Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,160, kuwapunguzia adhabu ya kifungo na kuwaachia huru wengine.
Kikwete alitoa msamaha huo jana kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Pombe Magufuli.
Dk Magufuli aliapishwa jana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya Kikwete kumaliza kipindi chake cha miaka 10, aliongoza awamu mbili, kila mmoja miaka mitano.
Sherehe za kumuapisha Dk Magufuli, zilifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe jana jijini Dar es Salaam, Kikwete amewaachia huru wafungwa 867 na kuwapunguzia vifungo gerezani 3,293.
Chikawe alisema Kikwete amesamehe wafungwa hao wenye magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu (TB), saratani na wazee kuanzia umri wa miaka 70 na watu wenye ulemavu wa viungo na akili.
Alisema pia amewasamehe wanawake wenye ujauzito, wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Waziri huyo alisema msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha, kupokea na kutoa rushwa.
Alisema wengine ni wale waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na silaha na risasi kinyume cha sheria.
Chikawe aliwataja wengine ambao hawatahusika na msamaha huo wa Kikwete kuwa ni wale waliofungwa kwa makosa ya kulawiti, kunajisi, kubaka na kuwapa mimba wanafunzi chini ya miaka 18.
Alisema pia wamo wezi wa magari, pikipiki au waliofungwa kwa kujaribu kutenda makosa hayo
Chikawe alisema wengine waliokosa msamaha huo ni wale waliofungwa kwa kutoroka chini ya ulinzi halali wakati wanatumikia kifungo gerezani, kufanya biashara haramu ya binadamu, nyara za Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma.
No comments:
Post a Comment