ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 7, 2015

Nuru the Light aachia video ya wimbo wake mpya ‘L’


Muimbaji wa Tanzania mwenye makazi yake nchini Sweden, Nuru The Light ameachia video ya wimbo wake mpya ‘L’. Nuru alifanya uzinduzi rasmi wa video hiyo Jumamosi hii kwenye kiota kipya cha starehe, Jozi Lounge kilichopo Msasani jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mastaa, marafiki zake wa karibu na mashabiki.

Video ya wimbo huo imefanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na muongozaji na mshindi wa tuzo kibao, Adam Juma aka AJ. Mandhari ya kuvutia ya fukwe za bahari ya Hindi yanaonekana vyema kwenye video hii na uzuri wa Nuru unaongeza kitu cha kuvutia machoni.

Nuru alikuwa kimya kwa takriban miaka miwili baada ya kuachia wimbo wake ‘Muhogo Andazi’ aliomshirikisha Bob Junior. Aliamua kuandika wimbo huo wa mapenzi na kuupa jina la ‘L’ kwa kuwa herufi hiyo inawakilisha vitu vingi chanya hasa kwenye uhusiano wa mapenzi.


‘L’ umetayarishwa nchini Sweden katika studio za Joevibes Productions na tangu uanze kuchezwa kwenye radio mbalimbali nchini umepokelewa vizuri na mashabiki na watangazaji wa radio hizo huku wakimtaka kueleza alipoipata idea hiyo ya kipekee.

“L inasimama badala ya maneno mengi chanya, inaweza kuwa Love, Light, Love, Life na mengine mengi, vilevile nilitaka kuonesha kuwa sio lazima wimbo uwe neno zima, ukiwa mbunifu zaidi hata herufi moja tu inaweza kusimamia wimbo mkubwa wenye maana kama huu,” anasema.

k “Pia nilitaka kuonesha kuwa kwa msanii ni muhimu muda mwingine kupumzika kidogo, ku-refocus, kurudi upya na kuwa na ile njaa kali ya kuandika nyimbo bora zaidi, kusimama jukwaani na kuwa mbunifu zaidi kwa sababu sometimes unachoka,” aliongeza.

Pamoja na Muhogo Andazi, Nuru aliwahi kutamba na nyimbo kama Walimwengu, Msela na Nisubiri Usilale.

No comments: