ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 19, 2015

'Taifa Stars ilikosa umakini, nidhamu'

Siku moja baada ya Taifa Stars kuweka rekodi ya kichapo cha mabao 7-0 katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia usiku wa kuamkia jana dhidi ya Algeria, wadau mbalimbali wa michezo wamemwaga hadharani sababu zilizoifanya timu hiyo kupotea kwenye mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja kwa dakika zote tisini.

Stars imetolewa baada kufungwa jumla ya mabao 9-2, ikiambulia sare mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.

Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kiwhelu alisema kipigo cha Stars kilitarajiwa kwa sababu haijafika kiwango cha kushindana na timu kubwa kama Algeria.

“Kwa upande wangu, timu bado inafanya vizuri sana...lakini kwa kiwango chetu kutegemea ushindi kutoka Algeria ni jambo gumu. Hata hivyo, tuwatie moyo wachezaji wetu badala ya kuwabeza,” alisema Julio.

Kocha wa zamani wa JKT Ruvu, Felix Minziro alisema timu ilikosa mipango, umakini na nidhamu ya mchezo.

"Kwenye soka unapokosa vitu muhimu kama hivyo, lazima upate madhara. Kwa kuangalia tu, wachezaji wetu hawakuwa makini," alisema Minziro.

Alisema kocha Boniface Mkwasa alikuwa na mipango mizuri ya ushindi, lakini ameangushwa na wachezaji waliokosa umakini.

“Algeria walikuwa na mipango madhubuti ndiyo maana walionekana kucheza mpira uliokuwa kwenye mpangilio na kulishambulia lango la Stars muda wote wa mchezo,” alisema.

Aidha, Kocha mkongwe Kennedy Mwaisabula alisema katika mchezo huo wachezaji walikosa nidhamu na kadi na kadi nyekundu waliyopewa haikushangaza.

Aliongeza kuwa, magoli waliyofungwa ni uzembe wa wachezaji kutokana na kutokuwa kwao makini na kuwaruhusu wenyeji kuucheza mpira walivyotaka.

“Algeria ni wazuri kila idara ndiyo maana waliweza kutawala mchezo, lakini pia hali hiyo ilichangiwa na ukosefu wa umakini wa wachezaji wa Stars,” alisema.

Aliongeza kuwa kipigo hicho ni funzo kwa mechi zingine za kimataifa, kwani tunatakiwa kutumia vizuri nafasi tunazopata.

Mkuregenzi wa bodi ya ligi wa TFF, Boniface Wambura alisema kimsingi kipigo walichokipata Stars ni kikubwa katika historia ya hivi karibuni lakini ni lazima wachezaji watiwe moyo na wasikatishwe tamaa.

"Mara ya mwisho nakumbuka kipigo kikubwa kilitoka kwa Misri cha magoli 6-0, bado tunapaswa kuisapoti timu yetu," alisema Wambura.

Alisema ni vizuri wachezaji kutambua umuhimu wa kucheza uwanja wa nyumbani na kutumia kila nafasi wanayoipata ndani ya uwanja.

Kwa upande wa nyota wa zamani wa timu ya Taifa Stars, Bakari Malima alisema Stars ilikosa mbinu za kuwakabilia wenyeji ndiyo maana wamefungwa idadi kubwa ya mabao.

"Kuna umuhimu kwa wachezaji wetu kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kwenye mashindano makubwa kama hayo kama walivyofanya Algeria," alisema Malima na kuongeza:
"Unapotumia vizuri uwanja wa nyumbani unapunguza presha kwenye mechi ya marudiano, lakini Stars ilishindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani pamoja na kupata nafasi nyingi za kufunga."

Katibu Mku wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya alisema kimsingi kipigo walichopata Stars kimewasikitisha hasa kutokana na kiwango kizuri walichokionyesha kwenye mchezo wa kwanza.

Lihaya alisema hakuna sababu ya kumlaumu Kocha wala wachezaji na kinachotakiwa timu ijipange upya.

Kaimu Mkurugenzi wa michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Alex Nkenyenge alisema Stars ilipaswa kujiandaa na kujipanga kikamilifu kabla ya kuwakabili Algeria.

Kikosi cha Stars kilitarajiwa kurejea nchini leo alfajiri wakitokea Algeria.

Imeandikwa na Faustine Feliciane, Renatha Msungu na Devotha Kiwhelu
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Wazungu wanasema " if you don't spend enough money today, you won't satisfy tomorrow"
Hivyo kwa mawazo yetu watanzania tunafikiri mkwasa ni kocha wa kiwango cha dunia?
Mambo yamebadilika sana duniani hasa katika masuala ya michezo wakati sisi tumebakia kule kule katika miaka ya sabini. Kocha wa timu ya Taifa sio mtu wa kudhania anaweza bali kunatakiwa kuwe na uthibitisho wa uwezo wa taaluma yake. Mkwasa anaweza kuwa kocha lakini sio wa timu ya Taifa kwani hata angekuwepo yule muholanzi waliemtimua taifa star isingefungwa 7:0.
Ukocha sio kufundisha mpira tu bali pia uwezo wa kumeneji timu nzima pamoja na akili za wachezaji na mipango ya ushindi, uwezo huo mkwasa hana hata robo yake kigezo kikubwa ni uzawa. Uzawa?
Inaonesha yakuwa kila wakati wa kuchaguliwa kocha wa timu ya taifa wa Tanzania anakuwa anatafutwa kocha wa majaribio. Kuna makocha wengi wazuri tu na wa viwango duniani tena Tanzania inaweza ikamudu harama zao bila ya shaka yeyote ile lakini linapokuja suala la Taifa au suala la taasisi ya Taifa inayotuwakilisha kimataifa Tanzania mara nyingi tunakosa umakini. Ukiangalia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania utagundua inawachezaji wakutufikisha mbali sana. Utagundua yakwamba wale wachezaji wanawalimu wazuri zaidi huko katika timu zao kuliko mwalimu wao wa timu ya Taifa. Kwa hakika kabisa bila ya kumungunya maneno mkwasa anakosa modern football expertise utakaomuwezesha kuiongoza timu ya Taifa kumbana na makocha wanaotoka katika nchi za dunia ya kwanza. Watu wanafanya mzaha sana kufungwa tena kwa aibu kwa timu ya Taifa na kwa kuwa ni mchezo unaopendwa sana Tanzania na watanzania wengi kuliko mchezo mwengine wowote basi tayari machungu hayo yamesha zalisha at least wagonjwa wapya million tano wa misongo ya mawazo. Fikiria mpenzi wako wa dhati anapokusaliti machungu yake yanakuwaje? Basi wataalam wanatuambia hakuna tofauti na shabiki la soccer alieweka matarajio ya ushindi kwa timu yake na mwisho wa siku inanwangusha. Ushauri kwa timu ya Taifa ya Tanzania hasa kwa kufuata kauli mbiu ya sasa ni kazi katika kulijenga taifa waingie sokoni kutafuta kocha wa maana wa kiwango cha kimataifa hata kama atakuwa kocha wa kulipwa zaidi kama anauwezo na kutudhalishia maprofessionals wengi watakaokwenda kucheza nje ya nchi basi nchi itakuwa imejilipa tena pengine mara nyingi zaidi ya gharama ya kocha. Viongozi husika wanatakiwa kuona mbele zaidi na kutokukubali kukaa pale pale miaka nenda miaka rudi kwa kweli vitu vinavyomfehesha na kukatusha tamaa kwa watanzania.