Mwanachama wa Maskani ya Nia njema Fujoni akiwasilisha changamoto ya Vijana wa Maskani hao ya ubovu wa uwanja wao wa michezo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi aliyekaa kutoka mwanzo kulia.
Balozi Seif akisisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kupenda michezo ili kuimarisha afya zao na kujijengea mazingira ya ajira katika sekta hiyo ya michezo.
Baadhi ya wanachama wa maskani ya Nia njema ya Fujoni Kilimani wakifuatilia hotuba ya Mbunge wao Balozi Seif hayupo pichani wakati akibadilishana mawazo na kutafuta mbinu za kutatua changamoto zinazowakabili.
Balozi Seif akitembelea na kukaguwa uwanja wa michezo wa Timu ya Soka la Fujoni Boys { Maarufu Huibary } ambao una matatizo ya mawe makubwa.
Kulia ya Balozi Seif ni Afisa Tawala wa Wilaya ya Kaskzini “ B “ Ndugu Juma Abdulla Hamad.
Kepteni wa Timu ya Soka ya Fujoni Bays Kingwaba Salum akimpatia maelezo Balozi Seif hatua waliyofikia na kukwama katika kuufanyia matengenezo uwanja wao wa michezo.
Picha na –OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Uongozi wa Jimbo hilo una mtazamo wa kuangalia uimarishaji wa michezo mengine badala ya ule uliozoeleka wa soka ili kuwapa fursa zaidi vijana kuendelea kupenda michezo hapa Nchini.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuwaepusha vijana walio wengi kuondokana na vitendo vinavyoweza kuashiria kujiingiza katika vitendo viovu na hatimae kuzikanya mila,silka na Tamaduni zao.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Vijana wa Maskani ya Nia Njema iliyopo Kilimani Fujoni katika Jimbo la Kitope ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Sera ya Chama cha Mapinduzi imetilia Mkazo suala la kuendeleza Sekta ya michezo kwa lengo la kuimarisha afya za Wananchi sambamba na kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana.
Balozi Seif alieleza kwamba wachezaji wengi wa zile Timu maarufu za ulaya wametokea katika Nchi za Bara la Afrika ambazo ziliamua kutilia mkazo michezo katika kuwaimarisha vijana wao katika soko la ajira.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope amewaeleza Vijana hao wa Fujoni kwamba wakiamua kuimarisha mazoezi na kudumisha nidhamu uko uwezekano siku moja wa kuibua Drogba wa Zanzibar.
Akipata fursa ya kuutembelea uwanja wa Vijana hao wenye timu ya Soka ya Fujoni Boys { Maarufu Huibary } kwa kujionea changamoto zinazoukabili uwanja huo Balozi Seif aliahidi kutafuta mbinu za kuwatatulia changamoto hizo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mbinu hizo ni pamoja na kutafuta vitendea kazi vitakavyokidhi mahitaji ya kufanya matengenezo pamoja na kutia udongo uwanja huo uliosheheni mawe makubwa.
Naye Kepteni wa Fujonbi Boys Kingwaba Salum alimueleza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif kwamba Uongozi pamoja na Wanachama wa Timu hiyo wamejitahidi kupunguza mawe kwa kutumia kijiko na kufanikiwa kupata robo ya sehemu ya uwanja huo.
Kingwaba Salum alisema sehemu hiyo ndogo ambayo waliitia udongo ndio wanayoendelea kufanyia mazoezi jambo ambalo halikidhi kwa mujibu wa sheria 17 za mchezo wa Soka Duniani.
Mapema akitoa Taarifa fupi ya Vijana hao wa maskani ya Nia njema Fujoni Kilimani Mmoja wa wanachama hao Khadija Suleiman Yussuf alisema tatizo kubwa linalowakabili vijana hao ni ubovu wa uwanja wao wa kuendeleza michezo.
Khadija alisema tatizo hilo linaweza kutoa mwanya kwa baadhi ya vijana hao kuanza kujiingiza katika vitendo vilivyo nje ya maadili kwa kukosa sehemu za kufanyia mazoezi.
No comments:
Post a Comment