Wednesday, August 19, 2015

BALOZI SEIF AZINDUA MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA KWA WANANCHI WA SHEHIA YA JONGWE, JIMBO LA KIWANI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi mradi wa Maji safi na salama wa Wananchi wa Shehia ya Jongwe iliyomo ndani ya Jimbo la Kiwani, Wilaya ya Mkoni, Mkoa wa Kusini Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi akiutembelea mradi wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Wkilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni kuona harakati za maendeleo ya ujenzi wake unaofanywa na Kampuni ya Ruuns.
Mhandisi wa Ujenzi wa Kampuni ya Runs Bwana Mohammed Hamad aliyevaa nguo nyeupe akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikia ya ujenzi wa majengo ya Skuli ya Sekondari ya Wilaya ya Mkoani iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni.Nyuma ya Mhandisi Mohammed Hamad ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid.
Balozi Seif akizungumza na Walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah ya Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Madrasa hiyo na kujionea changamoto zinazowakabili.

Mwalimu Mkuu wa Madrasat Nur Minal Quran ya Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hatua waliyofikia ya ujenzi wa jengo lao ambapo wanahitaji kuungwa mkono na wadau wa elimu ya Dini. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mheshimiwa Mwanajuma Majid. Picha na – OMR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Wananchi wa Shehia ya Jongwe kwa uamuzi wao wa kujitafutia mbinu za kupambana na changamoto zinazowakabili katika Shehia yao hasa lile la 
huduma za maji safi na salama. 

Alisema uamuzi wao huo ndio uliopelekea washirika wa 
maendeleo,Viongozi pamoja na wahisani kuamua kuwaunga mkono katika kukabiliana na tatizo la huduma za maji safi na salama baada ya kuona juhudi walizozionyesha. 

Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati akiuzindua rasmi mradi wa Maji safi na salama wa Wananchi wa Shehia ya Jongwe iliyomo ndani ya Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoni Mkoa wa Kusini Pemba. 

Alisema Serikali inaelewa changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi katika maeneo yao tofauti Nchini na ndio maana ikatoa kipaumbele katika kuwasaidia nguvu za uwezeshaji na hata taaluma katika kupambana nazo. 
 


Balozi Seif aliwashauri Wananchi wa Shehia ya Jongwe kuhakikisha kwamba jukumu la kulinda mazingira yanayolizunguuka eneo la Kisima cha maji liko mikononi mwao. 

Alisema ipo tabia kwa wananchi walio wengi kuona tatizo na kuliachia bila ya kuchukuwa hatua yo yote na matokeo yake kulalamikia changamoto za tatizo hilo linalochukuwa muda mrefu kulipatia ufumbuzi. 

Akigusia suala la amani ya Nchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi hao wakiendelea kujiandaa na maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa Mwezi wa Oktoba mwaka huu waelewe kwamba suala la utulivu wa amani wanalisimamia kwa nguvu zao zote. 

Alitahadharisha kwamba Serikali itaendelea kulinda amani iliyopo na kamwe haitamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga hazina na lulu hiyo inayoringiwa naTanzania katika nyanja ya Kimataifa.




Balozi Seif alifahamisha kwamba hakuna Mtu mwenye akili timamu akajaribu kuwa na mawazo au kauli za kuitakia mabaya nchi yake ilhali na yeye anaendelea kuishi ndani ya nchi hiyo. 

Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Shehia ya Jongwe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alichangia shilingi Milioni 1,000,000/- na kuahidi i kukamilisha nyengine iliyobaki ili kulipa Deni la vifaa walivyokopa Wananchi hao katika kukamilisha mradi huo wa maji safi na salama. 

Akisoma Risala Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Shehia ya Jongwe Ndugu Mussa Juma alisema mradi wa maji safi na salama ulibuniwa mnamo Tarehe19 Machi mwaka 2014 kufuatia usumbufu mkubwa uliokuwa ukiwapata Wananchi hao wa kupata maji safi na salama. 

Ndugu Mussa alisema Wananchi hao walikuwa wakitumia maji yasiyo safi na kupelekea kukumbwa na maradhi ya miripuko yaliyosabisha madhara kwa wananchi walio wengi wa Kijiji hicho. 

Alisema juhudi za pamoja za Wananchi kupitia Kamati yao ya Maendeleo ndio iliyofanikisha mradi huo ulioungwa mkono na Viongozi mbali mbali,wahisani, mfuko wa Jimbo, Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }pamoja na shirika la Umeme Zanzibar {ZECO }. 

Naye Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu Hemed Salum alisema mradi mkubwa wa maji safi na salama katika ukanda huo ulibuniwa na kuanza rasmi mwaka 2006 baada ya mripuko wa maradhi ya matumbo katika Jimbo la Kiwani. 

Nd. Hemed alisema hatua za uchimbaji kisima zilianza mwaka 2007 kwa ufadhili ya Jumuiya ya Misaada ya Maendeleo ya Al – Yousuf Charitable Society ya Nchini Saudi Arabia na kufaidisha takriban Vijiji vya Mwambe na Shamiani. 

Afisa mdhamini huyo wa Wizara ya Ardhi, makazi, Maji na Nishati aliwahakikishia Wananchi hao wa Jongwe kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } itaandaa utaratibu maalum wa kukifanyia utafiti Kisima hicho ili kuelewa mienendo ya maji yake kwa vile kiko karibu na Bahari. 

Akijibu changamoto inayowakabili Wananchi hao ya kufungwa kwa Mashine ya Tukuza kwenye kisima hicho Nd. Hemed aliwaahidi Wananchi hao kwamba jukumu hilo litabebwa na Wizara hiyo ili kuwaondoshea usumbufu 
Wananchi hao wa kukatika katika kwa huduma za Umeme kwenye kisima hicho. 

Kisima hicho cha maji safi na salama kilichopo Jongwe Mwambe chenye uwezo wa kuzalisha Lita Tani Elfu 10,000 kwa saa moja kikiwa na mifereji 89 iliyosambazwa kuhudumia wananchi wa Vijiji vitatu vya Jongwe, Mwambe na Shamiani kimegharimu zaidi ya shilingi Milioni 44,755,000/-. 

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizitembelea Madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah na Madrasat Nur Minal Quran za Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani. 

Akizungumza na Walimu, Wazazi pamoja na Wanafunzi wa Madrasa hizo baada ya kuona changamoto zinazowakabili Balozi Seif alisema uamuzi wa wazee hao kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata elimu watoto wao ni jambo zuri na la msingi. 

Aliwatahadharisha walimu wa madrasa hizo kujiepusha na tabia ya baadhi ya walimu nchini wenye hulka ya kuwapotosha wanafunzi na kusahau wajibu wao wa kuwapatia watoto elimu ya dini kama ilivyoagizwa katika 
vitabu vya Muumba wa ulimwengu. 

Katika kuunga mkono jitihada za walimu na wazazi wa Kijiji hicho Balozi Seif alichangia shilingi Milioni 1,000,000/- kwa madrasat ahidu Fiiy - sabililah na kuahidi kusaidia shilingi Milioni 5,000,000/- kwa kila madrasa zote mbili katika kipindi kifupi kijacho. 

Hatua ya Balozi Seif pia ilimuhamasisha Mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa Kusini Pemba Mh. Faida Moh’d Bakari ambaye naye aliahidi kuchangia shilingi 2,000,000/- kwa madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah na shilingi Milioni 5,000,000/- kwa Madrasat Nur Minal Quran. 

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Wilaya ya Mkoani iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni. 

Ujenzi wa Skuli hiyo unaenda sambamba na ule wa Skuli ya Sekondari ya Wilaya ya Kusini Unguja iliyopo Kibuteni aliyoitembelea hivi karibuni ambazo zote zinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA }. 

Mhandisi Mkuu wa Ujenzi wa Skuli hiyo kutoka Kamuni ya Ujenzi ya Runs Bwana Mohammed Hamad alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni yake inatarajia kukabidhi Skuli hiyo mwishoni mwa Mwezi Disemba mwaka huu ili iwahi kuanza kuchukuwa wanafunzi mapema mwezi Januari mwaka 2016. 

Bwana Mohammed alisema wafanyakazi wa kampuni hiyo hivi sasa wanaendelea na hatua za mwisho za ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi, kupaka rangi madarasa pamoja na kukamilisha sehemu za michezo mbali mbali ndani ya eneo la skuli hiyo. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionyesha kuridhika kwake na ujenzi huo unaokwenda kwa kasi zaidi kuliko ule ya majengo ya Skuli ya Sekondari ya Kibuteni licha ya kuanza mwanzo kwa zaidi ya miezi mitatu nyuma ya Skuli ya Mkanyageni.

No comments: