ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 6, 2015

BALOZI SEIF ATANGAZA NIA YA KUWANIA UWAKILISHI KUPITIA JIMBO JIPYA LA MAHONDA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Wajumbe wa Kamati za siasa za Mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini B Jimbo la zamani la Kitope na Kamati tekelezaji za UWT na Vijana ambao alifanya kazi nao pamoja katika kipindi cha miaka 10 akiwa Mbunge wa Jimbo la zamani la Kitope.Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Hilika Ibrahim Khamis na kushoto ya Balozi Seif ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa huo Kanal Mstaafu Juma kassim Tindwa.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati za siasa za Mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini B Jimbo la zamani la Kitope na Kamati tekelezaji za UWT na Vijana hapo ukumbi wa CCM Kinduni.

Balozi Seif pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskzini Unguja kushoto yake Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa Na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini B Nd. Hilika Ibrahim wakiangalia karatasi yenye mabadiliko ya mkato wa majimbo Zanzibar.

Balozi Seif akibadilishana mawazo na baadhi ya wajumbe wa Kamati za siasa za Mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini B Jimbo la zamani la Kitope na Kamati tekelezaji za UWT na Vijana mara baada ya kikao chao cha kuagana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiteta na Sheha wa Shehia ya Fujoni Wilaya yaKaskazini “B “ Bwana Said Mgeni Bakari nje ya ukumbi wa Ofisi ya Jimbo la zamani la Kitope Kinduni.
Baadhi ya Wana CCM wa Jimbo la zamani la Kitope wakipigwa butwaa kutokana na uwamuzi wa Balozi Seif kuwamua kutangaza nia ya kugombea Uwakilishi Jimbo Jipya la Mahonda. Picha na – OMPR – ZNZ.

Hatimae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametangaza rasmi nia ya kutaka kugombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Jimbo Jipya la Mahonda ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mahonda ni moja ya Jimbo jipya miongoni mwa Majimbo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { NEC } kutokana na mabadiliko ya ongezeko la idadi ya watu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita pamoja na uhakiki wa mipaka katika Wilaya na Majimbo mbali mbali hapa Zanzibar.

Nia hiyo ameitangaza wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini “B”, Jimbo la Kitope pamoja na Kamati Tekelezaji za Jumuiya ya Vijana, Wazee na UWT ambao alifanya nao kazi kwa karibu Kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa iliyokuwa Ofisi ya Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”.

Mjadala mzito wa Viongozi hao ulionyesha kuridhika na utendaji wa Balozi Seif uliopelekea kuzaa mawazo mawili yaliyopingana ya kumtaka agombee katika Majimbo mawili tofauti ya Mahonda na Kiwengwa kwa nafasi moja ya uwakilishi.

Akitoa uwamuzi wake baada ya mjadala huo mzito Balozi Seif alisema amemua kugombea nafasi hiyo ya Uwakilishi katika Jimbo jipya la Mahonda kwa vile kwa mujibu wa mkato wa majimbo Jimbo jengine jipya la Kiwengwa upo uwakilishi wa nafasi hiyo unaotokana na jimbo la zamani la Kitope.

Balozi Seif aliwaeleza Viongozi hao kwamba endapo CCM itampitisha kugombea nafasi hiyo na hatimae kufanikiwa kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda ana mtazamo wa kuhuisha uimarishaji wa Maabara za Skuli za Sekondari zilizomo ndani ya Jimbo hilo.

Mapema Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa huo Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa amewaasa wana CCM kuendelea kujenga tabia ya nidhamu katika kugombea nafasi za uongozi wa ngazi mbali mbali.

Kanal Mstaafu Tindwa alisema wapo baadhi ya wanachama wa chama hicho wanashindwa kuheshimu viongozi wao waliyoonyesha jitihada kubwa za kuwatumikia Wananchi ambapo wanastahiki tena kuendelea kuzitumia nafasi hizo katika vipindi vyengine.

Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshatumia jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tisa { 900,000,000/- } ndani ya Jimbo la zamani la Kitope katika kipindi cha miaka kumi iliyopita mbali ya shilingi Milioni 130,000,000/- alizopewa kwa ajili ya mfuko wa jimbo.

Fedha hizo alizielekeza zaidi katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo na ustawi wa Jamii ikiwemo zaidi sekta ya elimu na ujasiri amali ndani ya Jimbo hilo la zamani la Kitope.

Jimbo Jipya la Mahonda limejumuisha shehia Tisa ambazo ni pamoja na Matetema, Kitope Mangapwani, Fujoni, Mkadini, Kiomba Mvua, Kinduni na Mahonda yenyewe.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments: