Wakizungumza jana katika semina elekezi kwa wabunge iliyofanyika katika jengo la Millennium Tower jijini Dar es Salaam, wabunge hao walisema kauli ya Serikali juu ya kuanzisha viwanda nchini, haiendani na maelezo yaliyomo katika mapendekezo ya kuanda mpango huo.
Wakati wabunge wakieleza hayo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Honest Ngowi ambaye pia alitoa mada katika semina hiyo, alisema Serikali ni lazima ieleze sababu za viwanda vyake kufa, ianzie hapo kuvifufua ama kujenga vipya.
Katika mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Taifa katika mkutano wa pili wa Bunge la 11, suala la viwanda liliibuka na wabunge waliibana Serikali baada ya mpango huo kutofafanua kwa kina uanzishwaji wa viwanda nchini.
Akizungumza katika semina hiyo iliyohudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea aliitaka Serikali kuanza kueleza sababu za kuua viwanda, kabla ya kueleza mpango wa kuanzisha viwanda vipya.
“Serikali itueleze sababu za viwanda kufa, na ichambue kwa kina kama sababu hizo hazitaweza kuathiri mpango wake wa kuanzisha upya viwanda.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema, “Suala hili la kuanzisha viwanda lipo katika ilani ya CCM, lakini ukiutizama mpango huu hamna kitu kama hicho. Hatujaona nguvu iliyowekwa katika kilimo ili twende sambamba na uanzishaji wa viwanda.”
Lugola ambaye ni makamu mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) alisema, “Watueleze watajenga viwanda gani na wapi? Vitakuwa vingapi na itatugharimu kiasi gani kuvijenga.
Haya yote hatujaelezwa wakati huu ambao tunaelekea katika bajeti ya 2016/ 17. ”
Kwa upande wake mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalali Kafumu alisema, “Sijui tutafanya miujiza gani kufufua viwanda! Nimeishauri Serikali kufanya utafiti kwanza sababu za kufa kwa viwanda kwa sababu huu ni mpango wa siku nyingi sana lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.”
Mbunge wa Bagamoyo (CCM), Dk Shukuru Kawambwa alisema, “Tukitaka kufufua viwanda lazima tujifunze kwa nchi kama China, Singapore, Ufilipino na Malaysia ambazo zilikuwa na uchumi kama wetu ila baada tu ya kuanzisha viwanda zimekua sana.”
Alisema mpango wa Taifa wa maendeleo ni mzuri na kitu pekee kilichobaki ni utekelezaji, kwa maana ya Serikali kueleza nini itafanya ili kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.
Mbunge wa jimbo la Malindi (CUF), Ally Saleh alisema, “Utekelezaji wa mpango kama huu wa miaka mitano iliyopita ni asilimia 53 tu, sasa sijui huu wa miaka mitano ijayo utakuwaje? Serikali ifufue viwanda na si kujenga vipya. Inapaswa kutueleza itavifufuaje.”
Wabunge hao walisema hayo baada ya ofisa kutoka Tume ya Mipango, Kessy Maduka kuelezea mambo ya kuzingatia kufanikisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment