Dar es Salaam. Baada ya makada kumaliza kurejesha fomu za kuomba kugombea urais kwa tiketi ya CCM jana, macho sasa yanaelekezwa kwenye vikao vya juu vya chama hicho vitakavyotoa majina yasiyozidi matano yatakayokwenda kupigiwa kura na Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 11 na 12.
CCM imeshatangaza kuwa itatumia vigezo 13 ilivyojiwekea kuwachambua wagombea 41 waliochukua na kurejesha fomu ili kupata majina ya wachache watakaopigiwa kura na mkutano huo mkuu, lakini Kamati ya Wazee, ambayo itatoa ushauri utakaokuwa msingi wa uamuzi wa vikao vingine na Kamati Kuu, italazimika kuangalia sifa za ziada katika kuchuja watangazania hao.
Kamati ya Wazee, inayohusisha wenyeviti na makamu wao wa zamani wa CCM pamoja na marais wa zamani wa Zanzibar, imeripotiwa kuanza kazi ya uchambuzi na itawasilisha taarifa yake kwa Kamati Kuu itakayokutana Julai 9 na baadaye kupeleka mapendekezo yake kwenye Halmashauri Kuu, ambayo huandaa ajenda za Mkutano Mkuu.
Wakati vikao hivyo vikiandaliwa, uzoefu unaonyesha kuwa CCM huzingatia mambo mengi katika kufanya uchambuzi, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa mtu atakayeondoa makundi yaliyoundwa wakati wa kuelekea uteuzi wa mgombea urais wake, kuzingatia Muungano, jinsia, eneo la kijiografia, rekodi ya mtiania, mustakabali wa uongozi wa chama na kukubalika kwa kada, hasa katika kipindi hiki ambacho upinzani umeongezeka nguvu.
“Kuna katiba za aina mbili,” alisema mmoja wa makada ambaye aliomba jina lake lisitiriwe. “Katiba ya maandishi ambayo inatoa mwongozo wa kisheria wa namna ya kumpata Rais wa nchi, lakini pia kuna katiba ya kimtazamo ambayo si rasmi, bali ni fikra za watu wanapozungumzia aina ya rais wanayemfikiria.
“Mfano, kama kuna eneo fulani halijawahi kutoa kiongozi wa nchi, kipindi hiki sasa ni chao.”
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi uliojumuisha mahojiano na baadhi ya makada wenye uzoefu na mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM, mgombea wa chama hicho tawala anaweza kutoka katika makundi manne ambayo gazeti hilo limeyaita kundi la kifo, kundi la mteule mbadala, kundi la vijana na wanawake.
Iwapo mteule hataweza kutoka kwenye kundi la kifo, ambalo linajumuisha makada wenye nafasi kubwa ya kupitishwa, chama hicho kinaweza kuamua kuchukua mwanachama ambaye atatoka kundi la wateule mbadala kwa lengo la kuzika makundi makubwa yaliyozuka wakati huu, au kuteua kada kijana iwapo CCM itakuwa inataka mwelekeo mpya, au mgombea mwanamke kama ilivyokuwa mwaka 2010 ilipoamua kuachana ghafla na Samuel Sitta na kumweka mbele Anne Makinda kuwa Spika wa Bunge, kwa maelezo kuwa umefika wakati wa wanawake.
Kundi la kifo
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, kundi la kifo linaweza kuwa na makada sita ambao ni Profesa Mark Mwandosya, Steven Wasira, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, Bernard Membe na Mizengo Pinda.
Katika kundi hilo, Mwandosya amekuwa hahusishwi na kashfa wala kuwa na migogoro na makada wengine. Aligombea kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete, aliyeshinda na Dk Salim Ahmed Salim.
Pamoja na kutokuwa na mivutano na watu, Profesa amekuwa hasikiki kutokana na kupewa kazi inayomweka mbali na wananchi.
“Kuendelea kuwamo ndani ya Serikali hadi sasa, katika macho ya wengi, ataonekana hana jipya,” alisema mchambuzi huyo akimzungumzia Profesa Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu).
Kundi hilo pia linamjumuisha Wasira ambaye uzoefu wake mkubwa ndani ya chama na Serikali unampa nafasi kubwa ya kupewa dhamana hiyo. Amekuwa akitumiwa na CCM kutetea utendaji wa Serikali na hivi sasa amepewa jukumu la kuongoza kamati inayoandaa Ilani ya Uchaguzi.
Ukweli ni kwamba anatoka Kanda ya Ziwa, ambayo kichama ni kubwa kwa maana ya idadi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu, jambo linalompa nafasi kubwa ya kushinda iwapo jina lake litakwenda kwenye chombo hicho cha mwisho cha uamuzi.
Lakini nafasi yake inakuwa finyu kutokana na wakosoaji kumwona kuwa amepoteza mvuto baada ya kufanya kazi kwenye Serikali za awamu zote nne bila ya kuwa na kitu kinachomtofautisha na wengine na hilo linaweza kuipa nguvu Kamati Kuu kumwengua.
Pia, wamo mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa ambao wote walishawahi kuingia bila mafanikio kwenye mbio za urais kwa tiketi ya CCM.
Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo katika Serikali ya Awamu ya Tatu, aligombea mwaka 2005 lakini jina lake lilikatwa. Ni mtu ambaye hana makundi kwenye chama, amepangua tuhuma dhidi yake na daima amekuwa akionyesha wazi chuki yake dhidi ya rushwa.
Baada ya mawaziri wakuu kugonga mwamba katika chaguzi zilizopita, safari hii Sumaye atakuwa akitegemea kuwa, kati ya watatu walio kwenye kinyang’anyiro hicho, atapitishwa.
Lakini uzoefu wake kwenye nafasi ya waziri mkuu kwa kipindi chote cha miaka 10 na chuki yake ya wazi dhidi ya rushwa, hakuwezi kuwa sifa pekee. Bado hajajiimarisha ipasavyo ndani ya chama, ambacho kwa kumteua mgombea urais, kitakuwa kimempata mwenyekiti wake wa miaka 10 ijayo.
Atalazimika kushinda ushawishi wa wapinzani wake waliowahi kushika nafasi hiyo, Lowassa na Pinda ili apitishwe na CCM.
Kamati Kuu itakuwa na kazi ngumu itakapokutana na jina la Lowassa, Mbunge wa Monduli ambaye alikuwa amekaa kimya kwa muda mrefu tangu alipojiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na sakata la Richmond, lakini amerejea kwa kishindo katika miaka miwili iliyopita.
Lowassa amejijenga ndani ya CCM na ameonyesha nguvu yake ya kuungwa mkono na wanachama na watu wengine walio nje na pia wakati alipotangaza nia na baadaye kuzunguka mikoani kusaka wadhamini.
Kauli ya Rais Kikwete kuwa CCM inataka mtu ambaye anaungwa mkono ndani na nje ya chama imeitia nguvu kambi yake na amekuwa akitumia kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya chama hicho kuongoza mabadiliko, akijinadi kuwa ndiye anayeweza kuongoza mabadiliko hayo.
Mtaji wake wa wanachama, wabunge, wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu ambao wamejitokeza bayana kuonyesha msimamo wao, ndiyo unaompa nafasi kubwa.
Msuguano wa maneno kati yake na Katibu wa Uenezi, Nape Nnauye unaweza kumpa nguvu ya kuituhumu Sekretarieti ya CCM kuwa inamfanyia njama, kama mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru alivyoeleza kwenye moja ya mikutano yake.
Hata hivyo, kundi lake limekuwa na msuguano na kundi la kada mwingine, Bernard Membe, hali iliyokifanya chama kuonekana kimegawanyika makundi mawili.
Pia, ingawa hakuna mtu anayeelekeza kwake tuhuma za moja kwa moja kuwa anahusika kwenye ufisadi zaidi ya Kamati ya Bunge iliyomtaka ajitathmini kuhusu kuhusika kwake kwenye sakata la Richmond, wapinzani wake wamekuwa wakitumia mitandao ya jamii kumhusisha na kashfa hiyo.Alilazimika kujibu tuhuma hizo siku ya kurudisha fomu alipotaka wanaomtuhumu wajitokeze.
Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pia anaingia kwenye kundi hili kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kujikubalisha ndani ya chama.
Tangu Benjamin Mkapa atoke kwenye wizara hiyo na kuwa Rais mwaka 1995 na kufuatiwa na Kikwete, wizara hiyo inaonekana kuwa ni bomba la kupitishia marais. Membe ameshikilia wizara hiyo kwa takriban miaka minane. Mbunge huyo wa Mtama amekuwa hahusishwi na mambo machafu na yanayokera wananchi.
“Huwezi kupitisha mtu ambaye ni kero kwa wananchi,” alisema mchambuzi mwingine kutoka ndani ya chama hicho.
Baada ya kuhusishwa kwenye mitandao ya kijamii na fedha kutoka Libya, Membe aliamua kutoa ufafanuzi wa fedha hizo zinazokadiriwa kuwa Sh40 bilioni, akisema hakuzichota na kwamba maelekezo ya matumizi ya fedha hizo yalitolewa na Mahakama.
Tatizo linalosumbua kwa mtiania huyo ni msuguano baina ya kambi yake na ile ya Lowassa, ambao unaonekana kukigawa chama. Ufinyu wa nafasi yake pia unatokana na kanda anayotoka kutokuwa na nguvu kubwa ndani ya chama.
Waziri Mkuu Pinda pia anaingia kwenye kundi hili kutokana na rekodi yake ya kustahimili kushikilia nafasi hiyo kwa miaka minane tangu ateuliwe mwaka 2008, kutokuwa na kashfa na pia kutokuwa na vitendo vinavyokera wananchi.
Pinda, ambaye anajinadi kama “mtoto wa mkulima”, aligeuza mwelekeo wa mbio za urais baada ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho na katika kipindi kifupi kuonekana amepata wafuasi wengi. Ni mwadilifu na ameonyesha nidhamu kwa chama wakati wote, hasa katika hotuba zake wakati wa kusaka wadhamini, akieleza kuwa ataanzia pale ambako Rais Kikwete ataishia.
Kundi la mteule mbadala
Kundi la pili linahusisha makada ambao wana nafasi ya kupitishwa na kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, ikiwa ni mpango mbadala wa kuzima makundi yaliyojitokeza kwenye mbio za urais, au kama Kamati Kuu itaridhika kuwa makada hao sita wa kundi la kwanza wamepoteza sifa kwa kuangalia vigezo tofauti.
Katika kundi hili, wapo Dk Mohamed Ghalib Bilal (ambaye ni Makamu wa Rais), Jaji Augustino Ramadhani, Balozi Amina Salum Ali, Makongoro Nyerere, Balozi Ali Karume, Dk John Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
Dk Magufuli, ambaye ameingia kwa mara ya kwanza kwenye mbio za urais, ndiye anayeweza kushangaza wengi iwapo atapitishwa na Kamati Kuu kwenda kupigiwa kura. Rekodi ya utendaji wake ni bayana na karibu mawaziri 10 waliochukua fomu wametumia ujenzi wa miundombinu ya usafiri kuwa ni mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne ambayo alihusika.
Dk Magufuli hana madoa ya ufisadi wala utendaji mbovu na daima amekuwa akionyesha unyenyekevu kwa Rais Kikwete kila alipozungumzia mafanikio ya wizara yake. Nguvu ya Kanda ya Ziwa ndani ya chama inamfanya awe na nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais iwapo jina lake litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu.
Ufinyu wa nafasi yake kuteuliwa ni pale Kamati Kuu itakapokata jina lake na kumweka mtu mwingine kutoka kanda yake.
Kundi hili pia lina jina jingine kubwa lililokuwa likizungumzwa sana kabla ya mbio za urais kuanza, Jaji Ramadhani. Mwanasheria huyo mkuu wa zamani ana sifa na fursa nyingi za kupenya kwenye mchujo. Moja ya sifa zake kuu ni uadilifu, lakini pia ana Uzanzibari na Ubara ndani yake unaomfanya aweze kukubalika na pande zote mbili, hasa Zanzibar ambayo pia ina nguvu kubwa katika kufikia uamuzi.
Jaji Ramadhan pia ni tiba ya tatizo la makundi yaliyopo kwenye mbio za urais. Lakini wakosoaji wameshaanza kuhoji uhai wa uanachama wake na muda aliokuwa ndani ya CCM kutokana na ukweli kuwa amekuwa mtumishi wa Serikali wa ngazi ya juu na hivyo hakutakiwa kujihusisha na siasa.
Anajitetea kuwa alihuisha uanachama wake miaka mitatu iliyopita baada ya kustaafu. Suala la uanachama linahusisha pia nafasi yake ya kuwa mwenyekiti wa CCM, nafasi inayokwenda sambamba na urais. Katika kundi hili pia yupo, Dk Bilal ambaye anaingia kwenye kinyang’anyiro akiwa na kete ya usafi, lakini pia Uzanzibari ambao kama utaibuka kwenye vikao hivyo, makamu huyo wa rais, anaweza kuwa na nafasi kubwa.
Changamoto kwake ni kukubalika kwake ndani ya chama kama ilivyojionyesha kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar ambayo inaonyesha, licha ya kukubalika kwenye vikao vya chama upande wa visiwani na kuongoza kwenye kura ya maoni alipogombea urais wa Zanzibar, alishindwa kuwashawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma na kufanya jina lake lishindwe na kuibuka la Amani Abeid Karume ambaye alikuwa mgombea wa CCM Zanzibar na alishinda urais.
Suala la wanawake pia linajitokeza kwenye kundi hili, ambalo wamo Dk Migiro na Balozi Amina. Wote wameliwakilisha Taifa kwenye Umoja wa Mataifa, lakini Dk Migiro ndiye aliyepata umaarufu zaidi baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chombo hicho na sasa ni mmoja wa mawaziri waandamizi.
Jina lake linaweza kupenya kwenye tano bora na hatimaye kupitishwa na CCM kuwania urais iwapo kundi la kwanza litaonekana halina mgombea mwenye sifa kwa kuangalia vigezo tofauti. Changamoto kwa waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje ni nguvu yake ndani ya chama na uwezo wa kustahimili mikiki mikiki iwapo atakuwa mwenyekiti.
Balozi Amina amefanya kazi kwa muda mrefu ubalozini na hivyo kupata uzoefu mkubwa wa uongozi akiwa mwanadiplomasia. Hana madoa ya uchafu wala kuwa kero kwa wananchi na nafasi yake ni pale tu suala la wanawake na Uzanzibari litakapochukua nafasi.
Vilevile, Balozi Karume anaingia kwenye kundi hili akiwa moja ya tiba za tatizo la makundi, lakini pia suala la Muungano linampa nafasi ya ziada.
Butiama ilikuwa imesahaulika hadi zilipoibuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Makongoro Nyerere anaandaliwa kumrithi Kikwete. Imani hiyo iliimarika baada ya mtoto huyo wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Nyerere, kujitokeza.
Alitumia nafasi ya kutangaza nia kuwachambua watiania wenzake, akiwataja baadhi kwa majina na udhaifu wao. Amefanya kazi kubwa ya kukumbusha wanasiasa umuhimu wa falsafa za Baba wa Taifa na anaonekana kuwa na nafasi ya kupitishwa iwapo ataingia tano bora, akiwa hana madoa zaidi ya kuhama chama mwaka 1995 na kujiunga na NCCR, nguvu ya Kanda ya Ziwa na ujasiri wa kukemea utovu wa nidhamu ndani ya CCM vinaweza kumbeba.
Kundi la Vijana
Kundi la vijana limeweka changamoto kubwa kwenye uchaguzi wa CCM mwaka huu, likiongozwa na makada kama January Makamba, William Ngeleja, Dk Mwele Malecela, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Mwigulu Nchemba na Lazaro Nyalandu na baadhi ambao si maarufu na wengine hawana sifa zinazotakiwa kikatiba.
Nchemba ndiye anaongoza kwa kupewa nafasi katika kundi hili la vijana na kuna uwezekano akaingia tano bora. Alijiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara ili ajikite kwenye mbio hizo za urais.
Kwa kutumia nafasi yake, ameweza kujijenga ndani ya CCM huku misimamo yake wakati wa sakata la escrow, Bunge la Katiba na udhibiti wa matumizi ya Serikali vikimpatia umaarufu ndani ya chama hicho.
Pia, yupo January Makamba ambaye amekuwa mwandishi wa hotuba wa Rais kabla ya kugombea ubunge wa Jimbo la Bumbuli na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Makamba ameeleza bayana kuwa CCM inahitaji fikra mpya na hivyo kutakiwa kuongozwa na kijana ambaye atafanya mageuzi. Lakini alianza kukosolewa mara tu alipotangaza nia, huku Rais Kikwete akieleza kushtushwa na taarifa hizo. Dk Kigwangalla ni kijana mwingine mwenye kuthubutu, lakini wachambuzi wanasema muda wake kuwa kiongozi wa nchi bado haujafika, anahitaji kupikwa kwanza. Vivyo hivyo, kwa mbunge Luhaga Mpina ambaye kiukweli bado hajafahamika miongoni mwa wajumbe wengi ndani ya CCM.
Kundi la mwisho ni la wengineo ambao wana rekodi tofauti, sifa na nafasi tofauti zinazoweza kuwavusha hadi tano bora.
Kundi la wengine
Hapa wapo wanawake, ambao pia wamejipenyeza kwenye makundi mengine kutokana na sifa tofauti, mawaziri wa zamani na wa sasa, watendaji waandamizi wa zamani wa Serikali, wabunge na wanachama wa kawaida.
Kundi la mawaziri linaongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ambaye alisifika alipoongoza Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond na baadaye kuteuliwa kuwa waziri.
Pia, yumo Profesa Sospeter Muhongo, ambaye utendaji wake kwenye Wizara ya Madini umeifanya CCM iutumie kujinadi hasa kutokana na mradi wa umeme vijijini. Doa kubwa ni katika sakata la escrow ambalo alituhumiwa kwa kushindwa kulisimamia vizuri na kusababisha Serikali ikose mapato.
“Profesa Muhongo ni ‘potential’, lakini chama kinataka ushindi. Katika mazingira kama yale ya escrow huwezi ukamweka mbele hata kama hana matatizo,” alisema mmoja wa makada wa CCM.
Wanawake wanaoingia kwenye kundi la wengineo ni Ritta Ngowi, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega.
UTILITY
Kundi la kifo
1. Profesa Mark Mwandosya
2. Stephen Wasira
3. Frederick Sumaye
4. Edward Lowassa
5. Bernard Membe
6. Mizengo Panda
Kundi mbadala
1. Dk Mohamed Gharib Bilal
2. Jaji Augustino Ramadhani
3. Balozi Amina Salum Ali
4. Dk John Magufuli
5. Dk Asha-Rose Migiro
6. Makongoro Nyerere
Kundi la Vijana
1. January Makamba
2. William Ngeleja
3. Dk Mwele Malecela
4. Luhaga Mpina
5. Mwigulu Nchemba
6. Lazaro Nyalandu
7. Dk Hamisi Kigwangalla
Kundi la wengineo
1. Profesa Sospter Muhongo
2. Dk Harrison Mwakyembe
3. Samuel Sitta
4. Dk Titus Kamani
5. Mathias Chikawe
Mwananchi
No comments:
Post a Comment