Baadhi ya Eneo la Ekari Tisa za Mikarafuu lililounguzwa Moto na Watu wasiojuilikana hivi karibuni katika Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif AliIddi kati kati akifanya ziara maalum ya kukagua mashamba Matatu ya Mikarafuu ya Ekari Tisa yaliyotiwa Moto na watu wasiljuilikana hivi
Mwakilishi wa Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo na Maliasili Kisiwani Pemba mbae pia ni Afisa Misitu Bwana Idris Hassan Abdulla wa kwanza kutoka kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif juu ya hasara iliyopatikana baada ya kuungua moto miti ya Mikarafuu shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mheshimiwa Omar Khamis Othman.
Mzee Khamis Chande Mkaazi wa Mzambarauni anayeshughulikia Mashamba ya Serikali ya Mikarafuu aliiomba Serikali kupitia Balozi Seif isaidie nguvu za uwezeshaji wa mashamba hayo baada ya kutumia nguvu nyingi za Fedha katika kuyahuisha mashamba hao.
Balozi Seif akiliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliohusika na uchomaji moto mashamba ya Mikarafuu Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Baadhi ya Mikarafuu iliyoungua moto baada ya kuhujumiwa na watu wasiojuilikana huko Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Kisiwani Pemba. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kuendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu waliohusika na tukio la kuchoma moto Mashamba Matatu ya Mikarafuu yenye ukubwa wa Ekari Tisa huko katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema wahusika hao wa kuhujumu uchumi wa Taifa wanapaswa kupambana na mkondo wa dola kutokana na vitendo vyao vinavyorejesha nyuma mbali ya Maendeleo ya Taifa kwa jumla lakini pia kuviza vipato vya Wananchi
wanaotegemea mashamba hayo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo mara baada ya kuyakagua mashamba hayo yaliyopata kadhia hiyo karibu Wiki moja iliyopita na kusababisha hasara yenye thamani inayokisiwa kufikia shilingi Milioni 24, 525,000/-.
Alisema tabia ya baadhi ya watu kuendelea kufanya vitendo vya hujuma kwa kufikiria kwamba wanaikomoa Serikali Kuu waelewe kwamba wanakwenda kinyume na maamrisho ya Dini kwa vile vitendo vya vimekuwa vikileta hasara kwa Wananchi wenzao katika maeneo yao.
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kusimaia ipasavyo udhibiti wa vitendo viovu zinavyoonekana kushamiri katika baadhi ya maeneo vikihusihwa zaidi na itikadi za Kisiasa ambazo hazina msingi wala hatma njema kwa jamii na Taifa kwa pamoja.
Alitahadharisha kwamba zao la Karafu bado linaendelea kuwa muhimili wa Uchumi wa Visiwa vya Zanzibar. Hivyo vitendo vya watu hao vinaashiria wazi vikilenga kuhujumu mapato ya Taifa.
“ Hii ni hujuma iliyofanywa kwa makusudi na watu wasiyoitakia mema nchi yetu hasa ikilinganishwa na mazingira halisi ya mashamba yenyewe ”. Alisema Balozi Seif.
Mapema Mwakilishi wa Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo naMaliasili Kisiwani Pemba ambae pia ni Afisa Misitu Bwana Idris Hassan Abdulla alisema hujuma hiyo imeathiri jumla ya Mikarafuu 151ambapo kati ya hiyo Mikarafuu 36 haitofufuka tena kutokana na moto huo.
Bwana Hassan alisema Mikarafuu 115 katika mashamba hayo Matatu ambayo moja linamilikiwa na Serikali inaweza kuendelea kuzaa karafuu si zaidi ya miaka Mitatu kulingana na hali halisi ya mazingira ya miti hiyo kwa vile ina maji maji ya mafuta.
Alisema ukanda wa Kaskazini ya Kisiwa cha Pemba bado una mashamba mengi ya Serikali yenye mikarafuu ambayo yamekuwa yakihudumiwa na baadhi ya wananchi ambao tayari wameshawasilisha maoni Serikalini kwa
kutaka kumilikishwa rasmi.
Naye Mmoja wa Wananchi wanaosimamia huduma za mashamba hayo Mzee
Khamis Chande aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa mkusaidia nguvu
katika juhudi za kuyaendeleza mashamba hayo kwa vile tayari ameshatumia fedha nyingi katika kuhusisha miti ya Mikarafuu.
Mzee Khamis alisema kutokana na hujuma hiyo ya moto ndani ya mashamba hayo kwa sasa anahitaji msaada wa ziada katika kuona juhudi alizochukuwa za kuyaendeleza mashamba hayo zinaendelea kama kawaida licha ya hujuma hiyo.
Alisema tayari ameshatumia zaidi ya shilingi Milioni Moja na Nusu katika kuyafanyia usafi pamoja na kuotesha miti mipya ya Mikarafuu na ameushukuru Uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, Idara ya Misitu pamoja na Uongozi wa Serikali ya Mkoa huo kwa kumpa mashirikiano
makubwa baada ya kutokea kwa hujuma hizo.
Alisema kitendo hicho kimempa faraja kubwa jambo ambalo aliahidi kuendeleza jitihada hizo baada ya kuelewa faida na umuhimu wa kuimarisha zao la Karafuu ambalo kwa sasa ndio utio wa Mgongo wa Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alimueleza Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Mkoa wake itajipanga katika kuona Eneo hilo linaimarishwa na kurejea katika
haiba yake ya asili.
Mh. Omar alisema mipango hiyo italengwa zaidi kwenye siku ya Mazingita Duniani kwa kuwashirikisha Watendaji wa Taasisi za Maingira, Wanafunzi, Wananchi pamoja na Wakulima washirikia vyema katika upandaji Miti mipya ya Mikarafuu katika eneo hilo lililoathirika kwa moto.
Hadi sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linamshikilia Mtu Mmoja akituhumiwa kuhusika na vitendo vya utiaji Mtoto mashamba hayo ya Mikarafuu Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/2/2016.
No comments:
Post a Comment