Profesa Muhongo ameagiza Shirika la Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme kuanzia Januari.
Amewataka wakurugenzi wa mashirika hayo, kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei hiyo kutokana na kupungua kwa gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta.
Profesa Muhongo alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, baada ya kumaliza kikao kilichokaa kwa zaidi ya saa tano kati yake na watendaji wa wizara hiyo na mashirika hayo.
Miongoni mwa walioshiriki kikao hicho ni Naibu Waziri, Dk Medard Kalemani, Katibu Mkuu Omar Chambo na wakurugenzi wa mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Bei iko juu? Katika kikao hicho, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme haishuki, wakati gharama za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta, zimepungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Upo ukweli kuwa Shilingi yetu imezidi kupoteza thamani na vitu vya umeme vingi vinanunuliwa kwa Dola ya Marekani, lakini ni kwa nini umeme unashindwa kushuka wakati gharama za mafuta zimepungua? “Zamani pipa la mafuta katika soko la dunia lilikuwa ni Dola za Marekani 200, likashuka hadi dola 100 na sasa hivi ni kama dola 35 kwa pipa moja, Tanesco lazima wajue gharama za uzalishaji umeme wa mafuta zimepungua,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema moja ya ahadi za Rais John Magufuli ni kufufua viwanda, lakini haiwezekani kuwa na viwanda vingi, kama gharama za umeme zitakuwa juu kwa kuwa vitashindwa kujiendesha.
Profesa Muhongo alitumia nafasi hiyo kutoa tahadhari kwa yeyote atakayeona hataweza kutimiza majukumu yake ipasavyo, ajue kuwa ataondolewa katika nafasi yake, kwani suala la umeme ni la kufa au kupona.
Likizo Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo amesitisha likizo za wafanyakazi wote wa Tanesco na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo mpaka Februari, 2016 ili watumie muda huo kukabiliana na tatizo linaloonekana kuwa sugu la kukatika kwa umeme.
“Hawataenda likizo kwa sababu tumekubaliana kumaliza hili tatizo, Watanzania wanataka umeme wa uhakika, wamechoka na hii shida ya kukatika kwa umeme, wafanyakazi hawa wamesema wako tayari kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika,” alisema.
Alisema tatizo la kukatika kwa umeme, linaweza kuchangiwa na umeme unaozalishwa kutotosheleza, uchakavu wa mitambo au kuzidiwa, jambo ambalo anataka lifanyiwe kazi, ili kuhakikisha tatizo hilo linamalizika na kuanzia mwakani kunakuwa na umeme wa uhakika.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, hadi kufikia Februari mwakani, mitambo mingi itakuwa imerekebishwa na itakuwa ikifanya kazi vizuri, jambo litakalosaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alisema Serikali inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuwekeza katika sekta ya uzalishaji umeme, ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.
Alisema kuna vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, lakini bado umeme unaozalishwa hautoshi, hivyo wawekezaji wenye uwezo watumie fursa hiyo kuwekeza katika sekta hiyo.
“Ili tufanikiwe kufikia kuwa nchi yenye kipato cha kati kufikia mwaka 2025, ni lazima tuwe na umeme wa kutosha, hivyo tunatarajia hadi kufikia mwaka huo, tuweze kuzalisha megawati 10,000,” alisema.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment