ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 25, 2015

Usiri wazidi kutawala mwafaka Zanzibar, Dk. Shein, Maalim Seif wajichimbia mara ya tatu

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

MAZUNGUMZO ya kutafuta mwafaka wa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, yameendelea kufanyika jana Ikulu mjini Unguja, Zanzibar.

Kikao hicho cha tatu kilikuwa chini ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kikimshirikisha aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais.

Chanzo cha kuaminika kutoka Ikulu mjini Unguja, kililiambia MTANZANIA jana kuwa pamoja na kuwakutanisha mahasimu hao wa kisiasa wa vyama vya CCM na CUF, pia kimehudhuriwa na wajumbe ambao ni marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Matokeo ya mazungumzo hayo yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kupitia Mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha, kutoa tamko la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka huu jambo ambalo liliibua mgogoro wa kikatiba.

Novemba 9, mwaka huu, mawaziri sita wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kutoka katika Chama cha Wananchi (CUF), walijiuzulu kutokana na msuguano wa kisiasa visiwani humo.

Aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakar Khamis Bakary, alitoa taarifa ya kujiuzulu kwa mawaziri hao mbele ya waandishi wa habari mjini Unguja ambapo alieleza kuwa kila waziri na manaibu wao wamekabidhi magari ya Serikali pamoja na vifaa vingine kwa mamlaka.

Alisema kuwa wamechukua hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha (28) cha Katiba ya Zanzibar, ambacho kinaeleza umiliki wa ofisi kwa ajili ya wote akiwamo na Rais Dk. Shein na mawaziri kumalizika Novemba 2, mwaka huu.

Mawaziri waliojiuzulu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabibu Fereji, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji, Waziri wa Afya, Rashid Suleiman na Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdillah Jihadi.

Wengine waliojiuzulu ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi na Nyumba, Maji na Nishati, Haji Mwandani Makame, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Zahara Ali Hamed na Naibu Waziri wa Kilimo Maliasili, Mtumwa Kheir Mbarak.

Alipotafutwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ili kupata ufafanuzi wa mazungumzo hayo, alisema hadi sasa mazungumzo hayo bado ni siri kubwa, hata viongozi wa ndani wa chama chake, hawafahamu kinachoendelea tangu viongozi hao wa kitaifa walipoanza kukutana.

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar umekuwa ukichukua sura tofauti, ambapo wiki iliyopita Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza walifanya maandamano na kuitaka nchi hiyo iingilie kati na kutoa shinikizo kwa Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha mshindi wa uchaguzi wa rais wa Zanzibar anatangazwa na kuapishwa.

Maandamano hayo yamekuja kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo huku akitoa sababu tisa zilizobainika ikiwamo kuchezewa kwa matokeo katika Kisiwa cha Pemba na uchaguzi kutokuwa huru na haki.

Wazanzibari hao wanaiishi nchini Uingereza, walifanya maandamano hayo ambayo yaliishia katika Mtaa wa Downing zilipo ofisi za Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na kukabidhi barua yao.

Wakati vikao hivyo vya siri vya kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa visiwani Zanzibar vikiendelea, juhudi za kuupatia ufumbuzi mzozo huo zimehamia kutoka Ikulu ya Zanzibar na kufika Ikulu ya Marekani (White House).

Wazanzibari wanaoishi Marekani waliandamana hadi Ikulu ya nchi hiyo, ikiwa ni juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa ili kuupatia suluhisho mzozo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi mbele ya Ikulu hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari waishio Marekani (ZADIA), iliyoandaa maandamano hayo, Omar Haji Ali, alisema kuwa maandamano hayo yanakuja katika juhudi zao za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa katika kuukwamua mgando wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Alisema kwamba maandamno hayo pia yana lengo la kumkumbusha Rais Barack Obama wa Marekani kutekeleza ahadi yake ya kuilinda demokrasia barani Afrika.

Tangu kufutwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi, mataifa kadhaa ya nje yamekuwa yakiingilia hatua hiyo ikiwamo Serikali ya Marekani na kutaka tamko hilo liondolewe.

Serikali ya Marekani ilisema imeshtushwa sana na tamko la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, la kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

MTANZANIA

No comments: