Advertisements

Friday, August 21, 2015

Kaseja atua Mbeya, Ivo asaka timu nje

Kipa Juma Kaseja (kushoto) akikabidhiwa jezi na kiongozi wa Mbeya City. Katikati ni Tippo Athuman akishudia tukio hilo.

By Justa Musa, Oliver Albert
Dar/Mbeya. Wakati dirisha la usajili likifungwa jana usiku, kipa Juma Kaseja amesaini mkataba wa miezi sita wa kuichezea Mbeya City, huku mwenzake Ivo Mapunda akitangaza kusaka timu nje ya nchi.
Makipa hao wa zamani wa Taifa Stars, Kaseja na Ivo msimu uliopita hakuwa mzuri kwao kutokana na kuingia katika migogoro na klabu zao, Yanga na Simba.
Kaseja alikaa nje ya soka kwa muda mrefu kutokana na kuwa na mgogoro na klabu yake ya zamani Yanga uliohusisha masuala ya kimkataba.
Mgogoro huo ulipelekea Yanga kumpeleka Kaseja katika Makahama ya Kazi, Kitengo cha Usuluhishi hata hivyo bado kesi hiyo inaendelea, lakini haimzuii kipa huyo kujiunga na timu yoyote ili kuokoa kipaji chake.
Hata hivyo, juzi usiku Kaseja alisaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Mbeya City katika msimu huu wa Ligi Kuu unaotarajia kuanza Septemba 12.
Msemaji wa Mbeya City, Dismas Ten alisema kusajiliwa kwa kipa huyo ni kutokana na mapendekezo ya kocha Juma Mwambusi aliyeuambia uongozi wao kuhusu ubora wa kipa huyo.
‘’Ni kweli tumenasa kipa mwenye uzoefu wa hali ya juu nchini na amesaini miezi sita kwa ajili ya kuitumikia Mbeya City,’’ alisema.
Aliongeza kuwa Kaseja bado yupo Dar es salaam na muda wowote atatua jijini Mbeya kwa ajili ya kuungana na wachezaji wenzake kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu.
Alisema vipimo vyote vya kiafya kwa mchezaji huyo vimekamilika na kwamba japo Kaseja amesaini mkataba mfupi, lakini wana imani ataitoa Mbeya City kutoka hapa ilipo na kuifikisha katika hatua fulani.
Kocha Mwambusi alisema ameamua kumuweka Kaseja katika kikosi hicho kutokana na ubora wa kazi anayoonyesha akiwa langoni.
“Kaseja ni kipa aliyekuwa akimvutia wakati akiwa na timu mbalimbali ikiwamo Yanga aliyokuwa akitumikia misimu ya hivi karibuni na kwamba ubora huo sasa atauonyesha akiwa na Mbeya City.”
Wakati Kaseja akijikita Mbeya City, swahiba wake, Ivo Mapunda wa Simba alisema atarudisha fedha za usajili za klabu hiyo na kuendelea na jitihada zake za kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Mapunda aliyeidakia Simba kwa misimu miwili akitokea Gor Mahia ya Kenya aliingia katika utata wa usajili wake baada ya viongozi wake kudai anadengua kusaini mkataba huku yeye akipinga hilo na kudai kuwa hakuna kitu kama hicho.
Uongozi wa Simba ulidai kuwa umeamua kuachana na kipa huyo kwa madai ni msumbufu na hataki kusaini mkataba kwani kila walipomtaka kufanya hivyo alionekana kama hataki na wakati walishampa Sh 10 milioni ingawa Ivo alisema kuwa yupo kila siku na alikuwa anaumwa na viongozi wanajua sasa anashangaa kuambiwa hataki kusaini mkataba.
Kipa huyo aliliambia gazeti hili jana kuwa soka la Tanzania lina mizengwe na linahitaji uvumilivu mkubwa na yote yaliyotokea kwake anamwachia Mungu ana atarudisha fedha za usajili alizochukua.
Alisema malengo yake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ingawa hadi jana kama kuna timu iliyokuwa ikimuhitaji ilipewa ruksa ya kufanya naye mazungumzo kabla ya dirisha la usajili kufungwa jana usiku.
“Nitarudisha fedha zao za usajili, ingawa kwa sasa malengo yangu ni kucheza nje ya nchi, lakini sizizuii klabu za hapa zinazonihitaji kuzungumza na mimi ili kucheza kwa muda mfupi wakati naangalia mipango mingine ya kwenda nje.
Simba iliamua kuachana na Ivo baada ya kumsajili kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast , pia ilikuwa mbioni kumsajili kipa mwingine wa JKU ya Zanzibar, Abdulrahiman Mohammed, lakini inao makipa wengine chipukizi Manyika Peter jr na Dennis Richard.
Mwananchi

No comments: