Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Hati ya
umiliki wa eneo la Kilimo kwa Bwana Yuweni Kibwana Nzukwi Mmoja miongoni mwa wakulima wa Vijiji vya
Dole, Ndunduke na Kijichi baada ya
upatikanaji wa ufumbuzi wa mgogoro wa maeneo hayo.
Mkulima Ana Nyaka Buluju wa
Dole akikabidhiwa hati ya umiliki wa
eneo la kilimo kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo Skuli ya Wazazi Dole Wilaya ya
Magharibi “A".
Baadhi ya wakulima wa Vijiji vya Dole, Ndunduke na Kijichi
wakifuatilia zoezi la kukabidhiwa hati zao za umiliki wa maeneo ya kilimo
kwenye Vijiji vyao lililafanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi.
HATMA ya
Mgogoro wa maeneo ya Kilimo unaowahusisha Wakulima wa Vijiji vya Dole,
Ndunduke, Kijichi na Nguruweni dhidi ya baadhi ya watu wanaovamia maeneo hayo hivi sasa umeshafikia ukingoni
baada ya kurindima kwa takriban miaka 12.
Mgogoro huo
ulizuka kufuatia baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha pamoja na marafiki na
familia za maafisa wa taasisi za Kilimo kuvamia maeneo hayo wakati wakielewa
kwamba wakulima wa asili wa maeneo hayo walikuwa wakiyatumia kuendeleza
shughuli zao za kilimo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitekeleza Ahadi ya Serikali
aliyoitoa Tarehe 14 Disemba mwaka 2012 ya kuwamilikisha Wakulima hao alikabidhi
Hati za umiliki huo kwa Wakulima 145 wa Dole, Ndunduke na Kijichi hapo katika
maeneo ya skuli ya Wazazi Dole.
Wakulima hao
145 ni miongoni mwa wote Mia 222 wa Vijiji hivyo ambao walipata hati hizo baada
ya kuyatumia maeneo hayo ya Serikali yaliyokuwa chini ya Wizara ya Kilimo wanayolimwa
kwa kipindi kirefu cha maisha yao.
Akizungumza
na Wakulima na Wananchi wa Vijiji hivyo vya Dole, Ndunduke na Kijichi Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamuwa kufanya hivyo ili
kuwapa fursa ya umiliki wakulima hao waendeleze shughuli zao za Kilimo kwa
utulivu zaidi akiwatanabahisha kwamba maeneo waliyopewa ni kwa ajili ya kilimo.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wananchi na Wakulima wa Dole,
Ndunduke, Nguruweni na Kijichi kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouonyesha ambao
umeipa faraja Serikali na kufikia hatua njema na ya mafanikio.
Akitoa
Taarifa fupi katika mkutano huo wa
makabidhiano ya hati ya umiliki wa maeneo ya kilimo, Mwenyekkiti wa Wakulima wa
Dole, na Ndunduke Dr. Daudi Silas Mukaka alisema Serikali Kuu imeonyesha nia
thabiti ya kuwajali Wananchi wake.
Dr. Mukaka alisema
Wananchi pamoja na Wakulima wa Dole na Ndunduke wamefarajika sana kutokana na
kazi kubwa iliyochukuliwa na Serikali
Kuu chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa kushirikiana
na baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Kilimo na Ardhi katika kulipatia ufumbuzi
wa kudumu suala hilo la mgogoro wa maeneo ya kilimo.
Mapema Mkuu
wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdullah Mwinyi
alisema licha ya Wananchi wa Vijiji hivyo kuonyesha ishara ya hasira
lakini alifarajika kuona kwamba busara ilitawala katika kulishughulikia tatizo
hilo.
Mheshimiwa
Abdullah alisema Wananchi hao wanapaswa kuendelea kumpongeza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kutokana na Uongozi wake wa busara wa
kuweka ahadi na akawa makini kuitekeleza.
Migogoro ya
ardhi katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Zanzibar hivi sasa inaonekana
kuchukuwa sura mpya ya kuanza kuchukuliwa hatua za ufumbuzi kutokana na uamuzi
wake wa kusajili ardhi yote ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment