Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, (Taifa Stars) kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro kimeendelea kujifua katika uwanja wa Benki ya Biashara ya Ethiopia eneo la CMC asubuhi na jioni katika uwanja wa Taifa wa Addis Ababa.
Stars ambayo imeweka kambi jijini Addis Ababa imekua ikijifua mara mbili kwa siku, kuhakikisha wachezaji wanakua vizuri kuelekea katika mchezo dhidi ya timu ya Taifa Misri mwishoni mwa wiki hii jijini Alexandria.
Hali ya kambi kiujumla ni nzuri, wachezaji wote ni wazima, wakiwa wenye ari, na morali ya hali ya juu katika maandalizi ya mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2017.
Kocha mkuu wa Taifa Stars mholanzi, Mart Nooij amekuwa akiwafundisha vijana wake mbinu mbali mbali kuelekea kwenye mechi dhidi ya Misri, kuanzia sehemu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji kuhakikisha wanakua fit katika mchezo unaowakabili.
Ikiwa ni siku ya nne tangu Taifa Stars kuanza mazoezi yake jijini Addis Ababa, kocha Nooij amesema anashukuru vijana wake wanamuelewa vizuri anachowaelekeza, sasa timu inacheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, vijana wamechangamka na morali ni ya hali ya juu kambini kuelekea kwenye mchezo unaowakabili.
Hali ya nidhamu kambini ni ya hali ya juu, wachezaji waanatambua umuhimu wa mchezo huo, na kikubwa wameahidi kupambana kusaka matokeo mazuri katika mchezo dhidi ya Misri.
“Katika mpira hakuna kinachoshindikana, sie tumejiandaa vizuri, naamini tutakapofika Misri tutafanya vizuri na kuwapa furaha watanzania, kikubwa watuombee kwa mwenyezi mungu, tuwe wazima mpaka siku ya mchezo, naamini tutafanya vizuri” alisema Nadri.
Stars inatarajiwa kuelekea jijini Cairo siku ya ijumaa, kisha kuunganisha katika jiji la Alexandria tayari kwa mchezo dhidi ya Misri utakaochezwa katika uwanja wa Boeg El Arab siku ya jumapili Juni 14, 2015.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment