi kupambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi ambayo ni umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Akitangaza nia hiyo kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza jana, Ngeleja alisema anatambua kwamba Watanzania wa leo wanatamani kumpata rais ambaye atapambana kwa dhati na vitendo na maadui hao.
“Nina mikakati madhubuti ya kujibu swali la kiutafiti linaloonyesha kwamba mamlaka, idara na taasisi za umma zenye dhamana kubwa ya maisha ya Watanzania mfano, Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na watendaji wakuu wa taasisi za biashara (CEO) ndiyo wanaoongoza kwa tuhuma za kupokea rushwa,” alisema.
Ngeleja akiwa ameambatana na mkewe, Blandina na Mwenyekiti wa Kamati yake ya Maandalizi, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu waliingia ukumbini saa sita mchana na kupokewa na makada wa CCM waliohudhuria ambao walitoka maeneo mbalimbali ikiwamo vyuo vikuu, wajumbe wa halmashauri kuu kutoka bara na visiwani, wawakilishi wa wamachinga na wavuvi.
Alisema Watanzania wanatamani kuwa na rais ambaye atasimamia kwa dhati umoja na mshikamano wa kitaifa, Muungano, kulinda amani, kukemea kwa nguvu zote ubaguzi wa dini, kabila, rangi na aina nyingine yoyote ya ubaguzi inayoweza kujitokeza nchini na kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.
“Historia ya nchi yetu ni ndefu na imepita misukosuko mingi lakini kwa umoja, udugu na mshikamano wetu tumefanikiwa,” alisema.
Hata hivyo alisema hivi sasa rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili ni maadui wengine walioongezeka kwa kasi.
“Kadri Watanzania tunavyozidi kuongezeka kwa idadi na maadui zetu hawa nao wanazidi kujitanua. Hivyo mbinu, mikakati na silaha za kupambana na maadui hawa lazima zibadilike,” alisema.
Ngeleja alisema baada ya kushauriwa na baadhi ya Watanzania kutoka pande zote za nchi tena wa kada mbalimbali amejitafakari, kujitathmini na kujiridhisha kuwa anayo dhamira ya kweli kuwatumikia Watanzania.
“Nimejitafakari, nimejitathmini na kujiridhisha kwamba ninayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kupitia nafasi ya urais. Mbali ya dhamira ya kweli nimejipima kwamba ninao uwezo wa kubeba matarajio ya Watanzania, kupitia utekelezaji wa kaulimbiu yangu isemayo: “Maono Sahihi, Mikakati Thabiti, Matokeo Halisi (MMM),” alisema.
Alisema mwaka huu siyo wa siasa za kawaida kama ilivyozoeleka, utakuwa wa kutathmini hatma ya Taifa, kujitazama na kujiuliza, malengo na dira na juhudi za kila Mtanzania mmojammoja na kwamba, rais ajaye lazima atoe matokeo halisi dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Azungumzia kujiuzulu, escrow
Akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari, Ngeleja alisema hakufukuzwa uwaziri kwa sababu ya kashfa, bali ni mabadiliko ya kawaida na kwamba, ambaye ana ushahidi kuwa alifukuzwa kwa kashfa anampa nafasi kuuwasilisha.
“Sikuondolewa kwa kashfa, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) hajanitaja hata kwa herufi moja. Mwenye taarifa sahihi ajitokeze kesho na ushahidi anipinge kwamba niliondolewa kwa kashfa,” alisema Ngeleja na kuongeza:
“Mara kadhaa imekuwa ikisemwa kumbukumbu zipo kwa sababu mamlaka zipo, mabadiliko yaliyofanyika Novemba 4, 2012 yalikuwa ya kawaida, sikuwa, hata sasa siwezi na haitakuwa kuondolewa kwenye nafasi ya uwaziri kwa kashfa.”
Kuhusu kashfa ya Escrow iliyosababisha kuvuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Ngeleja alisema hawezi kuzungumza zaidi ya yale aliyozungumza Rais Jakaya Kikwete Desemba 22 mwaka jana.
“Mimi bado ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Wilaya ya Sengerema…naamini Watanzania watanipima kwa yale niliyofanya, naamini ninafaa kuliko wenzangu kwa mazingira ya sasa,” alisema.
Kasi ya maendeleo
Ngeleja alisema Watanzania wanatambua wazi kwamba aina ya uongozi watakaoweka madarakani ndiyo utakaotafsiri aina na kasi ya maendeleo wanayotaka kati ya sasa na mwaka 2025, hivyo ni fursa nyingine ya kumchagua rais mzalendo na mchapakazi, anayekerwa na umaskini wa wenzake wengi.
“Maendeleo ya kweli ya nchi yetu hayawezi kuletwa na sekta ya umma peke yake, bali yataletwa kwa kushirikisha kikamilifu sekta binafsi, ni muhimu rais wa awamu ya tano awe na weledi wa kutosha kuhusu utendaji wa sekta ya umma na binafsi,” alisema.
Pia, alisema atasimamia vizuri rasilimali za Taifa zilizopo sasa kwa manufaa ya Watanzania wote na kuzikabili changamoto za sasa na zijazo na kwamba, matarajio ya Watanzania ni kumpata rais mwenye hofu ya Mungu ambaye hataongoza nchi kwa jazba, mihemko wala visasi.
Umaskini
Alisema sehemu kubwa ya Watanzania ni watoto wa wakulima, wafugaji wa ng’ombe na wavuvi na kwamba kihistoria, wazazi wa vijana wengi hawakubahatika kusoma, hivyo wamekulia na kuuishi umaskini.
Ngeleja alisema kutokana na ukweli huo, Watanzania wengi wanajua madhila ya umaskini vizuri na kuongeza kuwa, dhamira ya kupambana nao ni sehemu ya maisha yao.
“Hata kwa upande wangu, ujasiri wa kujitosa katika kinyang’anyiro hiki unatokana na dhamira ya kweli ya kupambana na umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili kwa nchi yetu,” alisema Ngeleja na kuongeza:
“Shauku yangu ya kupata mafanikio ni kubwa kuliko hofu yangu ya kushindwa. Hii inatokana na ukweli kwamba shauku yangu hii ni dhamira ya dhati kuwakomboa wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo, wajasiriamali ambao ndiyo kundi kubwa la Watanzania linalokabiliwa na umaskini. Ukubwa wa kundi hili unaifanya shauku yangu ya kufanikiwa, kuwa kubwa zaidi kuliko hofu ya kushindwa.”
Alisema atakuwa na jibu la swali la msingi kwamba kwa nini wakati takwimu zinaonyesha uchumi unakuwa kwa wastani wa asilimia saba takriban kwa muongo mzima mfululizo, umaskini unapungua kwa wastani wa asilimia mbili kwa mwaka.
Keki ya Taifa
Ngeleja alisema atasimamia ugawanaji wa pato la Taifa na kwamba mikoa mingine inachangia zaidi lakini ipo nyuma kwa maendeleo, kwa sababu ya kutokuwapo kwa mgawanyo sawa wa keki hiyo.
Alisema licha ya uchumi kukua: “Takwimu za makazi zinaonyesha takriban asilimia 70 ya Watanzania bado wanaishi nyumba za tembe, wanaoishi katika nyumba bora ni asilimia 30 tu ya zaidi ya milioni 45,” alisema.
Aliahidi kuboresha huduma za jamii, elimu, afya, maji haraka iwezekanavyo, ndani ya muda mfupi ujao na kwamba ana mikakati thabiti na bora ya kurekebisha kasoro zinazohusu mikopo ya wanafunzi vyuoni na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Jeuri yake
Ngeleja alisema akigeuka nyuma na kuangalia alikotoka kutokana na utendaji wake kuhusu ya mambo aliyosimamia na kuyatekeleza alipokuwa Wizara ya Nishati na Madini (Januari 2007 – Mei 2012), anamejipima na kuridhika kwamba anatosha.
“Tuliasisi mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara – Dar es Salaam mwaka 2009, utekelezaji wake ukaanza 2011 na utakapokamilika baadaye mwaka huu utaliwezesha Taifa kuokoa zaidi ya Sh1.6 trilioni zinazotumika sasa kugharamia mitambo ya kufua umeme kwa kila mwaka. Mradi huu ni mwarobaini wa kero ya mgawo wa umeme nchini,” alisema.
Alisema walianzisha mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) nchi nzima kuanzia mwaka 2009, baada ya kutengewa Sh27 bilioni lakini kutokana na mafanikio waliyopata, bajeti ya mwaka 2010/11 iliongezeka hadi Sh137 bilioni.
“Tulibuni na kuanza kutekeleza miradi mingi ya kuzalisha umeme iliyopo Kinyerezi – Dar es Salaam, Somanga Fungu (Kilwa), Mchuchuma-Liganga (MW 600), Nyakato, Mwanza (MW 60), lengo likiwa ni kufikia uzalishaji wa umeme wa MW 3,000 ifikapo mwaka 2015/16,” alisema.
Pia, alisema walibuni mradi wa kuunganisha mikoa yote kwenye Gridi ya Taifa kupitia miradi ya North-West Grid (kutokea Shinyanga, Geita, Kigoma, Katavi, Rukwa hadi Mbeya), Makambako- Songea na kuimarisha huduma ya umeme kupitia North-East Grid (kutokea Dar hadi Kilimanjaro).
Alisema walianzisha kupitia Rea, utaratibu wa kuwaunganishia wananchi umeme kwa gharama nafuu na hivi sasa wanaunganishwa kwa Sh27,000.
“Tulisimamia ufungaji majenereta mapya ya kufua umeme maeneo ambayo hayakuwa yameunganishwa kwenye Gridi ya Taifa… mwaka 2008 nilisimamia utungwaji wa sheria mpya ya umeme iliyoondoa ukiritimba wa Tanesco kuhusu shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji nchini,” alisema.
Alisema mwaka 2008 alisimamia kutungwa kwa sheria mpya ya mafuta iliyoweka pamoja na mambo mengine, utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja.
Pia, alisema mwaka 2009, walitunga sera mpya ya madini, ambayo ilisababisha kutungwa Sheria ya Madini mwaka 2010 na baadhi ya manufaa yake ni sharti la Serikali kumiliki kwa niaba ya wananchi, hisa za bure katika migodi.
Vipaumbele vyake
Ngeleja alisema ili afanikiwe, lazima awe na vipaumbele vichache ambavyo aliviainisha kuwa ni uchumi imara, utawala bora, huduma za jamii na miundombinu.
Alisema akipewa ridhaa ya kuongoza nchi kipaumbele namba moja kitakuwa ni ujenzi wa uchumi imara akisema tangu nchi ipate uhuru bado kuna changamoto kubwa ya kuwa tegemezi.
“Nchi yetu imeendelea kuwa soko (dampo) la bidhaa zinazotengenezwa na nchi nyingine. Mwisho wa siku tunauza nje ajira ambazo Watanzania wangeajiriwa. Nikiteuliwa na baadaye kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ijayo, kazi kubwa ya kwanza itakuwa ni kurekebisha hali hii,” alisema.
Kuhusu ardhi, alisema atahakikisha ardhi ya wakulima na wafugaji imepimwa na hatimiliki kutolewa kwa wananchi na kuahidi wakulima watapatiwa mikopo yenye masharti nafuu na bima kwa mazao yao.
Habari hii imeandikwa na Midraj Ibrahim na Raymond Kaminyoge
Mwananchi
No comments:
Post a Comment