Sunday, November 1, 2015

CCM, Cuf Z`bar ngoma mbichi

Wakati Chama Cha Wananchi (Cuf), kikiitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) iendelee kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaunga mkono uamuzi wa kufutwa matokeo hayo.

Hali hiyo imejitokeza siku moja tu baada ya Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Cuf, Maalim Seif Hamad, kutangaza juzi kutokubaliana na maamuzi ya Tume hiyo na kuitaka kumtangaza mshindi.

Hatua ya kuunga mkono msimamo wa Zec, ilitolewa jana na Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

Vuai alikuwa ameambatana na wakala wa Mgombea Urais wa CCM, Balozi Mohammed Ramia, Ofisi Kuu ya chama hicho Kisiwandui, mjini hapa.

“CCM inapenda kutamka inapokea na kukubaliana na uamuzi wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Oktoba 28, mwaka huu,” alisema Vuai.

Katika mkutano huo pia alihudhuria aliyekuwa Spika wa Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, waziri wa zamani wa SMZ Asha Abdalla Juma, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Ramadhan Abdalla Shaabani, Naibu waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo na aliyekuwa Balozi wa Umoja wa Afrika, Amina Salum Ali.

Vuai alisema CCM imesikitishwa na vitendo vya uchafuzi wa uchaguzi ikiwamo mawakala kufukuzwa katika vituo wakiwamo wa CCM kunyimwa vitambulisho katika Wilaya ya Magharibi kisiwani Unguja.

Alisema uchaguzi huo ulitawaliwa na kasoro za kisheria ikiwamo kupatikana kwa kura bandia zisizopungua tano katika kituo kimoja cha wapiga kura huko Pemba.

WAJUMBE KUPIGANA
Alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe wa Zec kuvua mashati na kuanza kupigana kumeonesha walishindwa kutekeleza majukumu yao na wameifedhehesha Tume hiyo mbele ya Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa na wamejivua sifa ya kuwa wajumbe wa tume hiyo.

Naibu katibu mkuu huyo alisema kuwa hakuwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki huku baadhi ya matokeo ya wapiga kura yakionesha wengi kuliko idadi ya watu walioandikishwa katika daftari la kudumu kwa kila jimbo kisiwani humo.

YASHANGAA MAALIM KUTOCHUKULIWA HATUA
Aidha, alisema CCM imesikitishwa na hatua ya mgombea wa Cuf, Maalim Seif kutangaza matokeo ya uchaguzi huo kinyume na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 pamoja na kifungu cha 42 (5), kinachokataza mtu yeyote kutangaza matokeo ya urais kabla ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, imeweka adhabu ya Shilingi milioni tano au miaka mitano jela, lakini vyombo vya kusimamia sheria vimeshindwa kuchukuwa hatua licha ya uamuzi huo kuwa unaweza kuhatarisha umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.

“Kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi kabla ya kura hizo kufanyiwa uhakiki na Zec lengo lake lilikuwa ni kuanzisha mgogoro ambao tunauona hivi sasa, CCM tunashangaa hadi leo hii, hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya mgombea huyo,” alisema.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kudumisha amani na kuvitaka vyombo vya dola nchini kuimarisha ulinzi mjini na vijijini kuwadhibiti watu watakaojaribu kuchezea amani ya nchi au kuhujumu mali za umma visiwani humo.

Wakati huo huo, Chama cha Cuf kimesema kumeibuka wimbi la watu kukamatwa na kupigwa na vyombo vya ulinzi na usalama na kubambikiwa kesi tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi kisiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya Cuf, Mtendeni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Nassor Ahmed Mazrui, amesema watu wamekuwa wakivamiwa na kupigwa na kuharibiwa mali zao na askari wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Alisema vitendo kama hivyo vimefanyika katika kisiwa cha Tumbatu na kutaka vyombo vya ulinzi kusimamia majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuivusha Zanzibar katika hali ya amani wakati huu wa uchaguzi.

Alisema inasikitisha kuibuka kwa vitendo vya kulipuka mabomu ya kutegwa ya kienyeji katikati ya mji wa Zanzibar wakati serikali imetumia gharama kubwa ya kufunga kamera za kufuatilia uhalifu zenye uwezo wa kuona umbali wa kilomita moja.

Chama hicho kimesema kitaendele kusisitiza matokeo yaliyobakia yahakikiwe na mshindi atangazwe na viongozi wa CCM waondoe hofu kwani wataendelea kuwamo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vile ipo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ismaili Jusa Ladhu, alisema kuna juhudi za kidiplomasia zimeanza kufanyika katika kushughulikia tukio la Mwenyekiti wa Tume la kufuta matokeo ya uchaguzi kinyume na sheria na Katiba ya Zanzibar.

Hata hivyo, alisema Chama Cha Cuf kitaendelea kutoa taarifa kila hatua itakavyokuwa inaendelea kwa wafuasi na wanachama wake pamoja na kuwapo mpango wa kurejesha ajenda kwa wananchi ya kupinga kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu kama juhudi za kumaliza tatizo hilo halitafanikiwa kwa njia za kidiplomasia.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

5 comments:

  1. kwa hali hii inaonyesha kabisa nani alishinda,hongera Maalim Seif....wewe unasema kura zilizidi ulijuaje na matokeo hayajatangazwa?
    wasimamizi walipigana ni aibu kitaifa na kimataifa,wasimamizi wakimataifa wanasema ulikua mzuri tu....tatu hata Moshi wasimamizi walipigana mbona haukufutwa?na je huyo Jecha aliyekiri mapungufu mpaka uchaguzi kurudiwa yeye kwanin asijiuzulu...Amani ileeee

    ReplyDelete
  2. NGOMA ILIKUWA NZITO MARA HII EEE
    MNAWAONA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI WOTE WAPO MBELE YENU KUIBA KUKAWA SHUGHULI KUBWA EEE.
    SEIF HAJAJITANGAZIA ILA AMESEMA AMEPATA KURA NGAPI YEYE.
    MAANA MLIJIFANYA WAJUAJI NYINYI MAFISI-EMU MKAWA MNATANGAZA KIDOGO KIDOGO WAKATI KURA ZILIKWISHA KUHESABIWA ZOTE JIONI YA TAREHE 25 NA KUPEWA MAJIMBO YOTE UNGUJA NA PEMBA.
    NGOMA ILIVYOKUWA NZITO MKAANZA KUTANGAZA MAJIMBO YA UNGUJA KWANZA YALE AMBAYO CHENI KAPATA KURA NYINGI MKENDA MKENDA, MAJIMBO YA PEMBA KILA MKITAKA KUTANGAZA KIGUGUMIZI KIKAWAPATA MAANA CHENI HAJAPATA KITU
    KIGUGUMIZI KILIPOZIDI MKAONA HAMNA BUDI NI KUUFUTA UCHAGUZI.
    LOOO MNA ROHO GANI NYIE MAFISI-EMU
    HAMNA DINI
    HAMNA IMANI
    HAMNA UTU
    HAMNA HAMNA HAMNA TUU NYINGI TUU HAPA NITAJAZA PAPER.
    CCM KWISHAAA

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wahi Mirembe ukapate msaada wa matibabu!

      Delete
  3. kwani yupo mtu mwenye akili timamu ambaye hakuegemea kuyapata maneno kama hayo kutoka kwa vuai?yupo?ni nani.ccm mmeanguka na mtaondoka tuu.hebu tuulize hivi huyu shein kwa sasa yupo wapi?maana muda wake wa kuiongoza zanzibar umekwisha leo.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Na wewe wahi Mirembe ukapate msaada wa matibabu!

      Delete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake