Donald Ngoma akitumikia timu yake ya zamani, Platnum FC ya Zimbabwe
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma kesho anatarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda.
Ngoma aliyetua nchini tangu mwanzoni mwa wiki ni miongoni mwa usajili mpya uliofanywa na Yanga kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kitakachoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame, klabu bingwa Afrika na Ligi Kuu msimu ujao.
Mbali ya Ngoma. nyota wengine wapya watakaotamulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ni Geoffrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Malimi Busungu, Benedicto Tinoco na kiungo aliye kwenye majaribio, Lansana Kamara.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alithibitisha jana kuwa wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga watakuwepo uwanjani kesho akiwamo Ngoma, hivyo mashabiki wa klabu hiyo wajitokeze kwa wingi kuziona silaha zao kwa ajili ya msimu ujao.
“Hili ni pambano ambalo kocha na benchi lake la ufundi watalitumia ili kuitazama timu na kuona ni iwapo timu inatakiwa kurekebishwa kabla ya kuanza msimu ujao wa ligi, hivyo tunatarajia kuwatumia wachezaji wetu wote ikiwamo Ngoma,” alisema Tiboroha.
Ngoma aliyetokea Platinum ya Zimbabwe ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kikubwa kwenye pambano ambalo Yanga walikutana na timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezaji huyo amesajiliwa baada baadhi ya mastaa wa Yanga kuomba uongozi na benchi lao la ufundi kuhakikisha wanamsajili baada ya kukoshwa na kiwango kikubwa alichoonyesha dhidi yao.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye atakuwa mgeni rasmi kwenye pambano hilo kesho.
Mratibu wa mechi hiyo, Mosi Magere alisema kuwa Pinda ameridhia maombi ya kushiriki kwenye mechi hiyo itakayokuwa pia na burudani kutoka kundi la Yamoto Band.
Wakati huohuo, Yanga imepanga kukamilisha usajili wake kwa kunasa beki wa pembeni na beki wa kati kutoka nje ya nchi na muda wowote watatua nchini.
Habari ambazo gazeti hili imepata zinaeleza kuwa kocha Hans Pluijm anataka kuongeza nguvu upande wa beki ya pembeni, hasa ya kulia anakocheza Juma Abdul na Mbuyu Twite na upande wa beki ya kati wanakocheza Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Kiongozi mmoja wa juu wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa wanataka kujipanga, hasa kimataifa na ndiyo maana wanataka kujiimarisha katika maeneo hayo.
Alisema wanatafuta beki wa kati mahiri na wa pembeni na wote wanaweza kutoka Ghana au nchi nyingine zikiwamo za Afrika Mashariki.
Mpango huo wa kusajili wachezaji kwenye nafasi hizo unatokana na wasiwasi uliopo kuhusu uimara wa wachezaji kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Inaelezwa kuwa kiwango cha msimu uliopita cha Cannavaro kimewatia shaka viongozi kwani amekuwa akipata maumivu ya mara kwa mara ya goti na kifundo cha mguu ambayo yamemwandama hasi sasa wakati Yondani wakati mwingine anachoka.
“Pia, tunataka kuimarisha nafasi ya beki ya pembeni, hasa kulia anakocheza Juma Abdul kwani pamoja na Twite kucheza pia nafasi hiyo, tunatakiwa kujiimarisha kwani mchezaji huyo naye amekuwa na majeraha ya mara kwa mara tangu msimu uliopita,”alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa wakati wakifanya jitihada za kuwapata wachezaji hao wanaendelea na mchakato wa kuwatafutia timu Andre Coutinho na Kpah Sherman ili nafasi yao ijazwe na mchezaji mmoja wa nje.
Hadi sasa Yanga ina wachezaji watano wa kigeni, Twite, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Sherman na Coutinho.
Hata hivyo, Pluijm alisema wachezaji wawili wa Ghana wanatarajiwa kutua wakati wowote kujiunga na kikosi hicho, lakini aligoma nafasi zao.
“Kuna wachezaji Waghana watakuja na ndiyo nilitaka kuja nao mwanzo, lakini ikashindikana, nasubiri viongozi watakavyoamua ingawa siwezi kusema wanacheza nafasi gani, wakifika mtawaona,” alisema Pluijm.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment